TANGAZO
Katibu mkuu TAMISEMI Jumanne Sagini (Picha ya Maktaba)
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Ufundi imetoa waraka wa elimu kuhusu
elimumsingi bila malipo na kutoa orodha ya shule za msingi 11 za Serikali
ambazo hazihusiki na utoaji wa elimu bure uliotangazwa na Rais John Magufuli.
Elimumsingi inajumuisha elimu ya awali, ya
msingi na sekondari ambayo itaanza Januari mwakani.
Katika Waraka Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 kuhusu
utekelezaji wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, wizara hiyo imetaja
shule hizo kuwa ni Shule ya Msingi Olympio (Dar es Salaam); Shule ya Msingi
Diamond (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Oysterbay (Dar es Salaam); Shule ya
Msingi Iringa (Iringa) na Shule ya Msingi Mkapa (Mbeya).
Nyingine ni Shule ya Msingi Angaza (Mbeya); Shule
ya Msingi Nuru (Mbeya); Shule ya Msingi Lupilisi (Ruvuma); Shule ya Msingi
Tanga (Tanga); Shule ya Msingi Arusha (Arusha) na Shule ya Msingi Kisimani
iliyoko mkoani Arusha.
Wizara hiyo pia imesema waraka huo hauzihusu shule
zinazomilikiwa na mashirika ya umma ama taasisi za umma ambazo zinaendeshwa kwa
taratibu sawa na shule za binafsi.
Katika waraka huo, wizara hiyo imetoa
majukumu yanayotakiwa kufanywa na Wizara hiyo, Tamisemi, wakurugenzi wa
manispaa na halmashauri ya wilaya, wakuu wa shule, bodi za shule, wazazi na
wananchi.
Majukumu ya wazazi na walezi
Kuanzia Januari, wazazi wanatakiwa tu kununua sare
za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu, na
chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.
Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na
kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua
magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni
na wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali; na kukemea na kutoa taarifa
kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimumsingi bila malipo.
Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa
kuendelea kujitolea nguvukazi na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule
zilizoko ndani ya jamii.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi
Katika waraka huo, Wizara ina jukumu la kutenga
fedha za kugharimia utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kulingana
na idadi ya wanafunzi; kutenga fedha kwa ajili ya Uthibiti Ubora wa Shule na
kutenga fedha za kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimumsingi bila
malipo na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi.
Inachotakiwa kufanya Tamisemi Kwa upande wa
Tamisemi, waraka huo unaielekeza wizara hiyo kutoa miongozo ya matumizi ya
fedha za umma kwa wakuu wa shule, kuratibu uandaaji wa mipango na bajeti ili
kupata mipango na bajeti ya taifa kila mwaka inayozingatia mahitaji halisi ya
elimumsingi bila malipo.
Pia Tamisemi inatakiwa kufanya ukaguzi wa ndani,
ufuatiliaji na tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha elimumsingi bila malipo
inatolewa kwa ufanisi na viwango vya ubora inavyostahili.
Kuratibu utoaji mipango na bajeti za ruzuku ya
uendeshaji wa shule ikiwemo ulinzi, umeme, maji na ununuzi wa chaki na karatasi
pamoja na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia.
Kutenga na kutuma fedha shuleni kwa ajili ya
uendeshaji na usimamizi wa mitihani na majaribio mbalimbali shuleni ikiwemo
tathmini endelezi, kununua vitabu, kemikali na vifaa vya maabara, samani
yakiwemo madawati, vifaa vya michezo, matengenezo ya mashine na mitambo pamoja
na kujenga na kukarabati miundombinu ya shule.
Kutenga na kutuma fedha shuleni za kugharimia
wanafunzi wenye mahitaji maalumu waliopo kwenye shule na vitengo vya elimu
maalumu kwa kuwapatia chakula yaani mlo mmoja kwa wanafunzi wa kutwa na milo
mitatu kwa wanafunzi wa bweni pamoja na vifaa na visaidizi.
Wakuu wa shule
Waraka huo unawataka wakuu wa shule kuwapa
maelekezo wazazi kuhusu aina ya vifaa vinavyohitajika mfano rangi ya kitambaa
cha sare ya shule, sare za michezo, idadi na aina ya madaftari watakayotumia
wanafunzi ili wazazi wanunue wenyewe.
Pia wanatakiwa kusimamia na kuhakikisha fedha
inayotolewa na Serikali inatumika kama ilivyokusudiwa kulingana na taratibu za
fedha za Serikali na kutoa takwimu na taarifa sahihi za idadi ya wanafunzi na
mahitaji mengine ya shule.
Kamati au Bodi za Shule
Wizara katika waraka huo inataka kamati za shule
kufuatilia na kusimamia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali ili ziweze
kuleta tija; kuhakikisha kuwa sera, nyaraka, maelekezo na miongozo ya Serikali
inazingatiwa na kutoa ushauri stahiki.
Kuwashirikisha wazazi, walezi, walimu na wanafunzi
katika maamuzi na maazimio ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi na
maendeleo ya shule kwa ujumla.
Pia waraka huo umeainisha majukumu ya walimu ambao
kazi yao kubwa ni kusimamia sera na miongozo ya utoaji wa elimu bure. Wanafunzi
ambao ndio walengwa wakuu wa utoaji wa elimu pia wametakiwa kuhakikisha
wanakuwepo shule katika kipindi chote cha masomo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD