TANGAZO
Christopher Lilai,Nachingwea.
Wenyeviti wa vijiji wilayani
Nachingwea,mkoa wa Lindi wameahidiwa neema ya kuanza kupatiwa posho
ya kujikimu kila mwezi ili waweze kutekeleza majukumu yao bila kinyongo huku
wakitakiwa kusimamia ukusanyaji wa Mapato kwenye maeneo yao.
Ahadi hiyo imetolewa kwa nyakati
tofauti na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea,Ahmadi Makoroganya wakati
wa ziara yake anayoifanya kwenye kata mbalimbali ambapo anakutana na wajumbe wa
kamati za maendeleo ya kata na watumishi.
Alisema kuwa upo uwezekano mkubwa wa wenyeviti
hao kupatiwa posho kila mwezi iwapo ukusanyaji wa mapato utasimamiwa kikamilifu
kwa kuziba mianya inayochangia ukwepaji wa mapato.
Alisema baada ya kumaliza ziara hiyo atakuwa na
kikao na wenyeviti hao wa vijiji ili kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wa
changamoto zinazowakabili ikiwemo ya kutopata posho ili kurejesha ari ya
utendaji kwa viongozi hao wa ngazi ya kijamii.
Kauli ya Mwenyekiti huyo ilitokana na kilio cha
wenyeviti hao wa vijiji ambao waliomba wafikiriwe kupatiwa posho kutokana
na majukumu wanayoyafanya ya kila siku.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kipara Mtua,Helena
Mikongoro alisema wenyeviti ndio viongozi wakuu wa vijiji lakini hakuna
wanachokipata hivyo ni rahisi kushawishiwa na watendaji wa vijiji ili
kushirikia na na wakwepa ushuru wa mazao,hivyo ailiomba waanze kupatia posho za
kujikimu kila mwezi.
Aidha alitoa wito kwa viongozi hao na wananchi
kutoa ushirikiano wa kubaini Watendaji wa kata na vijiji wanaoshirikiana na
wafanyabiashara kukwepa ulipaji wa ushuru wa mazao kwenye maeneo yao.
Alisema kuwa serikali imepiga marufuku wafanyabiashara
kununulia mazao mitaani badala yake kununua kwenye vyama vya
msingi lakini watendaji hao kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu wa
idara ya mapato wamekuwa wakiruhusu ununuzi wa mitaani baada ya
kupatiwa fedha na wanunuzi hao.
“Tumepiga marufuku ununuzi wa kutumia Kangomba
mitaani lakini watendaji wanajifanya hawaoni kumbe wameshapatiwa fedha, hii
haitakubalika kabisa”alionya Makoroganya.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo aliwataka watendaji
hao wa kata na vijiji kutoa taarifa kwake iwapo watendaji wa halmashauri
wanaoshughulika na mapato watawalazimisha kuachia magari yanayosafirisha mzao
bila kibali au kulipiwa.
Alibainisha kuwa hali ya ukusanyaji wa mapato
kwenye halmashauri yake si mzuri kwani kwa kipindi cha miezi sita halmashauri
imekusanya asilimia 12.4 na inatokana na usimamaizi mbovu wa ukusanyaji mapato
na kuahidi kuwa kwa kipindi chake cha uongozi atahakikisha anasimamia
ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti nidhamu ya matumizi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD