TANGAZO
KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe akiwahutubia wananchi na wanachama wa CCM katika kata ya Kamundi Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara hii leo wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa chama hicho miaka 39 iliyopita.
Na Clarence Chilumba, Nanyumbu.
Katibu wa chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe
ameapa kuwafukuza kwenye nafasi zao viongozi wa chama hicho mkoani humo wenye
tabia ya kuingilia jitihada za serikali ya awamu ya tano katika utoaji wa elimu
ya msingi na sekondari bila malipo.
Pia ameweka wazi msimamo wa chama hicho mkoani Mtwara kuwa
hakitawabeba viongozi wote mizigo ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea
mazingira ambayo hupelekea wananchi kukichukia chama cha mapinduzi.
Aidha ametoa onyo kali kwa wenyeviti wa Halmashauri za wilaya wa
chama cha mapinduzi mkoani humo kuwa chama cha mapinduzi hakitasita kumfukuza
mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya atakayeshindwa kusimamia sera ya afya kwa
wananchi mkoani Mtwara.
Aliyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa
chama cha mapinduzi (CCM) miaka 39 iliyopita yaliyofanyika kimkoa katika kata
ya Kamundi Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani humo.
Alisema baadhi ya viongozi wa chama hicho wamekuwa wakisababisha
watendaji wa serikali washindwe kutimiza majukumu yao na kwamba yeyote
atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo vya hujuma dhidi ya serikali
atachukuliwa hatua kali za serikali ikiwa ni pamoja na kuwafukuza uongozi.
Alisema viongozi wa CCM katika ngazi zote mkoani Mtwara wanao
wajibu wa kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali walizoziahidi
kwa wananchi wakati wa kampeni na kwamba atakayeshindwa ni bora aachie ngazi
mwenyewe.
“Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “sasa hapa kazi tu”…hivyo
chama cha mapinduzi mkoani Mtwara kamwe hakitawabeba wala kuwaonea haya
viongozi wote mizigo wanaorudisha nyuma jitihada za serikali ya awamu ya tano
ya kuleta mabadiliko ya kweli.”alisema Akwilombe.
Alisema inashangaza kwa baadhi ya viongozi wenye dhamana kutoka
kwenye chama hicho tawala wakiwa kikwazo kwa shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo
elimu ambayo amekiri ni changamoto kubwa mkoani Mtwara.
Alisema wananchi mkoani Mtwara wamekuwa wakilalamika kuwa
wamekuwa wakiachwa nyuma katika suala la maendeleo ukilinganisha na mikoa
mingine kauli ambazo amepinga vikali na kudai kuwa wananchi wa mkoa wa mtwara
na kusini kwa ujumla wasitafute mchawi.
Kwa mujibu wa Akwilombe alisema wazazi wa mkoa wa Mtwara
wameshindwa kuwekeza kwa watoto wao katika suala la elimu na kwamba kwa miaka
mitatu mfululizo mkoa wa Mtwara umekuwa ukifanya vibaya kwenye matokeo ya shule
za msingi na sekondari nchini.
“Ndugu zangu mimi ni mzaliwa wa kusini kama nyinyi…leo nimeamua
niwaambie ukweli kuwa tuache kulalamika kuwa tumeachwa nyuma kimaendeleo tatizo
tunalo wenyewe hatutaki kuwekeza kwenye elimu na badala yake tumebaki
kuwarithisha watoto wetu mashamba ya mikorosho”alisema Akwilombe.
Alisema kamwe mikoa ya kusini haiwezi kusogea mbele kimaendeleo
kama wazazi na jamii kwa ujumla mkoani humo haitabadilika kwa kuacha kuwekeza
urithi wa watoto wao kwa kuwapa mashamba makubwa ya mikorosho vitu ambavyo
haviwezi kuleta mabadiliko.
Chama cha mapinduzi mkoani Mtwara kimefanya sherehe za kuzaliwa
kwa chama hicho kimkoa katika kata ya Kamundi wilayani Nanyumbu ambayo ni mpya
kwa lengo la kuwaeleza wananchi mikakati ya serikali inayoundwa na chama hicho
katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Masasi Kazumari Malilo (Simba wa Yuda) akisalimia wananchi wa kata ya Kamundi wilayani Nanyumbu waliojitokeza kwenye kilele cha maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM.
BAADHI ya wanachama wa chama cha Mapinduzi wakicheza kwa furaha wakati wa kilele cha siku ya kuzaliwa kwa chama hicho ambapo mkoa wa Mtwara umeadhimisha katika kata Mpya ya Kamundi iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD