TANGAZO
Na Clarence Chilumba,
Masasi.
Makada wanne kutoka chama
cha mapinduzi wilayani Masasi wamejitosa katika kinyang’anyiro cha kumpata
mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara.
Katibu msaidizi wa chama
hicho wilayani humo Ajali Mpataga aliiambia Blog ya Mtazamo Mpya leo kuwa
waliochukua fomu na kufanikiwa kuzirejesha ni pamoja na diwani wa kata ya
Mumbaka Nikwanya H.Sadiki na Philemoni Millanzi diwani wa kata ya Migongo.
Wengine ni aliyekuwa makamu
mwenyekiti katika baraza lililopita la madiwani la halmashauri hiyo ambaye pia
ni diwani wa kata ya Temeke Selemani Uledi Nivako pamoja na diwani wa kata mpya
ya Napupa Sospeter Nachunga.
Mpataga alisema wagombea
hao watapigiwa kura na madiwani wenzao kutoka kwenye Halamshauri hiyo yenye
jumla ya madiwani 18 huku kati yao 14 ni wa kuchaguliwa na wanne ni wale wa
viti maalumu ambao wote wameteuliwa kutoka chama cha mapinduzi.
Alisema uchaguzi huo
utafanyika siku moja kabla ya tarehe ya kuapishwa na kuanza rasmi kwa baraza
jipya la Madiwani ambapo alisema kuwa hadi sasa bado wanasubiri mwongozo ni
lini madiwani hao wataapishwa tayari kuanza kazi.
Katika hatua nyingine
katibu huyo msaidizi wa CCM wilaya ya Masasi Ajali Mpataga aliiambia blog ya
mtazamo mpya kuwa kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi tayari
wanachama wawili wamechukua fomu kuomba nafasi ya kuwa mwenyekiti wa
halmashauri hiyo.
Aliwataja wanachama hao
kuwa ni Juma Satma aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la madiwani lililopita ambaye
pia ni diwani wa kata ya Chiungutwa pamoja na diwani mpya wa kata ya Mwena
Nestory Chilumba.
Alisema wanatarajia kupata
wenyeviti bora na wazuri kutoka kwenye halmashauri zote mbili zinazounda wilaya
ya Masasi watakaoendana na kasi ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania
Dk.John Magufuli.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD