TANGAZO
KAMANDA wa polisi mkoa wa Mtwara Henry Mwaibambe akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu tukio la wafanyabiashara wanne wa madini raia wa Tanzania kuuawa na majambazi nchini Msumbiji.
Na Clarence Chilumba, Mtwara.
WAFANYABIASHARA Wanne raia wa Tanzania wameuawa nchini Msumbiji
watatu kati yao wakipigwa risasi baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa
ni majambazi waliokuwa na silaha za moto na mapanga.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, kamanda wa polisi mkoa wa
Mtwara, Henry Mwaibambe, alisema wafanyabiashara hao wa Dhahabu walivamiwa
wakiwa katika vibanda vyao vya kubadilishia fedha usiku wa Februari Nane mwaka
huu na kisha kushambuliwa kwa risasi na mapanga ambapo baadhi yao walifariki
papo hapo na wengine walifariki baada ya kufikishwa hospitalini.
Alisema waliouawa katika tukio hilo ni Salumu Mfanga (44) mkazi
wa Temeke, Dar es Salaam, Yusuph Twalibu (34) mkazi wa Tanga, Hamisi Mkapila
(40) mkazi wa Morogoro na Mariam Ramadhani mkazi wa Tanga ambaye yeye hakupigwa
risasi isipokuwa alifariki kwa kukosa huduma baada ya kuvunjika mguu wakati
anakimbia kujiokoa.
“Ndugu zao ambao wanaishi kule Msumbiji ndio ambao walikuja hapa
Mtwara na maiti, sasa utaratibu tuliofanya kwa sababu tukio limetokea katika
nchi jirani ya Msumbiji ni kwamba sisi hawa marehemu tuliwapeleka chumba cha
kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa ya Rufaa ya Ligula kwa ajili ya
uchunguzi kwasababu tulipata taarifa kwamba waliuawa na tumethibitisha kwamba
kweli wameuawa na wana majeraha ya risasi na wengine majeraha ya vitu vyenye
ncha kali kama vile panga au visu..” alisema Mwaibambe.
Alisema kutokana na marehemu hao kuwa sio wakazi wa Mtwara,
ilitolewa ruhusa ya kuisafirisha miili yao na baadhi ya ndugu na jamaa ambao
waliipokea miili hiyo kwa ajili ya kuisafirisha mpaka sehemu husika kwa ajili
ya shughuli za mazishi.
“Msumbiji ni majirani zetu, na kwamujibu wa ndugu wa marehemu ni
kwamba tukio lilitokea katika kijiji cha Mtoro, wilaya ya Mtepweshi kwahiyo
tutafanya mawasiliano na wenzetu wa Msumbiji tujue namna gani tukio hili
lilivyo..kwa taarifa ya ndugu wa marehemu ni kwamba jalada kule
limeshafunguliwa, lakini na sisi kwa taratibu zetu tutawasiliana na ngazi ya
mkoa ili tuweze kujua namna gani wenzetu hawa wafanyabiashara tukio hili
limewakuta na kuweza kuuawa..” alisema.
Kwa upande wa ndugu wa marehemu, Doto Ramadhani Mfanga, alisema
marehemu hao walipigwa risasi na wawili kati yao walifariki papo hapo huku
wawili wengine walifariki njiani wakati wakipelekwa hospitalini ambao ni Salumu
Mfanga na Mariam Ramadhani.
Alisema watu hao baada ya kutekeleza mauwaji hayo walifanikiwa
kuchukua fedha ambazo thamani yake ni sh. Milioni 20 zilizokuwa za marehemu
mmoja ambaye ni Salum Ramadhani, pamoja na dhahabu ambazo hazikufahamika ni za
thamani gani.
“Mimi tukio wakati linatokea nilikuwa Nampula, nikapata taarifa
siku ya Jumatatu saa Sita mchana kwamba tuko hapa njiani tunampeleka mjomba
wako hospitalini lakini amefariki wakati tunampeleka hospitalini ndio
wakanielezea mkasa mzima ulivyotokea.” Alisema.
Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya rufaa ya Ligula mkoani hapa,
Dickson Sahini, alipotafutwa kwa ajili ya kuelezea tukio hilo alidai kuwa hana
taarifa hizo na kushindwa kutolea maelezo.
MIILI ya wafanyabiashara hao ikiwa kwenye majeneza tayari kwa kusafirishwa
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MTWARA HENRY MWAIBAMBE
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD