TANGAZO
Na Chillumba Clarence,Malolo-Ruangwa.
Kila mwaka inapofika mwezi juni baada
ya shule za msingi kufungwa katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi Tz, yenye wenyeji wa asili wa
kabila la Wamwera kunakuwa na mila na desturi ya jando kwa watoto wa kiume na
unyago kwa watoto wa kike ingawa kwa miaka ya hivi karibuni utaratibu huo wa
kufanya shughuli hizo kila mwaka umevurugika na hii ni kutokana na mabadiliko
ya hali ya hewa yanayoambatanana na ukame unaosababisha njaa.
Katika mila na desturi hizo kwa kabila la Wamwera watoto hupelekwa jandoni ambako hupewa elimu ya namna ya kukabiliana na mazingira yao pindi wanaporejea kutoka kwenye mafundisho hayo.
Pichani chini,ni baadhi ya matukio yaliyojiri wakati wa sherehe hizo zilizofanyika Julai 7&8 2015 katika kijiji cha Malolo wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambako maelfu ya wananchi walijitokeza kushiriki shughuli hizo muhimu katika kabila la Wamwera.
WAZAZI na Marafiki wakiwa wamewabeba watoto wao wakielekea Kanisani kwa ajili ya kushiriki misa ya shukrani ya watoto wao baada ya kukaa kwa muda wa mwezi mmoja wakiwa jandoni ambako hufundishwa mambo mbalimbali kuhusu maadili mema.
JENGO ambalo watoto wa kike huwekwa katika kipindi chote
cha unyago maarufu (Chiputu) ambalo hujengwa kwa mabua ya mazao ya mtama au
Mahindi na kuezekwa kwa nyasi watoto hao hukaa katika jengo hilo kwa kipindi
kisichozidi mwezi mmoja kabla ya kuchukuliwa na wazazi wao siku ya kurudi
nyumbani siku ambayo wamwera huiita –Chianguro,siku ambayo hufanyika sherehe
kubwa inayoambatana na burudani za ngoma za asili.
BAADHI ya wazazi wa watoto wakicheza ngoma wakiwa chini
kuashiria furaha isiyo na kifani kurejea nyumbani kwa watoto wao wa kike na
kiume ambapo watoto wa kike huitwa unyago na kwa watoto wa kiume huitwa Jando.
Lengo kuu la mila hizo ni kumpa mtoto elimu ya maisha na mahusiano yake na
jamii inayomzunguka.
JENGO ambalo watoto wa kiume hukaa wakiwa jandoni kwa
kipindi cha mwezi mmoja au zaidi likiwa limeteketezwa kwa moto ikiwa ni ishara
kuwa tayari siku za watoto hao wa kiume kukaa hapo jandoni zimeisha na hatimaye
kurudi nyumbani kukutana nao tena wazazi wao.Sehemu hii wamwera wanaiita-Likuta
na siku jengo hilo linapochomwa moto wamwera huimba wimbo “Amwali….Mwali..kwa…Mwali…Kwa…Mwali…KwaX2..
Kumishonjo Kupile Moto” Tafsiri ya wimbo huo…mwanamke ulikuwa wapi? Tayari kule
jandoni kumeungua moto.
WATOTO waliotoka jandoni wakiogeshwa na ndugu,jamaa na
marafiki siku ambayo huitwa “Chianguro” ambapo baada ya shughuli hiyo ya
kuogeshwa watoto hao huveshwa nguo Mpya kuashiria kuwa tayari wako katika
ulimwengu mpya ambao wanakuwa tofauti kimaadili na watoto wenzao waliowaacha
nyumbani. Katika tukio hilo baadhi ya ndugu hulala chini na watoto hao huwa juu
yao pindi wanapoogeshwa.
WATOTO na Wazazi wakiwa kanisani katika misa ya shukrani
ambayo hufanyika kila mwaka kunapokuwa na shughuli hizo za jando na unyago
katika kanisa katoliki la Mtakatifu Joseph Parokia ya Malolo,Kigango cha
Malolo,Jimbo la Lindi. Baada ya misa hiyo ndipo watoto hutoka nje na kuelekea
uwanjani ambako hufanyika shughuli mbalimbali ikiwemo uchezaji wa ngoma za
asili maarufu Likomanga na Shikundumbwi.
WAZAZI na ndugu wakiwa wamewabeba watoto wao mabegani wakitoka
kanisani wakiwa wamevalishwa nguo mpya na mikononi mwao wakiwa wameshika
miavuli hiyo yote ni ishara kuwa tayari watoto hao wanakuwa wameingia kwenye
furaha ya siku hiyo ya Chianguro.
WAZAZI na ndugu wakiwa wamewabeba watoto wao mabegani wakitoka
kanisani wakiwa wamevalishwa nguo mpya na mikononi mwao wakiwa wameshika
miavuli hiyo yote ni ishara kuwa tayari watoto hao wanakuwa wameingia kwenye
furaha ya siku hiyo ya Chianguro.
WAZAZI wakicheza kwa furaha wakiwa kwenye uwanja ambao
huandaliwa kwa shughuli hiyo na mara baada ya sherehe za hapo uwanjani (Luwala)
watoto hao hupelekwa nyumbani ambako nako sherehe hizo huendelea kufanyika.
WATOTO hao wakiwa wamebebwa mabegani mwa wazazi wao tayari
kupelekwa nyumbani kwao kwa ajili ya kuendelea na sherehe zingine katika kufurahia mila na Desturi za kabila la Wamwera linalopatikana mkoani Lindi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD