TANGAZO
Naibu Waziri Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Seleman Said Jaffo.
Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri Ofisi ya
Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Seleman Said
Jaffo ameziagiza halmashauri zote nchini ambazo bado zinaendelea kukusanya
mapato yake bila ya kutumia mfumo wa kielektroniki ziwe zimefanya hivyo kabla
ya tarehe 10 januari 2016.
Akizungumza na Viongozi
na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi iliyopo Mkoani Dodoma, Mhe.Jaffo
amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha kuwa agizo lake
linatekelezwa na kuhakikisha kuwa mfumo huo unafanyakazi katika idara zote
muhimu za halmashauri ikiwemo Utawala, Afya na Maliasili.
Alisema kuwepo kwa mfumo
huo kutazisaidia halmashauri kuboresha ukusanyaji wa mapato na hivyo kuwa na
ongezeko la fedha kwa ajili ya kutoa huduma muhimu kwa wananchi hasa kuboresha
upatikanaji wa dawa katika zahanati na vituo vya afya vya halmashauri za wilaya.
Mhe.Jaffo aliongeza kuwa
halmashauri zimekuwa zikikusanya mapato kidogo kutokana na kutokuwa na mfumo
sahihi wa ukusanyaji mapato, na hivyo kuchangia mapato mengi kupotea mifukoni
mwa watu. Pia Naibu Waziri alizungumzia kero inayowakabili watumishi wa chini
ambao hawapati mrejesho pindi wanapohitaji huduma mbalimbali katika halmashauri
zao.
Alisema kumekuwa na
mtindo kwa wakuu wa idara na Maafisa wa Halmashauri kutoshughulikia malalamiko
ya watumishi wa chini hasa madai ya likizo za watumishi na kutopandishwa vyeo
katika madaraja mbalimbali, hivyo akatoa agizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri
kwa kushirikiana na Maafisa Utumishi kuhakikisha kuwa kero hiyo inashughulikiwa
.
Alisema endapo ataulizwa
swali bungeni kuhusu kero na malalamiko yanayohusu watumishi kutolipwa madai ya
likizo na kutopandishwa madaraja kwa watumishi wa ngazi za chini hapo nitajua
kuwa Mkurugenzi na Afisa Utumishi wa wa Halmashauri hiyo hatoshi katika nafasi
yake ya utawala.
“Unakuta mtumishi
anafuatilia madai yake muda mrefu bila kupewa mrejesho, na hivyo kukosa muda wa
kuendelea na majukumu yake katika kituo chake cha kazi, nawaagiza maafisa
utumishi kuhakikisha kuwa mnatoa mrejesho ili kuondoa kero hii”alisema Naibu
Waziri.
Kuhusu kutofanyika kwa
Mikutano ya vijiji, Naibu Waziri alisema vijiji vingi nchini tangu kufanyike
uchaguzi wa Serikali za Mitaa takribani mwaka mmoja uliopita havijafanya
mikutano yake na matokeo yake wananchi wanachangishwa fedha lakini hawasomewi
mapato na matumizi ya fedha hizo.
“Nina taarifa kuwa vijiji
vingi havijafanya mikutano toka mwaka jana uchaguzi wa Serikali za Mitaa
ulipofanyika, hivyo naagiza kila kijiji kifanye mikutano yake ili wananchi
wasomewe taarifa za mapato na matumizi”alisema
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Bahi Mhe. Francis Mwonga alimshukuru Naibu Waziri kwa kuwatembelea na
kuahidi kuyatekeleza maagizo mbalimbali yanayoihusu Wilaya yake.
Pia alisema kuwa
changamoto kubwa inayoikabili wilaya hiyo mbali na tatizo la njaa, ni
kukosekana kwa Maji ya uhakika.Mapema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi Bibi
Rachel Chuwa alimweleza Naibu Waziri kuwa Halmashauri inakitegemea kisima
kimoja cha maji ambacho kilichimbwa kutokana na fedha za wafadhili kutoka
shirika la kimataifa la UNDP ambao walichangia shilingi milioni 230 ambapo
serikali kuu iliahidi kuchangia shilingi milioni 680, ambapo licha ya
kufuatilia fedha hizo lakini hadi sasa hawajazipata.
Wilaya ya Bahi
ilianzishwa mwaka 2007 baada ya kugawanywa iliyokuwa Wilaya ya Dodoma vijijini
na mara kwa mara imekuwa ikikabiliwa na tatizo la njaa ambapo kwa mwaka huu
wilaya ina upungufu wa tani 7000 za chakula na hadi sasa wamekwishapokea tani
300 cha chakula cha Msaada kutoka idara ya maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD