Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

Wakulima Nachingwea Waiomba Serikali kuwapelekea Pembejeo za Kilimo Mapema

TANGAZO


Na Christopher Lilai,Nachingwea.
Wananchi wilayani Nachingwea wameilalamikia serikali kuchelewesha  pembejeo za ruzuku kwa vocha  ambapo  hadi hivi sasa wakulima hawajafikiwa ikiwa ni  muda wa kupanda mazao mbalimbali hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa kilimo.

Wakitoa kero mbalimbali kwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea,Ahmadi Makoroganya wakati wa  ziara yake kwenye kata walibainisha kuwa ucheleweshaji huo utaathiri mavuno kwani hata pembejeo hizo zikisambazwa hivi sasa zitakuwa hazina manufaa kwani wakulima wengi wameshapanda mazao kwa kutumia mbegu zisizo  na ubora na bila kutumia mbolea ya kupandia .

Mwenyekiti wa kijiji cha Nampemba kata ya Kilimanihewa,Abdalah Kumpunda, alisema kuwa mkakati wa kilimo kwanza unaendana na matumizi ya mbolea na pembejeo za kilimo hivyo amesikitishwa na utaratibu mzima wanaofanyiwa wakulima kwani imekuwa ni mazoea ya serikali kila mwaka kutozifikisha pembejeo za ruzuku  kwa wakati.

“Cha kushangaa wataalamu wa kilimo wanajua ni muda gani wa kupanda  lakini hadi muda huu wakulima hatujapatiwa hizo pembejeo na hata zikipatikana leo hazitakuwa na faida yoyote kwetu”alisema Kumpunda.

Nae Mtendaji wa kijiji cha Nammanga kata ya Ruponda,Mtibuwa Kijazi alisema kuwa serikali imesambaza  vocha  za pembejeo na huku pembejeo zenyewe hazijulikani zitasambazwa lini jambo ambalo linaonesha kutokuwa na umakini na  swala zima la kuwasaidia wakulima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Nachingwea,alikiri kuwa hadi hivi sasa halmashauri yake haijasambaza pembejeo za vocha  na kuwa utaratibu wa kumpata mzabuni atakayesambaza ameshapatikana na kuwa muda wowote mbejeo hizo zitawafikia wakulima.

Makoroganya pia akiri kuwepo na ucheleweshaji wa mchakato mzima wa mpango huo ambao haundani na muda wa kilimo hivyo kuahidi kuwa katika kipindi chake cha uongozi hatahakikisha mchakato mzima wa vocha za pembejeo unaanza mapema ili uendane na msimu wa kilimo tofauti ya inavyofanyika hivi sasa ambapo hauzingatii ratiba ya kilimo.


Mwenyekiti huyo katika ziara yake  alihimiza wakulima kubadili kilimo kwa kutumia mbolea  za kupandia na kukuzia na matumizi ya mbegu bora ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili kuwa na kilimo chenye tija.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top