TANGAZO
Na Boppe Kyungu,Mkuranga.
Halmashauri ya Wilaya ya
Mkuranga mkoani Pwani inatarajia kugawa
vyandarua kwa kaya zipatazo 78,000 vilivyotiwa viuatilifu kwa lengo la kupambana
na maambukizi ya ugonjwa hatari wa malaria.
Akizungumza jana kwenye
mafunzo ya uhamasishaji wa ugawaji wa vyandaraua hivyo,mratibu wa wa mpango wa
malaria wilaya ya Mkuranga Elinas Nnko alisema mradi huo ni kampeni ya kitaifa
ya ugawaji wa vyandarua vilivyotiwa viuatilifu wilayani humo lengo ni kupambana
na ugonjwa huo.
Mafunzo hayo yalifanyika
katika kata ya Mbezi wilayani Mkuranga kwa watendaji wa kata,vijiji pamoja na
maofisa afya wa kata hiyo ya Mbezi huku kila kaya ikitarajia kupata vyandarua
viwili hadi vinne kulingana na idadi ya sehemu za kulala za kaya husika.
Alisema kampeni hiyo ni mwendelezo
wa mradi huo ambao ulianza kutekelezwa
mwaka 2009 hadi 2012 kwa kutoa vyandarua kwa watoto walio na umri wa chini ya
miaka mitano na kwamba kwa sasa mradi huo umelenga kutoa vyandarua kwa kaya yote
na unatarajia kukamilika Juni 2016.
“Kampeni hii ni ya kitaifa….na
kwa sasa ni takribani miaka minne imepita
tangu mradi wa awali ulipotekelezwa hivyo kuna umuhimu kwa wananchi kupewa
vyandarua vingine na kwa kuanzia tumeanza kwa kutoa mafunzo kwa kamati za Afya
ya msingi Wilaya (DPHC), watendaji wa
kata, vijiji na maofisa afya wa kata husika”.alisema Nnko.
Alisema baada ya mafunzo hayo yatafuata mafunzo kwa waandikishaji ambayo
yatajumuisha watu wanne kwa kila kijiji na kwamba mara baada ya mafunzo hayo
utafuata uandikishaji ambao utafanyika kwa muda wa siku tano na hatimaye zoezi
la ugawaji wa vyandarua hivyo kwa wananchi litaanza rasmi.
Kwa mujibu wa mratibu huyo
wa Malaria wilaya ya Mkuranga alisema kuwa mradi huo unafadhiliwa na mfuko wa dunia wa kupambana na
magonjwa ya kifua kikuu, UKIMWI na Malaria kwa ushirikiano na Wizara ya Afya,Maendeleo ya jamii,jinsia,wazee
na watoto ambayo imepewa jukumu la kutoa mafunzo kwa ngazi ya Mkoa,wilaya,kata
na vijiji.
Kwa upande wake Ofisa
mtendaji wa kijiji cha Msufini wilayani humo Selemani Kiumbo alisema ziko baadhi ya changamoto ambazo zinaweza
kusababisha zoezi hilo kutofikiwa malengo ikiwa ni pamoja na muda waliopewa wa
uandikishaji kuwa mdogo.
“Siku tano tulizopewa
kuandikisha wananchi wetu hazitoshi…kwa mfano katika kijiji change cha Msufini
kina vitongoji sita na kaya zaidi ya 600 hivyo ni vigumu kumaliza zoezi la
uandikishaji kwa muda uliopangwa”.alisema Kiumbo.
Zaina Shaaban ni ofisa mtendaji
wa kijiji cha Boza ambaye alisema baada ya zoezi la ugawaji wa vyandarua
kukamilika atahakikisha vinatumika ipasavyo kwa kutembelea kaya hadi kaya
ambapo ataomba kuingia sehemu ya malazi kwa
lengo la kujionea kama vinatumika
ilivyokusudiwa.
Nae ofisa tarafa wa tarafa
ya Shungubweni Faidha Salim alisema vyandarua
hivyo vinatolewa bure hivyo ni jukumu la maofisa watendaji wa vijiji, wenyeviti wa vijiji kuandikisha kaya zao ili kila mwananchi apate
mgao huo wa vyandarua.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD