Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

#Diwani Aanika Mafanikio Yake Kwa Wananchi Tangu Kumalizika Kwa Uchaguzi Mkuu 2015.


Diwani wa kata ya Marika Asha Milanzi akizungumza wakati wa sherehe zake za kuwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kumchagua.

DIWANI wa kata ya ‪#‎MARIKA‬ Halmashauri ya mji wa ‪#‎MASASI‬ Asha Millanzi hii leo amewashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kumchagua kwa kura nyingi zilizomwezesha kuwa Diwani katika kata hiyo mpya.
‪#‎AIDHA‬ Diwani huyo ametumia siku hiyo kuelezea mafanikio yake katika kutekeleza ‪#‎AHADI‬ alizozitoa wakati wa kampeni,miongoni mwa shughuli za maendeleo alizozifanya mara baada ya uchaguzi mkuu 2015 ni pamoja na:
1.Mchango wa Bati 20 za ujenzi wa shule ya msingi,Mifuko mitano ya saruji pamoja na mifuko 10 ya chokaa katika kijiji cha ‪#‎Machombe‬.
2.Ametekeleza ahadi yake ya kuchangia bati 10 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya kijiji na kuwapatia vijana uwanja wa michezo wenye thamani ya shilingi 320,000/= katika kijiji cha Namatunu.
"ONA AIBU MTOTO WAKO KUKAA CHINI SHULENI...JITOLEE KUTENGENEZA DAWATI...MASASI NI MIMI NA WEWE".


 Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Masasi Kazumari Malilo (Simba wa Yuda) akipokea gwaride la heshima kutoka kwa kikosi cha Green Guard.










Akwilombe Awacharukia Viongozi Mizigo Wa "CCM" Aapa Watakaoshindwa Watafukuzwa Uongozi

 KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe akiwahutubia wananchi na wanachama wa CCM katika kata ya Kamundi Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara hii leo wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa chama hicho miaka 39 iliyopita.


Na Clarence Chilumba, Nanyumbu.
Katibu wa chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe ameapa kuwafukuza kwenye nafasi zao viongozi wa chama hicho mkoani humo wenye tabia ya kuingilia jitihada za serikali ya awamu ya tano katika utoaji wa elimu ya msingi na sekondari bila malipo.

Pia ameweka wazi msimamo wa chama hicho mkoani Mtwara kuwa hakitawabeba viongozi wote mizigo ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea mazingira ambayo hupelekea wananchi kukichukia chama cha mapinduzi.

Aidha ametoa onyo kali kwa wenyeviti wa Halmashauri za wilaya wa chama cha mapinduzi mkoani humo kuwa chama cha mapinduzi hakitasita kumfukuza mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya atakayeshindwa kusimamia sera ya afya kwa wananchi mkoani Mtwara.

Aliyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi (CCM) miaka 39 iliyopita yaliyofanyika kimkoa katika kata ya Kamundi Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani humo.

Alisema baadhi ya viongozi wa chama hicho wamekuwa wakisababisha watendaji wa serikali washindwe kutimiza majukumu yao na kwamba yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo vya hujuma dhidi ya serikali atachukuliwa hatua kali za serikali ikiwa ni pamoja na kuwafukuza uongozi.

Alisema viongozi wa CCM katika ngazi zote mkoani Mtwara wanao wajibu wa kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali walizoziahidi kwa wananchi wakati wa kampeni na kwamba atakayeshindwa ni bora aachie ngazi mwenyewe.

“Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “sasa hapa kazi tu”…hivyo chama cha mapinduzi mkoani Mtwara kamwe hakitawabeba wala kuwaonea haya viongozi wote mizigo wanaorudisha nyuma jitihada za serikali ya awamu ya tano ya kuleta mabadiliko ya kweli.”alisema Akwilombe.

Alisema inashangaza kwa baadhi ya viongozi wenye dhamana kutoka kwenye chama hicho tawala wakiwa kikwazo kwa shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu ambayo amekiri ni changamoto kubwa mkoani Mtwara.

Alisema wananchi mkoani Mtwara wamekuwa wakilalamika kuwa wamekuwa wakiachwa nyuma katika suala la maendeleo ukilinganisha na mikoa mingine kauli ambazo amepinga vikali na kudai kuwa wananchi wa mkoa wa mtwara na kusini kwa ujumla wasitafute mchawi.

Kwa mujibu wa Akwilombe alisema wazazi wa mkoa wa Mtwara wameshindwa kuwekeza kwa watoto wao katika suala la elimu na kwamba kwa miaka mitatu mfululizo mkoa wa Mtwara umekuwa ukifanya vibaya kwenye matokeo ya shule za msingi na sekondari nchini.

“Ndugu zangu mimi ni mzaliwa wa kusini kama nyinyi…leo nimeamua niwaambie ukweli kuwa tuache kulalamika kuwa tumeachwa nyuma kimaendeleo tatizo tunalo wenyewe hatutaki kuwekeza kwenye elimu na badala yake tumebaki kuwarithisha watoto wetu mashamba ya mikorosho”alisema Akwilombe.

Alisema kamwe mikoa ya kusini haiwezi kusogea mbele kimaendeleo kama wazazi na jamii kwa ujumla mkoani humo haitabadilika kwa kuacha kuwekeza urithi wa watoto wao kwa kuwapa mashamba makubwa ya mikorosho vitu ambavyo haviwezi kuleta mabadiliko.

Chama cha mapinduzi mkoani Mtwara kimefanya sherehe za kuzaliwa kwa chama hicho kimkoa katika kata ya Kamundi wilayani Nanyumbu ambayo ni mpya kwa lengo la kuwaeleza wananchi mikakati ya serikali inayoundwa na chama hicho katika kipindi cha miaka mitano ijayo.


 MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Masasi Kazumari Malilo (Simba wa Yuda) akisalimia wananchi wa kata ya Kamundi wilayani Nanyumbu waliojitokeza kwenye kilele cha maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM.
BAADHI ya wanachama wa chama cha Mapinduzi wakicheza kwa furaha wakati wa kilele cha siku ya kuzaliwa kwa chama hicho ambapo mkoa wa Mtwara umeadhimisha katika kata Mpya ya Kamundi iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu.

Nimekuwekea Hapa Picha Za Matukio ya Sherehe za CCM Jimbo La Masasi Hii Leo Wakisherehekea Ushindi wa Chuachua

 Wapenzi na wanachama wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Masasi wakisherehekea ushindi wa mgombea wao wa nafasi ya ubunge jimbo hilo Rashid Chuachua hii leo nje ya ofisi ya CCM wilaya.


 Mbunge mteule wa jimbo la Masasi (CCM) Rashid Chuachua akiongea na wanachama pamoja na wananchi wa jimbo la Masasi nje ya ofisi ya CCM wilaya ya Masasi.
 Rashid Chuachua mbunge mteule wa jimbo la Masasi akiongea na waandishi wa habari ndani ya ofisi ya CCM wilaya ya Masasi kuhusu namna atakavyotekeleza ahadi zake kwa wananchi waliomchagua

Wanachama wa chama cha mapinduzi wakifuatilia sherehe hizo za ushindi wa mgombea wa CCM jimbo la Masasi.

RASHID CHUACHUA (CCM) AIBUKA KIDEDEA UCHAGUZI JIMBO LA MASASI,AMBWAGA KUNDAMBANDA WA CUF

Mbunge mteule wa jimbo la Masasi Rashid Chuachua (kushoto) aliyeshika kitabu cha ilani ya CCM akiombewa kura kwa wananchi wa jimbo la Masasi na katibu wa chama cha mapinduzi mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe (picha ya maktaba).

Na Clarence Chilumba, Masasi.
Mgombea ubunge jimbo la Masasi kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Rashid Chuachua ameibuka kidedea kwa kupata ushindi katika uchaguzi huo mdogo kwa kumshinda mpinzani wake wa karibu kutoka chama cha wananchi (CUF).

Uchaguzi huo mdogo wa ubunge katika jimbo la Masasi umefanyika jana  kutokana na kushindwa kufanyika oktoba 25 baada ya mgombea ubunge wa jimbo hilo kutoka chama cha  NLD Dk.Emmanuel Makaidi kufariki dunia oktoba 15,mwaka huu katika hospitali ya Misheni ya Nyangao mkoani Lindi kutokana na tatizo la shinikizo la damu.

Akitangaza matokeo hayo jana majira ya saa 6:00 usiku msimamizi wa uchaguzi jimbo la Masasi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Masasi Fortunatus Kagoro alisema katika uchaguzi huo jumla ya wananchi 60,598 waliandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Alisema Rashid Chuachua wa chama cha mapinduzi alipata kura 16,597, huku mpinzani wake wa karibu kutoka chama cha wananchi CUF Ismail Makombe (Kundambanda) akipata kura 14,069.

Wagombea wengine ni Mustapha Swalehe wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) aliyepata kura 512,Dkt.Peter Timothy Mrope  wa chama cha ACT- Wazalendo kura 347 huku mgombea wa chama cha NLD akiambulia kura 70 pekee.

Kwa upande wake wakala wa mgombea wa CUF ambaye ni mbunge wa jimbo la Mtwara mjini Maftaha Nachuma alisema mgombea wao ameshindwa kwa kura na kwamba tume ya uchaguzi imetenda haki kwa kuendesha uchaguzi wa uwazi na ukweli  kuanzia kwenye vituo vya upigaji kura hadi kwenye majumuisho ya matokeo.

“Mgombea wetu ameshindwa kwa kura hivyo tunaomba wafuasi wetu waamini hivyo kwani tunachopaswa sasa ni kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020,”alisema Nachuma.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi lililazimika kufyatua risasi hewani na mabomu ya machozi kwa ajili ya kuwatawanya wafuasi wa Ukawa waliokuwa wamekusanyika nje ya ofisi za kutangazia matokeo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokubaliana kwao na matokeo ya uchaguzi huo.




BREAKING NEWS:CCM YAIBUKA KIDEDEA JIMBO LA MASASI,RASHID CHUACHUA AWA MBUNGE MPYA WA JIMBO HILO

Mbunge mpya wa jimbo la Masasi Rashid Chuachua (Kulia) akiombewa kura na mbunge wa jimbo la Iramba Mwigulu Nchemba(picha ya maktaba).

MATOKEO:

1.RASHID CHUACHUA-CCM KURA 16567
2.ISMAIL MAKOMBE(KUNDAMBANDA) CUF KURA 14069
3.MUSTAPHA SWALEHE-CHADEMA KURA 512
4.DK.PETER TIMOTHY MROPE-ACT WAZALENDO KURA 347
5.ANGELUS THOMASI-NLD KURA 70

"SI LAZIMA KUPIGA KURA YA "HAPANA" KWA MTU UNAYEMWAMINI KWENYE UONGOZI WA SIASA" (MBUNGE)

Mbunge wa Jimbo la Ndanda Cesil Mwambe (Chadema) kushoto akipongezwa na mbunge wa jimbo la Lulindi Jerome Bwanausi (CCM)  baada ya uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM kumalizika yaliyompa ushindi Mariam Kasembe.(Picha ya Maktaba).

Na Clarence Chilumba, Masasi.
Mbunge wa jimbo la Ndanda kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) Cesil Mwambe amesema mazoea si sheria katika kufanya maamuzi mbalimbali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Aliyasema hayo wakati anajibu moja ya maswali aliyoulizwa na waandishi wa habari kuwa ni  kwa nini mara nyingi kunapokuwa na mchanganyiko wa vyama vya siasa kwenye baraza la madiwani kunakuwa na kura za hapana wakati wa uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa halmashauri.
Akijibu swali hilo alisema kuwa mazoea sio sheria na kwamba wao lengo lao ni kutengeneza Halmashauri iliyo bora itakayowatumikia wananchi kwenye maeneo mbalimbali waliyoyaahidi wakati wa kampeni.
Alisema  si lazima kupiga kura ya hapana kwa mtu unayemwamini kwa kuwa ana imani na uwezo wa mwenyekiti wa Halmashauri aliyechaguliwa ambapo hakuona sababu ya kupiga kura ya hapana kwa mtu mwenye uwezo wa kutetea maslahi ya wananchi wa wilaya ya Masasi.
Kwa mujibu wa mbunge huyo kijana alisema jukumu la madiwani ni kumsimamia mwenyekiti wa halmashauri na kwamba hakuchaguliwa na wananchi wake kama mwenyekiti bali alichaguliwa kama diwani kutokana na kuaminika kwake kwa wananchi wake waliomchagua.
“Naamini uwezo wa mwenyekiti wa halmashauri aliyechaguliwa na ndio maana nimempa kura yangu ya ndio… lakini haina maana kwamba kila atakachokifanya nitakubaliana nae isipokuwa kwa imani yangu kwake niliona ni bora nikampa kura ya ndio ili nimwelekeze ninachotaka akifanye…
Na kuongeza kuwa “katika kundi la wagombea kuna baadhi ya watu nilikuwa siwaamini na laiti wangepewa nafasi katika jambo hili muhimu mimi ningekataa mara moja na kamwe nisingewapigia kura ya ndio”.alisema mbunge huyo.
Alisema jimbo la Ndanda ni jipya na kwamba linahitaji mtu mwenye uwezo atakayewaunganisha wananchi pamoja na halmashauri yao na kwamba maendeleo ya haraka yanahitajika ili liweze kufanana kama majimbo mengine ya zamani.
Aidha alitoa angalizo kwa madiwani wote wa halmashauri hiyo kuwa wakumbuke kuwa walitoa ahadi kwa wapiga kura wao wakati wa kampeni za uchaguzi na kwamba kwa sasa jukumu lao ni kutimiza kikamilifu ahadi zao walizozitoa.
Alisema yuko tayari kutoa ushirikiano kwa madiwani wote bila kujali vyama vyao katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yao ikiwemo elimu, afya, maji, bei za mazao pamoja na miundo mbinu ya barabara.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri hiyo aliyechaguliwa Juma Satma ambaye ni diwani wa kata ya Chiungutwa aliwashukuru wajumbe kwa kumpa kura zote za ndio na kuwaahidi kutenda haki kwa wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara inaundwa na majimbo mawili ya uchaguzi ya Lulindi na Ndanda ambapo kwa jimbo la Ndanda CCM ilifanikiwa kupata viti 15 kati ya 16 vya madiwani huku chama cha demokrasia na maendeleo Chadema kikifanikiwa kupata diwani mmoja na mbunge.

CCM RUANGWA WAPITISHA JINA LA MWANASIASA MKONGWE NAKUMBYA KUWANIA UENYEKITI WA HALMASHAURI


Na Bashiru Kauchumbe,Ruangwa.
Diwani wa kata ya Mbekenyera Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Rashid Hasani Nakumbya (CCM) amependekezwa kuwa mgombea wa kiti cha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kwenye uchaguzi utakaofanyika baadae mwezi huu.
Katika mchakato huo wa uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa kutoka kwa wagombea ndani ya chama cha mapinduzi wilayani humo  Nakumbya alipata kura  10 na  kuwabwaga vibaya wapinzani wake wa karibu Andrew Chikongwe Diwani wa kata ya Nandagala aliyeambulia kura 6 pekee.
Wengine walioangushwa na kada huyo maarufu katika siasa za Ruangwa ni Elius Nkane aliyepata kura 2 pamoja na Rashidi Mnunduma aliyeambulia kura 1.
Aidha mtifuano mwingine ulikuwa ni kwenye kinyang’anyiro cha kumpata mwana CCM atakayegombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambapo kwa pamoja wajumbe wa kikao hicho walimpitisha kwa kauli moja diwani kijana wa kata ya Nanganga Shabani Kambona aliyepata  kura 12 na kumzidi mpinzani wake Omari Songea diwani wa Kata ya Chibula aliyepata kura 7.

Wateuliwa hao kutoka ndani ya chama cha mapinduzi wilayani Ruangwa watapigiwa kura na wajumbe wa baraza la Madiwani katika mkutano wa uzinduzi wa baraza hilo Disemba 10,2015 kwa kukutanishwa na wagombea kutoka vyama vya CHADEMA pamoja na CUF.


MWIGULU NCHEMBA ANGURUMA MASASI MJINI AVITAKA VYAMA VYA SIASA KUFANYA KAMPENI ZA AMANI.

 Mbunge wa Iramba (CCM) Mwigulu Nchemba akimnadi mgombea wa ubunge jimbo la Masasi Rashid Chuachua jana kwenye viwanja vya Kisiwani mjini Masasi.

Na Clarence Chilumba, Masasi.
Mbunge wa Jimbo la Iramba na aliyekuwa naibu waziri wa wizara ya fedha katika serikali ya awamu ya nne Mwigulu Nchemba amewataka wananchi wa jimbo la Masasi kufanya siasa za amani na utulivu ili waweze kuchagua mbunge sahihi kwa maendeleo ya jimbo la Masasi.

Nchemba aliyasema hayo jana mjini Masasi wakati anawahutubia wanachama pamona na wananchi a jimbo la Masasi kwa ujumla kwenye mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea wa nafasi ya ubunge kupitia CCM Rashid Chuachua.

Mkutano huo wa kampeni ulifanyika kwenye mtaa wa Kisiwani Halmashauri ya mji wa Masasi ambapo alisema Chuachua ana sifa zote za kumwezesha kuwa mwakilishi wao wa jimbo la Masasi na kwamba wasifanye makosa kupeleka bungeni mbunge asiye na sifa za kuwa mwakilishi wa wananchi.

Alisema chama cha mapinduzi kimejipanga kushinda kwenye uchaguzi huo mdogo unaofanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mgombea wa NLD Dk.Emanuel Makaidi ambapo aliwataka wananchi na wanachama wa vyama vya siasa kuacha vitendo vya vurugu wakati wa mikutano ya kampeni na hata siku ya uchaguzi.

 Kwa mujibu wa Nchemba alisema kiongozi bora ni yule anayetoka chama cha mapinduzi hivyo ni vyema wananchi wa jimbo la Masasi wakafanya maamuzi sahihi na yaliyo bora kwa kumchagua mgombea wa CCM Rashid Chuachua.

“Ndugu zangu wana Masasi suala la uwakilishi ni nyeti sana na linahitaji mtu makini mwenye uwezo wa kujenga hoja kwa serikali…mchagueni Chuachua awaletee maendeleo na mabadiliko ya kweli yatakayoendana na kasi ya Rais Dk.John Magufuli”.alisema Nchemba.

Kwa upande wake mgombea ubunge jimbo la Masasi kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Rashid Chuachua aliendelea kuwaomba wananchi wa jimbo la Masasi wamchague kwa kura nyingi ili aweze kutekeleza ahadi mbalimbali alizoziahidi kwao wakati huu wa kampeni.


Baadhi ya Askari wa kikosi cha Green Guard wa chama cha Mapinduzi wilaya ya Masasi wakipiga Push-Up nje ya ofisi ya Chama hicho wilaya ya Masasi tayari kwa mikutano ya kampeni inayoendelea mjini hapa.

MBUNGE WA MTWARA VIJIJINI (CCM) MHESHIMIWA HAWA GHASIA AMUOMBEA KURA RASHID CHUACHUA

Mgombea Ubunge kwa tiketi ya CCM Rashid Chuachua (aliyesimama) kwenye moja ya mikutano yake ya kampeni mjini Masasi (Picha ya maktaba).

Na Clarence Chilumba, Masasi.
MBUNGE wa jimbo la Mtwara vijijiji kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM) Hawa Ghasia ambaye pia alikuwa Waziri wa Tamisemi serikali ya awamu nne amewaomba wakazi wa jimbo la Masasi kumchagua mgombea ubunge wa CCM Rashidi Chuachua kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Ombi hilo alilitoa wilayani humo wakati alipokuwa akiwahutubia
mamia ya wakazi wa jimbo hilo kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo zinazoendelea jimboni hapa, ambapo mkutano huo
ulifanyika kwenye viwanja vya  Terminal Two maarufu uwanja wa fisi  mjini hapa.


Alisema ameamua kuja Masasi kwa lengo la kuwaomba wananchi wa jimbo
la Masasi kwamba siku ya Desemba 20 ambapo uchaguzi mdogo wa kuchagua mbunge wa jimbo hilo unafanyika wamchaguwe mbunge wa chama cha mapinduzi ndiye atakaye weza kumaliza kero zao.


Alisema kwa kuwa kata jumla ya 11 kati ya 14 tayari madiwani wa CCM
wameshinda kwa kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu uliomalizika oktoba
25 hivyo wasikubali kufanya makosa badala yake wamchaguwe mbunge wa chama cha mapinduzi kuwa mbunge wao katika jimbo hilo.


Mbunge huyo aliongeza kuwa anamfahamu Chuachua kuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa katika utendaji kazi hivyo akiwa mbunge wa jimbo la Masasi ataweza kumaliza kero zote ambazo zinawakabili wananchi wa
jimbo hilo.


“Kwakuwa serikali ya CCM awamu ya tano tayari imeshaingia Ikulu basi
nawaombeni wakazi wa jimbo la Masasi msichaguwe mbunge wa upinzani
bali mchaguweni mgombea wa CCM ili aungane na kasi ya Raisi Magufuli
kuleta maendeleo,”alisema Ghasia


Kwa upande wake mgombea huyo wa CCM Chuachua alisema iwapo wananchi hao wakimchaguwa kuwa mbunge wa jimbo la Masasi atahakikisha anafufua kiwanda cha kubangua korosho kilichopo wilayani Masasi ili kutoa fursa za ajira kwa wakazi hao.


Aidha mgombea huyo aliongeza kwamba atasimamia ipasavyo bei ya zao la
korosho kwa wakulima ili waweze kunufaika na kilimo hicho ambacho ni
nyenzo kuu ya maisha kwa wakazi wa mikoa ya kusini.

“Nawaombeni kura zenu ili niwe mbuge wa jimbo hili nawaahidi
nitamaliza kero zenu zote naowambeni tena nichaguweni mimi nitakuwa
mkombozi wa jimbo la Masasi,”alisema Chuachua


Chuachua alisema akiwa mbunge wa jimbo hilo atasimamia pia mapato ya
ndani ya halmashauri yaweze kutumika kwa ajili ya kuwaletea maendeleo
wananchi na kusisitiza kwamba suala la rushwa kwenye halmashauri
atalishughulikia kikamilifu.




VIGOGO WANNE WAJITOSA KATIKA KINYANG'ANYIRO CHA KUTAFUTA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA MJI WA MASASI

Baraza la madiwani la halmashauri ya mji wa Masasi lililomaliza muda wake (Picha ya Maktaba).

Na Clarence Chilumba, Masasi.
Makada wanne kutoka chama cha mapinduzi wilayani Masasi wamejitosa katika kinyang’anyiro cha kumpata mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara.
Katibu msaidizi wa chama hicho wilayani humo Ajali Mpataga aliiambia Blog ya Mtazamo Mpya leo kuwa waliochukua fomu na kufanikiwa kuzirejesha ni pamoja na diwani wa kata ya Mumbaka Nikwanya H.Sadiki na Philemoni Millanzi diwani wa kata ya Migongo.

Wengine ni aliyekuwa makamu mwenyekiti katika baraza lililopita la madiwani la halmashauri hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Temeke Selemani Uledi Nivako pamoja na diwani wa kata mpya ya Napupa Sospeter Nachunga.

Mpataga alisema wagombea hao watapigiwa kura na madiwani wenzao kutoka kwenye Halamshauri hiyo yenye jumla ya madiwani 18 huku kati yao 14 ni wa kuchaguliwa na wanne ni wale wa viti maalumu ambao wote wameteuliwa kutoka chama cha mapinduzi.

Alisema uchaguzi huo utafanyika siku moja kabla ya tarehe ya kuapishwa na kuanza rasmi kwa baraza jipya la Madiwani ambapo alisema kuwa hadi sasa bado wanasubiri mwongozo ni lini madiwani hao wataapishwa tayari kuanza kazi.

Katika hatua nyingine katibu huyo msaidizi wa CCM wilaya ya Masasi Ajali Mpataga aliiambia blog ya mtazamo mpya kuwa kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi tayari wanachama wawili wamechukua fomu kuomba nafasi ya kuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Aliwataja wanachama hao kuwa ni Juma Satma aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la madiwani lililopita ambaye pia ni diwani wa kata ya Chiungutwa pamoja na diwani mpya wa kata ya Mwena Nestory Chilumba.

Alisema wanatarajia kupata wenyeviti bora na wazuri kutoka kwenye halmashauri zote mbili zinazounda wilaya ya Masasi watakaoendana na kasi ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli.


MGOMBEA UBUNGE AHAIDI KUJENGA STENDI MPYA NA YA KISASA MJI WA MASASI ENDAPO WATAMCHAGUA.

Katibu wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe akimnadi mgombea wa ubunge jimbo la Masasi Rashid Chuachua.

Na Clarence Chilumba, Masasi.
MGOMBEA wa nafasi ya ubunge kupitia chama cha mapinduzi (CCM) jimbo la Masasi Rashid Chuachua amewaahidi wananchi wa mji wa Masasi na viunga vyake kuwa endapo watampa ridhaa ya kuwa mbunge wao atajenga stendi mpya ya mabasi katika mji huo.

Uchaguzi huo mdogo wa ubunge katika jimbo la Masasi unatarajia kufanyika Disemba 20 mwaka huu kutokana na kushindwa kufanyika oktoba 25 baada ya mgombea ubunge wa chama cha NLD Dk.Emanuel John Makaidi kufariki dunia oktoba 15 katika hospitali ya misheni ya Nyangao mkoani Lindi kutokana na tatizo la shinikizo la damu.
.

Aidha amewaomba wamchague ili aweze kuboresha sekta ya kilimo kwa kurasimisha ardhi ya wakulima waweze kupata hati za kimila zitakazowawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha.

Akihutubia leo  maelfu ya wananchi wa jimbo la Masasi wakati wa mkutano wa kampeni za chama hicho  zilizofanyika katika viwanja vya Terminal two (Uwanja wa Fisi) mjini humo  alisema anafahamu kero walizonazo wananchi wa jimbo la Masasi ikiwemo stendi kuu ya mabasi ambayo haina hadhi ya mji wa Masasi.

Amesema uwepo wa stendi kuu ya mabasi ya kisasa kutaongeza mapato kwa halmashauri kutokana na kodi kutoka kwa wafanyabiashara na wamiliki wa mabasi hayo watakaolaza mabasi yao ndani ya stendi hiyo.

Kwa mujibu wa mgombea huyo alisema endapo wananchi wa jimbo la Masasi watampa ridhaa hiyo ya kuwa mbunge wao atashirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje katika kufanikisha ujenzi wa stendi mpya na ya kisasa.

“Ndugu zangu kwa sasa mji wetu wa Masasi hauna stendi ya kisasa inayoendana na hadhi ya mji wetu…hivyo nawaomba ifikapo desemba 20 mnipe kura nyingi za ndio ili niweze kutekeleza kwa vitendo ahadi zangu ikiwemo hii ya stendi”.alisema Chuachua.

Akizungumzia kuhusu  taarifa zinazosambazwa na wapinzani wake kuwa yeye si mzaliwa wa wilaya ya Masasi alisema,wananchi wasipotoshwe na uvumi huo na kwamba yeye ni mzaliwa wa wilaya ya Masasi huku akiwataka wananchi kumpinga kiongozi anayetaka kuchaguliwa kwa kigezo cha ukabila,udini na ukanda.

Pia amehaidi kushughulikia matatizo ya watumishi wa sekta ya afya ambao wamekuwa wakishindwa kupewa stahili zao kwa wakati licha ya umuhimu wa kazi yao kwa jamii huku akiweka wazi dhamira yake ya kuwa mbunge mwenye nia thabiti ya kupambana na umaskini.

Mkutano huo wa kampeni ni mwendelezo wa harakati za kampeni zilizoanza kutimua vumbi Novemba 15 mwaka huu na zinatarajiwa kukamilika Desemba 19 ambapo katika mkutano huo wa leo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwemo mbunge wa jimbo la Mtwara Vijijini Hawa Ghasia.

MATUKIO KATIKA PICHA YA SHEREHE ZA KUMUAPISHA WAZIRI MKUU MPYA MHESHIMIWA MAJALIWA K.MAJALIWA.

 Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, akimpongezwa na mkewe baada ya kuapishwa rasmi leo kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma, leo Nov 20, 2015.

 Rais Dkt. John Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wake, Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto) na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, baada ya kuapishwa Waziri huyo Mkuu kwenye Viwanja vya Ikulu Ndogo Chamwino mjini Dodoma leo.

 Rais Dkt. John Pombe Magufuli, akimwapisha Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa awamu ya tano, wakati wa sherehe hizo zilizofanyika leo Nov 20, 2015 kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma.

 Rais Dkt. John Pombe Magufuli, akimkabidhi nyaraka za Serikali baada ya kumwapisha Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa awamu ya tano, wakati wa sherehe hizo zilizofanyika leo Nov 20, 2015 kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimpongeza Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa baada ya kuapishwa rasmi leo kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma, leo Nov 20, 2015.

 Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimpongeza Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa baada ya kuapishwa rasmi leo kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma, leo Nov 20, 2015.aliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na mtoto Majaliwa mtoto wa Waziri Mkuu mpya kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.aliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

WANANCHI MASASI WAPONGEZA HOTUBA YA DK.JOHN MAGUFULI,WENGI WAMFANANISHA NA NABII MUSA.

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli.

Na Clarence Chilumba,Masasi.
Wananchi wilayani Masasi mkoani Mtwara wameimwagia sifa hotuba iliyotolewa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli wakidai imesheheni matumaini mapya kwa watanzania wa kipato cha chini.

Hotuba hiyo ameitoa hii leo bungeni mjini Dodoma ikiwa ni hotuba yake ya kwanza ambayo ni rasmi kuitoa tangu aapishwe kuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Novemba 5 mwaka huu.

Wakizumgumza na blog ya mtazamo mpya hii leo mara baada ya hotuba hiyo kumalizika wananchi hao walisema wana imani kubwa na Rais Magufuli kwa kuwa ameonesha wazi kuwa anayo dhamira ya dhati kutoka moyoni mwake ya kuwakomboa watanzania.

Kassian Ashapira mkazi wa mji wa Masasi alisema hotuba ya Rais Magufuli imeonesha ni kwa namna gani serikali yake ya awamu ya tano itakuwa na kwamba cha msingi kwa sasa ni kwa viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kumuunga mkono.

Alisema wao kama wananchi wa kawaida wamepokea kwa mikono miwili uamuzi wake wa kufuta safari za viongozi nje ya nchi,matumizi ya magari yenye thamani kubwa pamoja na matibabu ya nje kwa viongozi wa serikali yanayopoteza fedha nyingi za serikali.

Kwa mujibu wa Ashapira alisema watanzania kwa sasa wanahitaji kuona viongozi wa kitaifa wakiwa kama Dk.Magufuli ambaye ameonesha wazi kuwa ahadi alizozitoa wakati anaomba ridhaa kwa watanzania ya kuwa Rais zitatekelezwa kwa kiwango kikubwa na kwamba serikali hii ni ya neema kwao.

Kwa upande wake Fatuma Ally mkazi wa mtaa wa matankini mjini Masasi alisema hakuna ubishi kuwa kwa sasa Tanzania imepata kiongozi anayefanana na mwalimu Nyerere,mwenye msimamo na atakayeleta mabadiliko yenye tija kwa watanzania.

Alisema ahadi ya Rais Magufuli ya elimu bure pamoja na kufuta michango yote mashuleni imekuja wakati muafaka kwa kuwa wazazi wamekuwa na mzigo mkubwa wa michango hiyo na kudai kuwa hata hiyo fedha hawajui inafanya kazi gani kwenye shule hizo.

“Binafsi sio mshabiki wa chama chochote ila ukweli ni kwamba nimemfuatilia sana Rais Magufuli alipokuwa anaomba kura wakati wa kampeni…na nikabaini kuwa ni mtu mwenye dhamira ya kutuondolea umaskini na changamoto mbalimbali”alisema Ally.

Naye Ahmad Namtyoka mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kagera Halmashauri ya mji wa Masasi kupitia Chadema amempongeza Dk.Magufuli kwa hotuba yake na kuongeza kuwa imani yake kwake imeongezeka tofauti na hapo awali kwa kuwa mambo aliyoyaahidi wakati wa kampeni ameendelea kuyasisitiza kuwa atatekeleza.

Alisema wao kama viongozi wa kuchaguliwa na wananchi wanaomba nao walipwe mshahara au posho kama ilivyo kwa viongozi wengine kwani wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu huku wakikosa kuwa na vitendea kazi.

Aidha Mbaraka Rajabu alisema alitegemea hotuba ya Rais Magufuli itakuwa na maneno mengi ya kuisifu na kuipongeza serikali ya awamu ya nne lakini imekuwa ni tofauti kwani Dk.Magufuli alitumia muda mwingi wa hotuba yake kueleza atawafanyia nini watanzania kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

Alisema ameipokea kwa mikono miwili hotuba ya Rais Magufuli hasa pale alipowataka wabunge kuacha tofauti zao za itikadi za vyama vyao na badala yake wafanye kazi huku akitoa uhuru kwa wabunge kuikosoa serikali yake pale itakapokosea.
Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top