TANGAZO
Katibu mkuu wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi Profesa Sifuni Mchome.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, amesema wizara yake inaandaa mwongozo
utakaotoa maelekezo juu ya muundo, mfumo na utaratibu nyumbufu utakaohakikisha
kuwa ifikapo Januari mwakani, elimu ya msingi inatolewa bila malipo.
Profesa Mchome
aliyasema hayo juzi jioni katika kikao na watendaji wakuu wa taasisi zote na
vyuo vilivyopo chini ya wizara yake katika kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya
Serikali ya Awamu ya Tano. Chini ya Rais John Magufuli, Serikali imetangaza
kuwa kuanzia mwakani itatoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha
nne.
Profesa Mchome
alisisitiza juu ya utekelezaji wa kutoa elimu bure bila kuathiri ubora wa elimu
itakayotolewa na kuziagiza taasisi zinazohusika pamoja na walimu kushughulikia
kero zao katika ngazi mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa nyumba za walimu.
Alisema wizara yake
inatarajia kuongeza uandikishwaji wa watoto wa awali kutoka asilimia 45 mwakani
hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2020. Katika kikao hicho ambacho pia kilijadili
mwelekeo wa Sera na Mipango ya Elimu katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya
Tano, Profesa Mchome alisema wizara inajipanga kuhuisha taratibu za kujiunga na
taasisi zinazotoa elimu msingi na mafunzo katika ngazi mbalimbali.
Profesa Mchome
alitoa vipaumbele elekezi 20 vya utekelezaji katika kuboresha sera na mipango
ya elimu kwa kipindi cha miaka mitano kutoka 2015 hadi 2020. “Wizara ina mpango
wa kuandaa mfumo, muundo na taratibu nyumbufu za kutoa elimu ya awali na elimu
ya msingi bila malipo ili kuongeza uandikishwaji wa watoto wa awali kutoka
asilimia 45 mwaka 2015 hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2020,” alisema Profesa
Mchome.
Aidha, Profesa
Mchome alisisitiza kuhuisha sifa na kutambua sifa zinazohitajika katika mifumo
na taasisi tofauti ili kuongeza udahili ili asilimia 20 ya wahitimu wa elimu ya
msingi wawe wakijiunga na elimu ya sekondari huku asilimia 80 wakiendelea na
mafunzo ya ufundi.
Alisema lengo la
mpango huo ni kuhakikisha kuwa asilimia 70 ya wahitimu hao wanaweza kujiajiri
na kuajiriwa ili kukidhi mahitaji ya soko hasa ikizingatiwa kwamba Serikali ya
Awamu ya Tano imekusudia kupeleka nchi katika uchumi wa viwanda.
Pia aliziagiza
taasisi zilizo chini ya wizara kuhuisha mipango yake kufikia malengo ya uongozi
wa Dk Magufuli ikiwemo kuongeza nafasi za wanafunzi kujiunga na taasisi
mbalimbali na wakati huo huo ubora wa elimu inayotolewa iwe chachu ya
maendeleo.
Alizitaka taasisi
hizo na vyuo kuhakikisha kuwa wanaweka msisitizo katika masomo ya sayansi ili
kuandaa wanasayansi wa kutosha katika kumudu mahitaji ya soko la uchumi wa
viwanda.
Aliviagiza vyuo vya
elimu ya juu kukaa pamoja ili kujadili mahitaji ya kitaifa na kuandaa programu
zitakazokidhi mahitaji hayo na kuitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya
Juu kupitia upya vigezo vya utoaji wa mikopo kulingana na vipaumbele vya
mahitaji ya soko.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD