TANGAZO
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Joseph Magufuli.
Baraza Jipya: Mpango wake ni kuteuwa idadi ndogo ya mawaziri
ambao ni wachapa kazi kama ilivyokuwa katika enzi ya awamu ya kwanza ya hayati
baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
John Magufuli, anatarajiwa kuzifuta wizara 15 kati ya zilizopo sasa na kubaki
na baraza dogo litakalokuwa na wachapakazi makini ili kutimiza dhamira yake ya
kubana matumizi na kuinua maisha ya Watanzania.
Kadhalika, inaelezwa kuwa Dk. Magufuli aliyeahidi kuleta
mabadiliko ya kweli wakati akiomba kura kwa Watanzania kabla ya kuibuka na
ushindi wa asilimia 58.46 dhidi ya wapinzani wake katika uchaguzi mkuu Oktoba
25, sasa yuko mbioni kutangaza baraza lake la mawaziri litakalokuwa na wizara
15, idadi inayofanana kwa kiasi kikubwa na ile ya Baraza la Mawaziri la miaka
ya 1980 lililoundwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa hayati Mwalimu
Julius Nyerere.
Serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, ilimaliza muda
wake Novemba 5, 2015 ikiwa na Wizara 30. Kadhalika, alipoingia kwa mara
ya kwanza mwaka 2005, Rais Kikwete alikuwa na serikali kubwa yenye mawaziri na
naibu wao zaidi ya 60.
Kufikia leo, Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, mwaka 2015,
tayari ameshamteua Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa
serikali yake ya awamu ya tano na Ijumaa iliyopita alizindua rasmi Bunge la 11.
Chanzo kimoja cha uhakika kimeiambia Nipashe jana kuwa hivi
sasa, tayari Rais Magufuli kwa kushirikiana na wasaidizi wake, ameshakamilisha
sehemu kubwa ya mchakato wa kuunda baraza lake la mawaziri na kwamba,
kinachosubiriwa sasa ni kulitangaza wakati wowote kuanzia sasa.
Chanzo hicho kiliambia Nipashe kuwa Dk. Magufuli ambaye
amejichimbia mjini Dodoma tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, anatarajiwa
kutangaza baraza lake dogo la mawaziri wakati wowote kuanzia leo.
Kwa mujibu wa ibara ya 55 (1) ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, mawaziri wanakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri na pia kwa mujibu wa
ibara ya 54, mawaziri huteuliwa na rais baada ya kushauriana na Waziri
Mkuu.
“Kuna mambo madogo bado hayajakamilika… baada ya hapo
Mheshimiwa Rais atalitangaza Baraza la Mawaziri siku yoyote kuanzia leo.
Kimsingi mkakati wake ni kuwa na baraza dogo lenye wizara 15,” kilieleza chanzo
hicho.
Aidha, ilielezwa zaidi kuwa sura kadhaa katika baraza hilo dogo
zitakuwa mpya na kwamba, mawaziri waliokuwamo katika serikali ya awamu ya nne
wana nafasi ndogo ya kuteuliwa katika baraza hilo.
“Kwa kiasi fulani Baraza hili jipya linafanana na lile la
Serikali ya Mwalimu Nyerere miaka ya 1980… lina wizara chache sana, zenye lengo
la kubana matumizi ya serikali lakini likiwa na uhakika wa kuchapa kazi usiku
na mchana ili kutimiza lengo la Rais Magufuli katika kuwaletea maisha bora
Watanzania,” chanzo kiliongeza.
BARAZA LA MAWAZIRI LA NYERERE
Uchunguzi wa Nipashe kupitia vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja
na maandiko mbalimbali, umebaini kuwa iwapo Magufuli ataunda Baraza lake kwa
kuangalia muundo wa Mwalimu Nyerere miaka ya 1980, maana yake baadhi ya wizara
maarufu hazitakuwapo tena kwani zitakuwa miongoni mwa zile 15 zitakazofutwa na
majukumu yake kuhamishiwa katika wizara nyingine za idadi kama hiyo
zitakazosalimika.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa miaka ya 1980, Mwalimu Nyerere
alikuwa na serikali yenye wizara 15; ambazo ni Wizara ya Elimu; Wizara ya
Mipango; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Wizara ya Mambo ya Ndani;
Wizara ya Ujenzi; Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Kazi na Ustawi
wa Jamii.
WQizara nyingine wakati huo ni Wizara ya Habari na Utamaduni;
Wizara ya Afya; Wizara ya Nishati, Madini na Maji; Wizara ya Sheria;
Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha.
CHANZO: NIPASHE.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD