TANGAZO
Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini Maftaha Nachuma (Picha ya Maktaba)
Na Mwandishi Wetu,Mtwara.
Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini
Maftaha Nachuma amesema kuwa kuanzia leo ofisi yake itaanza kutoa vifaa kwa
akina mama wajawazito wote wanaotarajia kujifungua na kuwataka akina mama hao
kufuata utaratibu wa kwenda kujiandikisha kwa watendaji wa mtaa au kijiji ili
kuweza kutimiza masharti ya kupatiwa vifaa hivyo.
Akizungumza leo ofisini kwake na
waandishi wa Habari Mh; Nachuma amesema kuwa ofisi yake imebaini changamoto
nyingi zinazowakabili akina mama wajawazito ikiwemo ya kukosa vifaa salama
ambavyo vinatumika wakati wa kujifungua hali ambayo imemlazimu kulishughulikia
suala hilo mapema kwa kuamua kutoa vifaa hivyo katika ofisi yake.Vifaa ambavyo
vitatolewa na ofisi ya mbunge ni pamoja na Nyembe, Gloves,Pamba, Mikasi,Mabomba
ya Sindano Ndoo na Beseni.
Maftaha amesema kuwa ili kukizi
vigezo vya kuweza kupatiwa vifaa hivyo ni lazima muhusika ajiandikishe katika
ofisi ya mtedaji wa mtaa au kijiji ili kuweza kupata utambulisho wake ambao
utamwezesha kupata vifaa kwa urahisi na kuongeza kuwa zoezi hilo litakuwa
linawahusu wakazi wa jimbo la Mtwara mjini pekee na litakuwa endelevu hadi
mwaka 2020.
Aidha katika hatua nyingine
Mh.Maftaha amewataka wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani kuendelea
kujitokeza na kujiandikisha kwa ajili ya kusoma somo la ziada la kiingereza
ambalo litakuwa linafundishwa na kuratibiwa na ofisi yake kwa lengo la
kuwajengea uwezo wananchi kwa kuzungumza kiingereza ili kuweza kuchangamkia
fursa zinazotokana na rasilimali ya gesi asilia inayopatikana mkoani hapa.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD