TANGAZO
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli.
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Wananchi wilayani Masasi
mkoani Mtwara wameimwagia sifa hotuba iliyotolewa na Rais wa jamhuri ya
muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli wakidai imesheheni matumaini mapya
kwa watanzania wa kipato cha chini.
Hotuba hiyo ameitoa hii leo
bungeni mjini Dodoma ikiwa ni hotuba yake ya kwanza ambayo ni rasmi kuitoa
tangu aapishwe kuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Novemba 5 mwaka
huu.
Wakizumgumza na blog ya
mtazamo mpya hii leo mara baada ya hotuba hiyo kumalizika wananchi hao walisema
wana imani kubwa na Rais Magufuli kwa kuwa ameonesha wazi kuwa anayo dhamira ya
dhati kutoka moyoni mwake ya kuwakomboa watanzania.
Kassian Ashapira mkazi wa
mji wa Masasi alisema hotuba ya Rais Magufuli imeonesha ni kwa namna gani
serikali yake ya awamu ya tano itakuwa na kwamba cha msingi kwa sasa ni kwa
viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kumuunga mkono.
Alisema wao kama wananchi
wa kawaida wamepokea kwa mikono miwili uamuzi wake wa kufuta safari za viongozi
nje ya nchi,matumizi ya magari yenye thamani kubwa pamoja na matibabu ya nje
kwa viongozi wa serikali yanayopoteza fedha nyingi za serikali.
Kwa mujibu wa Ashapira
alisema watanzania kwa sasa wanahitaji kuona viongozi wa kitaifa wakiwa kama
Dk.Magufuli ambaye ameonesha wazi kuwa ahadi alizozitoa wakati anaomba ridhaa
kwa watanzania ya kuwa Rais zitatekelezwa kwa kiwango kikubwa na kwamba
serikali hii ni ya neema kwao.
Kwa upande wake Fatuma Ally
mkazi wa mtaa wa matankini mjini Masasi alisema hakuna ubishi kuwa kwa sasa
Tanzania imepata kiongozi anayefanana na mwalimu Nyerere,mwenye msimamo na
atakayeleta mabadiliko yenye tija kwa watanzania.
Alisema ahadi ya Rais
Magufuli ya elimu bure pamoja na kufuta michango yote mashuleni imekuja wakati
muafaka kwa kuwa wazazi wamekuwa na mzigo mkubwa wa michango hiyo na kudai kuwa
hata hiyo fedha hawajui inafanya kazi gani kwenye shule hizo.
“Binafsi sio mshabiki wa
chama chochote ila ukweli ni kwamba nimemfuatilia sana Rais Magufuli alipokuwa
anaomba kura wakati wa kampeni…na nikabaini kuwa ni mtu mwenye dhamira ya
kutuondolea umaskini na changamoto mbalimbali”alisema Ally.
Naye Ahmad Namtyoka
mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kagera Halmashauri ya mji wa Masasi kupitia
Chadema amempongeza Dk.Magufuli kwa hotuba yake na kuongeza kuwa imani yake
kwake imeongezeka tofauti na hapo awali kwa kuwa mambo aliyoyaahidi wakati wa
kampeni ameendelea kuyasisitiza kuwa atatekeleza.
Alisema wao kama viongozi
wa kuchaguliwa na wananchi wanaomba nao walipwe mshahara au posho kama ilivyo
kwa viongozi wengine kwani wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu huku
wakikosa kuwa na vitendea kazi.
Aidha Mbaraka Rajabu
alisema alitegemea hotuba ya Rais Magufuli itakuwa na maneno mengi ya kuisifu
na kuipongeza serikali ya awamu ya nne lakini imekuwa ni tofauti kwani
Dk.Magufuli alitumia muda mwingi wa hotuba yake kueleza atawafanyia nini
watanzania kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.
Alisema ameipokea kwa
mikono miwili hotuba ya Rais Magufuli hasa pale alipowataka wabunge kuacha
tofauti zao za itikadi za vyama vyao na badala yake wafanye kazi huku akitoa
uhuru kwa wabunge kuikosoa serikali yake pale itakapokosea.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD