TANGAZO
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara Mohamedi Sinani (picha ya Maktaba)
Na Clarence Chilumba, Masasi
WABUNGE, Madiwani na viongozi wengine wa vyama vya siasa mkoani Mtwara
wameshauriwa kuweka kando itikadi za kisiasa badala yake washikamane katika
kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli katika kuwatumikia wananchi ili kuleta
maendeleo ndani ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Wito huo ulitolewa wilayani Masasi na mwenyekiti wa Chama cha
mapinduzi(CCM) mkoa wa Mtwara,Mohamedi Sinani alipokuwa akiwahutunia mamia ya
wakazi wa wilaya ya Masasi katika sherehe za maadhimisho ya miaka 39 ya
kuzaliwa kwa Chama cha mapinduzi,ambapo wilaya ya Masasi imeamua kuazimisha
jana mjini hapa.
Alisema muda wa kufanyiana masuala ya upinzani wa vyama
umeshakwisha hivyo hakuna sababu kwa viongozi hao wa siasa kuendelea
kutunishiana misuli ya upinzani wa kisasa bali kwa sasa ni kutafakari kuhusu
maendeleo hivyo ni bora kumuunga mkono Rais Magufuli katika kuwatumikia
wananchi kwa ajili kumsaidia kupambana katika kuleta maendeleo.
Sinani alisema kwa sasa uchaguzi umekwisha na Raisi tayari
ameshachaguliwa na wananchi ni vema viongozi hao wakaweka kando itikadi za
kisiasa na kuangalia masilahi ya taifa ambayo hata Dk. Magufuli anayapigania
kwa ajili taifa.
Alisema viongozi wa kisiasa wanayofursa kubwa katika kusukuma
mbele maendeleo hivyo wabunge, madiwani wawe kitu kimoja katika kumunga mkono
Magufuli kuleta maendeleo kwa wananchi.
“Viongozi wa vyama vya siasa wekeni kando itikadi zenu za
kisiasa na tumuunge mkono Raisi Magufuli katika kuwatumikia wananchi kwani
hakuna sababu ya kuendelea kuchukiana kwa mambo ya vyama vya siasa,”alisema
Sinani
Aidha, Sinani aliwahakikishia wakulima wa zao la korosho wa
mikoa ya kanda ya kusini kwamba chama cha mapinduzi kitatekeleza ilani ya chama
hicho kwa kuwawekea wakulima mazingira bora ya soko la zao la korosho ili
wasiwe na tatizo la kuuza korosho zao.
Alisema viongozi vya chama wanatambua kuwa zao la korosho katika
mikoa hiyo ndio nyenzo kuu ya uchumi kwa wakazi wa mikoa ya kanda ya kusini.
Sinani aliongeza kuwa iwapo wakazi wa mkoa wa Mtwara wakitumia
vema fursa zilizowazunguka katika kujiletea maendeleo hata kiwango cha ukuwaji
wa uchumi kuanzia ngazi ya kaya,kijiji kata,wilaya hadi mkoa kwa
ujumla kitapanda na kuondokana na lindi la umasikini.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD