TANGAZO
Naibu Waziri TAMISEMI anayeshughulikia Utawala Bora na Utumishi Mh: Jafo Selemani (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi Mhe: Sospeter Nachunga wakati wa ziara yake aliyoifanya hospitali ya Mkomaindo Masasi.
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Wakati tatizo la maambukizi ya Ukimwi likiongezeka kwa baadhi ya maeneo nchini,
mji wa Masasi mkoani Mtwara kwa kushirikiana na idara ya afya hospitali ya
Mkomaindo imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa kasi ya maambukizi ya ugonjwa
huo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowahi kutolewa na mratibu wa Ukimwi halmashauri
ya mji wa Masasi Sada Mustapha kwenye kilele cha maadhimisho
ya siku ya Ukimwi duniani Desemba 1,2014 katika kijiji cha Mtakuja zilionesha
kuwa kiwango cha maambukizi kiliongezeka kutoka asilimia 6.1 kwa mwaka 2013
hadi asilimia 7.2 kwa mwaka 2014.
Mganga mkuu wa hospitali ya
Mkomaindo Dk.Gaspar Kumalija aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kiwango cha maambukizi ya Ukimwi katika
mji wa Masasi kimeshuka kutoka asilima 7.2 kwa mwaka 2014 hadi asilimia 5.4 kwa
mwaka 2015.
Alisema katika kipindi cha
januari hadi Desemba 2015 jumla ya wananchi 11,219 walijitokeza kupima Ukimwi
kwa hiyari yao na wengine kwa kushauriwa na watoa huduma za afya (PITC) ambapo
kati yao waliokutwa na maambukizi ya Ukimwi ni 612 huku wanaume wakiwa ni 238
na wanawake ni 374.
Alisema wateja
walioandikishwa katika kituo cha kutolea huduma kwa watu wenye maambukizi ya
Virusi vya Ukimwi kati ya mwezi Januari 2015, ni 401 na kwamba walioanzishiwa
dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) katika kipindi hicho ni 427 kati yao
wanawake ni 300 na wanaume ni 127.
“Kwa ujumla kasi ya maambukizi
ya Ukimwi katika mji wa Masasi imepungua… na hii ni kutokana na kuongezeka kwa
idadi ya watoa huduma waliopata mafunzo yanayohusu huduma za Ukimwi (PITC, ART)
pamoja na kupungua kwa unyanyapaa kupitia elimu inayotolewa na waelimishaji
rika ambao wanajitangaza wenyewe kuwa wana VVU”alisema Dk.Kumalija.
Kwa mujibu wa mganga mkuu
wa hospitali hiyo alisema tangu huduma za matibabu kwa wagonjwa
walioathirika na virusi vya Ukimwi (VVU) zianzishwe katika Halmashauri ya mji wa Masasi
jumla ya wateja wote walioandikishwa ni 6935 na kwamba kati yao wateja
wanaotumia ARV ni 4232 huku watoto walio chini ya umri wa miaka 15
walioandikishwa ni 487.
Alisema idara ya afya kwa
kushirikiana na ofisi ya mkurugenzi wa mji wa Masasi kwa nyakati tofauti
imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za
uhamasishaji katika jamii kuhusu umuhimu wa kupima Virusi vya Ukimwi
mapema,kufundisha watoa huduma,usimamizi shirikishi pamoja na usafirishaji wa
sampuli za damu kavu (DBS na CD4).
Aidha alibainisha baadhi ya
changamoto wanazokumbana nazo katika kupambana na kasi ya maambukizi ya Ukimwi
ikiwemo Kuendelea kuwepo kwa watu ambao hawapendi kubadilika kitabia pamoja na
kuwepo kwa matukio mbalimbali ya ngoma za asili na ngoma za vigodoro ambazo ni chanzo cha maambukizi ukimwi kwa wakazi wa mji wa
Masasi.
Halmashauri ya mji wa
Masasi vituo saba vya kutolea huduma,hospitali moja na zahanati nane ambazo
zote kwa pamoja hutoa huduma za upimaji huku vituo sita vikitoa huduma ya
upimaji kwa hiyari,vituo vitatu hutoa huduma ya matunzo na ushirikishwaji wa
wagonjwa wa kifua kikuu na Ukimwi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD