TANGAZO
Paroko wa Kanisa katoliki parokia ya Masasi,Jimbo la Tunduru Masasi mkoani Mtwara Rev:Dominick Mkapa (Picha ya Maktaba).
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Waumini wa kanisa katoliki wilayani Masasi katika
mkoa wa Mtwara jana waliungana na wakristo wenzao kote duniani katika
maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mwokozi wao yesu kristo miaka 2000 iliyopita.
Akitoa mahubiri wakati wa mkesha wa krismasi paroko
wa kanisa katoliki parokia ya Masasi jimbo la Tunduru Masasi Dominick Mkapa alisema
viongozi waliopewa dhamana na wananchi wanapaswa kutenda haki ili kudumisha
amani iliyopo nchini.
Alisema ili amani iwepo ni vyema wenye mamlaka katika
maeneo mbalimbali ya huduma kwa wananchi wakatenda haki kwa lengo la kuepusha
migogoro isiyo ya lazima inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Alisema kwa sasa kote duniani amani inaelekea
kutoweka kutokana na baadhi ya watu waliopewa dhamana serikalini kujaribu
kutotenda haki kwa maslahi yao binafsi na kwamba hata mji aliozaliwa masiha
Yesu kristo Bethlehem kwa sasa hauna tena amani kutokana na matumizi mabaya ya
madaraka ya watawala.
Kwa mujibu wa paroko huyo aliitaka idara ya mahakama
nchini kuangalia upya namna ya utoaji wa adhabu kwa washtakiwa ambapo alisema
ni muhimu sasa adhabu zinazotolewa ziendane na makosa ya washtakiwa tofauti na
ilivyo sasa ambapo mshtakiwa hupewa adhabu kubwa tofauti na kosa alilotenda.
“Natumia mkesha huu wa Noel katika kutoa wito kwa
mahakama za hapa nchini…zitoe adhabu kulingana na makosa aliyofanya
mshtakiwa,haiwezekani mtu kaiba kuku anafungwa miaka 30 wakati mtu fisadi
aliyepora haki ya wananchi wengi akihukumiwa kifungo cha miezi sita jela”alisema
Mkapa.
Alisema kila mmoja kwa nafasi yake mahali alipo
ikiwemo kanisani,hospitali,ofisi za serikali,shuleni na nyinginezo zitoazo
huduma kwa jamii anapaswa kutenda haki kwa kuwa haki ni zao la amani ambayo ni
fahari ya watanzania.
Alisema waumini wa kanisa hilo wanapaswa kuiga mifano
kadhaa kutoka kwa Rais wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli ikiwemo zoezi la
kufanya usafi nchi nzima na kwamba wao kama waumini jukumu lao ni kuiga mfano
huo kwa kufanya usafi wa kiroho.
Aidha amewataka wazazi kutambua kuwa wana wajibu
mkubwa wa kulea kiroho familia zao kwani ndiko wanakozaliwa watenda maovu pindi
wanapokuwa na kupewa dhamana katika ngazi mbalimbali ikiwemo
ufisadi,rushwa,ukatili pamoja na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na
maadili.
Mkapa alisema waumini wa kanisa hilo waishi kwa
kufuata maisha aliyoishi mkombozi wao yesu kristo na kwamba vitendo vya ukiukwaji
wa maadili vinavyoendelea kushamiri nchini ni ishara kuwa waumini hawana tena hofu ya mungu.
Alisema sikukuu ya Noeli ama krismasi ni wokovu kwa
waumini wa madhehebu ya kikristo hivyo ni vyema wakazishika na kutekeleza amri
kumi za mungu katika kutekeleza shughuli zao za kila siku hapa duniani.
Maadhimisho ya kuzaliwa kwa yesu kristo miaka 200 iliyopita huadhimishwa
na wakristo kote duniani ambayo kwao kristo mwokozi wao huzaliwa upya mioyoni
mwao huku wakiamini kuwa wanapompokea
kupitia adhimisho la ekaristi takatifu nao huzaliwa upya kama wana wa mungu.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD