TANGAZO
Mbunge mteule wa jimbo la Masasi Rashid Chuachua (kushoto) aliyeshika kitabu cha ilani ya CCM akiombewa kura kwa wananchi wa jimbo la Masasi na katibu wa chama cha mapinduzi mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe (picha ya maktaba).
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Mgombea ubunge jimbo la Masasi kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Rashid
Chuachua ameibuka kidedea kwa kupata ushindi katika uchaguzi huo mdogo kwa
kumshinda mpinzani wake wa karibu kutoka chama cha wananchi (CUF).
Uchaguzi huo mdogo wa ubunge katika jimbo la Masasi umefanyika jana kutokana na kushindwa kufanyika oktoba 25 baada ya mgombea ubunge wa jimbo hilo
kutoka chama cha NLD Dk.Emmanuel Makaidi kufariki dunia oktoba 15,mwaka
huu katika hospitali ya Misheni ya Nyangao mkoani Lindi kutokana na
tatizo la shinikizo la damu.
Akitangaza matokeo hayo jana majira ya saa 6:00 usiku msimamizi wa
uchaguzi jimbo la Masasi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa
Masasi Fortunatus Kagoro alisema katika uchaguzi huo jumla ya wananchi 60,598
waliandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Alisema Rashid Chuachua wa chama cha mapinduzi alipata kura 16,597, huku
mpinzani wake wa karibu kutoka chama cha wananchi CUF Ismail Makombe
(Kundambanda) akipata kura 14,069.
Wagombea wengine ni Mustapha Swalehe wa chama cha demokrasia na
maendeleo (CHADEMA) aliyepata kura 512,Dkt.Peter Timothy Mrope wa chama cha ACT- Wazalendo kura 347 huku
mgombea wa chama cha NLD akiambulia kura 70 pekee.
Kwa upande wake wakala wa mgombea wa CUF ambaye ni mbunge wa jimbo la
Mtwara mjini Maftaha Nachuma alisema mgombea wao ameshindwa kwa kura na kwamba
tume ya uchaguzi imetenda haki kwa kuendesha uchaguzi wa uwazi na ukweli kuanzia kwenye vituo vya upigaji kura hadi
kwenye majumuisho ya matokeo.
“Mgombea wetu ameshindwa kwa kura hivyo tunaomba wafuasi wetu waamini
hivyo kwani tunachopaswa sasa ni kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020,”alisema
Nachuma.
Katika hatua nyingine jeshi la polisi lililazimika kufyatua risasi
hewani na mabomu ya machozi kwa ajili ya kuwatawanya wafuasi wa Ukawa waliokuwa
wamekusanyika nje ya ofisi za kutangazia matokeo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni
kutokubaliana kwao na matokeo ya uchaguzi huo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD