Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

WANANCHI MKOANI LINDI WATAKIWA KUHESHIMU MIPAKA YA ASILI ILI KUPUNGUZA MIGOGORO YA ARDHI

TANGAZO

Na Clarence Chilumba,Lindi.
Migogoro ya mipaka kati ya vijiji vya Mkanga ya kwanza na kijiji cha Kineng’ene, manispaa ya Lindi na wa kijiji cha Muungano halmashauri ya Lindi  imetajwa kuchangiwa na wanasiasa ambao  hawaheshimu mipaka halali iliyopo kwa maslahi ya kisiasa.


Hayo yalibainishwa na viongozi wa vijiji  hivyo walipokutana na timu ya wataalamu toka  Mjumita iliyoongozwa na afisa mradi wa mkuhumi, Exervery Kigosi waliotembelea baadhi ya vijiji vilivyo kwenye majaribio ya mpango wa hifadhi wa mkuhumi hivi karibuni,ambapo waliomba viongozi wanaochaguliwa kuheshimu  mipaka iliyopo ili kuepuka uvunjifu wa amani.


Mwenyekiti wa kijiji cha Mkanga ya kwanza,Mustafa  Abdeleheman alisema kuwa kijiji chake kina mgogoro wa mpaka kati yake na kijiji cha Kineng’ene ambapo uongozi wa kijiji hicho  wamehamisha jiwe la mpaka  la awali na kuliweka ndani ya eneo la kijiji cha Mkanga ya pili na hivi sasa kunafanyika uvunaji haramu wa miti kwa ajili ya mkaa.

 Alibainisha baada ya wananchi wa kijiji cha Kineng’ene kufanya uharibifu mkubwa wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na upasuaji wa mbao wamevamia hadi kwenye kijiji chao ambako wameanza kukata miti kwa ajili ya mkaa na kuwa tatizo hilo linachangiwa na uongozi wa kata hiyo.


“Tatizo la migogoro mingi iliyopo hivi sasa si kwamba watu hawajui mipaka yao bali wanasiasa ndio wanachangia”. alisema Mustafa.


Alisema kuwa baadhi ya viongozi hao ambao ni   Wenyeviti wa vijiji na Madiwani mara wanapochaguliwa huwa hawafuati mipaka iliyowekwa awali na viongozi waliowatangulia hivyo kusababisha migogoro  hasa kwenye vijiji vilivyo kwenye mpango wa utunzaji wa misitu kwa ajili ya
 utunzaji wa hewa ya ukaa (MKUHUMI).


Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Muungano, Juma Njangati ambacho msitu wao wa hifadhi umevamiwa na wakazi wa kijiji cha  Milola alisema  wananchi hao wameweka makazi  ndani ya hifadhi hiyo na kuendesha  shughuli za kilimo kwa kudai kuwa eneo hilo ni la kijiji cha Milola ambapo wameoneshwa na viongozi wa Kijiji.

Kwa upande wake mwanasheria wa taasisi ya wanasheria wanaoshughulikia masuala ya mazingira (LEAT),Irene Fugara aliwatakaviongozi nchini kuheshimu mipaka halali inayofahamika kisheria.


Aidha aliwataka kufuata sheria zilizopo katika kutatua migogoro ya mipaka iliyopo kwani ilibainika kumekuwa na kutozitumia sheria zilizopo na badala yake kuamua mambo hayo kwa kuzingatia uzoefu na kusababisha migogoro hiyo kutomalizika.
 

Irene alibainisha kuwa katika vijiji walivyotembelea vya Likwaya,Muungano,Nandambi,Kiwawa,Milola na Mkanga  ya kwanza walibaini kutofuata sheria ndogo zilizopo kwenye vijiji hivyo katika kuamua mashauri yanayojitokeza yakiwemo ya wanaokamatwa wakiharibu mazingira kwa ukataji haramu wa miti.



TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top