TANGAZO
Mbunge wa Jimbo la Ndanda Cesil Mwambe (Chadema) kushoto akipongezwa na mbunge wa jimbo la Lulindi Jerome Bwanausi (CCM) baada ya uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM kumalizika yaliyompa ushindi Mariam Kasembe.(Picha ya Maktaba).
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Mbunge wa jimbo la Ndanda kupitia chama cha demokrasia
na maendeleo (Chadema) Cesil Mwambe amesema mazoea si sheria katika kufanya
maamuzi mbalimbali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Aliyasema hayo wakati anajibu moja ya maswali
aliyoulizwa na waandishi wa habari kuwa ni kwa nini mara nyingi kunapokuwa na
mchanganyiko wa vyama vya siasa kwenye baraza la madiwani kunakuwa na kura za
hapana wakati wa uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa halmashauri.
Akijibu swali hilo alisema kuwa mazoea sio sheria na
kwamba wao lengo lao ni kutengeneza Halmashauri iliyo bora itakayowatumikia
wananchi kwenye maeneo mbalimbali waliyoyaahidi wakati wa kampeni.
Alisema si lazima
kupiga kura ya hapana kwa mtu unayemwamini kwa kuwa ana imani na uwezo wa
mwenyekiti wa Halmashauri aliyechaguliwa ambapo hakuona sababu ya kupiga kura
ya hapana kwa mtu mwenye uwezo wa kutetea maslahi ya wananchi wa wilaya ya
Masasi.
Kwa mujibu wa mbunge huyo kijana alisema jukumu la
madiwani ni kumsimamia mwenyekiti wa halmashauri na kwamba hakuchaguliwa na
wananchi wake kama mwenyekiti bali alichaguliwa kama diwani kutokana na
kuaminika kwake kwa wananchi wake waliomchagua.
“Naamini uwezo wa mwenyekiti wa halmashauri aliyechaguliwa
na ndio maana nimempa kura yangu ya ndio… lakini haina maana kwamba kila
atakachokifanya nitakubaliana nae isipokuwa kwa imani yangu kwake niliona ni bora
nikampa kura ya ndio ili nimwelekeze ninachotaka akifanye…
Na kuongeza kuwa “katika kundi la wagombea kuna baadhi
ya watu nilikuwa siwaamini na laiti wangepewa nafasi katika jambo hili muhimu
mimi ningekataa mara moja na kamwe nisingewapigia kura ya ndio”.alisema mbunge
huyo.
Alisema jimbo la Ndanda ni jipya na kwamba linahitaji mtu
mwenye uwezo atakayewaunganisha wananchi pamoja na halmashauri yao na kwamba maendeleo
ya haraka yanahitajika ili liweze kufanana kama majimbo mengine ya zamani.
Aidha alitoa angalizo kwa madiwani wote wa halmashauri
hiyo kuwa wakumbuke kuwa walitoa ahadi kwa wapiga kura wao wakati wa kampeni za
uchaguzi na kwamba kwa sasa jukumu lao ni kutimiza kikamilifu ahadi zao
walizozitoa.
Alisema yuko tayari kutoa ushirikiano kwa madiwani wote
bila kujali vyama vyao katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye
maeneo yao ikiwemo elimu, afya, maji, bei za mazao pamoja na miundo mbinu ya
barabara.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri hiyo
aliyechaguliwa Juma Satma ambaye ni diwani wa kata ya Chiungutwa aliwashukuru
wajumbe kwa kumpa kura zote za ndio na kuwaahidi kutenda haki kwa wote bila
kujali itikadi za vyama vyao.
Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara inaundwa
na majimbo mawili ya uchaguzi ya Lulindi na Ndanda ambapo kwa jimbo la Ndanda CCM
ilifanikiwa kupata viti 15 kati ya 16 vya madiwani huku chama cha demokrasia na
maendeleo Chadema kikifanikiwa kupata diwani mmoja na mbunge.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD