TANGAZO
Na Christopher Lilai,Liwale.
Mbunge wa jimbo la Liwale mkoani
Lindi,CUF,Zuberi Kuchauka,amewataka wale wote waliovamia maeneo ya huduma za
jamii yakiwemo maeneo ya zahanati na shule kuondoka mara moja.
Agizo hilo amelitoa hivi karibuni alipotembelea
kijiji cha Mpengele,kata ya Makata kukagua eneo la zahanati ambalo
limevamiwa na wafanya biashara huku akiwataka viongozi wenye tabia ya kushiriki
kuhujumu maeneo hayo kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kuchauka ambaye alikuwa kwenye ziara ya kwanza
mara baada ya kuapishwa alisema kila kijiji kilitenga maeneo kwa
ajili ya huduma za kijamii hivyo ni vyema viongozi wakayalinda na
kuhakikisha hayavamiwi kwa maslahi ya mtu binafsi.
“Kila kijiji kina maeneo yametengwa kwa ajili ya
makazi na shughuli za kijamii ni vizuri yakaheshiwa kwa maslahi ya umma na si
maslahi binafsi”alisema Kuchauka.
Alimtaka Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo
kufanya uhakiki wa maeneo yote ya huduma za kijamii yaliyovamiwa ili
hatua zichukuliwa kwa wale watakaobainika wamehusika na ugawaji
kiholela au kuvamia.
Aidha alimtaka Mkurugenzi mtendaji huyo
kuhakikisha maeneo yote ya umma yakiwemo ya mijini na vijijini
yanapimwa na yanapatiwa hati za kumiliki kisheria ili kuepuka migogoro
isiyo na lazima.
Kwenye kijiji cha Mpengele,serikali ya kijiji
hicho umeingia mgororo mkubwa kati yao na mfanyabiashara na mkazi wa
kijiji hicho Kaimu Mkungu ambaye amejenga ndani ya eneo la
zahanati ambapo licha ya kutakiwa kuondoka amekuwa anagomea kwa kudai
kuwa eneo hilo alipatiwa na uongozi wa kijiji hicho tangu mwaka 2006.
Kuchauka pia amemwagiza afisa Mtendaji wa kata
ya Makata,Chande Kilemba kuingilia kati mgogoro huo ili eneo hilo liendelee
kuwa chini ya mmiliki halali ambae ni serikali ya kijiji cha Mpengele.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD