TANGAZO
Mmoja wa madiwani walioiomba ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Masasi Philemon Millanzi kusaidia Ofisi za Maofisa Watendaji wa Kata katika Halmashauri hiyo.
Na Hamisi Nasiri, Masasi.
MADIWANI wa halmashauri ya mji Masasi mkoani Mtwara
wameitaka ofisi ya mkurugenzi kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia ofisi za
watendaji wa kata ili watendaji hao waweze kutekeleza majukumu yao bila ya
vikwazo tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo watendaji hao hulazimika kutumia
fedha zao za mifukoni kutekeleza shughuli za kiofisi.
Ombi hilo limetolewa jana na madiwani wa halmashauri hiyo katika
kikao cha baraza la madiwani kilichoketi kwa ajili ya kuwasilisha taarifa za
maendeleo ya kata kwa kipindi cha miezi mitatu Oktoba hadi disemba 2015.
Awali,akiwasilisha taarifa ya kata ya Migongo diwani wa kata
hiyo,Philemon Milanzi alisema kuna haja kwa ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri
hiyo kutenga fedha kwa ajili ya kuzipeleka katika ofisi za watendaji wa kata
ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa fedha zilizopo kwenye ofisi hizo ambazo
zinakwamisha utendaji kazi.
Alisema wapo baadhi ya watendaji wa kata ambao wanalazamika
kutumia fedha zao za mifukoni ili kutoa huduma za kiofisi kutokana na ofisi
hizo kukabiliwa na uhaba wa fedha za kuendeshea shughuli za kiofisi jambo
ambalo wao kama madiwani hawaridhishwi nalo.
“Si vibaya kwa mtendaji wa kata kutumia fedha zake za mfukoni
kwa ajili ya kutekeleza mambo ya ofisi yake lakini…halmashauri pia inawajibu wa
kuziwezesha ofisi hili ili ziweze kujiendesha maana si kila mtendaji wa kata
anauwezo wa kutumia fedha zake mwenyewe,”alisema Milanzi
Naye diwani wa kata ya Temeke Selemani Uledi alieleza kuwa ofisi
za kata zinashindwa kutekeleza baadhi ya shughuli za kimaendeleo kwa kukosa fedha
za uendeshaji hivyo halmashauri ione namna ya kuziwezesha ofisi hizo ili kazi
zinazofanywa na watendaji hao zifikie malengo yake.
Alisema ni mara kadhaa tatizo hilo limekuwa likipigiwa kelele na
madiwani hao katika vikao vilivyopita juu ya kuziwezesha ofisi za kata ili
ziweze kutekeleza majukumu yake ikiwemo kupata huduma ambapo hivi sasa hata
karatasi za kuandikia taarifa mbalimbali zinakosekana hivyo watendaji hao
wanalazimika kununua kwa fedha zao wenyewe.
Aidha, madiwani hao kwa pamoja walionesha kutoridhishwa na mfumo
wa uandishi wa taarifa za maendeleo ya kata uliotumika na watendaji wa kata
zote 14 za halmashauri hiyo na kuhoji kuwa kwa nini unatofautiana.
Walisema ni bora mfumo wa uandishi wa taarifa ukawa wa aina moja
jambo ambalo litarahisisha kuzifanya taariza hizo kuwa katika hali ya kueleweka
kwa urahisi zaidi na kushauri kwamba watendaji hao wa kata wapatiwe mafunzo
maalumu ya uandishi wa taarifa hizo ili katika vikao vinavyokuja waweze
kuandika taarifa zenye ubora.
Madiwani hao waliwaomba watendaji hao wa kata pindi wanapoandaa
taarifa hizo za maendeleo ya kata kuwashirikisha madiwani wao hatua ambayo
itasaidia kupunguza kasoro ambazo zinajitokeza kwenye taarifa hizo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD