TANGAZO
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi (CCM) Mzee Ramadhani Pole (Kushoto) akimpongeza katibu wa jimbo la Masasi wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Faraji Mangochi (Kulia) mara baada ya kujiunga na CCM hapo jana wakati wa mkutano wa kampeni.
Na Clarence Chilumba,Masasi.
WAKATI pazia la kampeni za ubunge za uchaguzi mdogo katika jimbo
la Masasi mkoani Mtwara zimenduliwa rasmi juzi Chama cha mapindizu
(CCM) kimeanza kampeni zake jana kwa kishindo baada ya katibu wa jimbo
la Masasi wa Chama cha demokrasia na maendeleo Chadema Faraji
Mangochi kukihama Chama hicho na kujiunga na CCM.
Katibu huyo wa Chadema alitangaza azma hiyo ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi jana katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM za kumnadi kwa wananchi mgombea wa Chama hicho,Rashidi Chuachua ambapo mkutano huo ulifanyika katika viwanja vya Nyasa Magengeni mjini hapa.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi kadi yake ya Chadema kwa katibu wa CCM mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe na kukabidhiwa kadi mpya ya Chama cha mapinduzi Mangochi alisema ameamua kukihama Chama hicho baada ya kuona kuwa mipango mingi iliyopo ndani ya chama hicho kamwe haiwezi kuwakomboa wananchi kimaendeleo.
Alisema amekuwa mwanachama wa Chadema kwa zaidi ya miaka mitano na kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo hiyo ya ukatibu wa jimbo la Masasi lakini kwa muda wote huo hajaona mikakati yoyote inayopangwa kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi isipokuwa viongozi kugombania nafasi za uongozi pekee.
“Nilikwenda Chadema kama kijiweni tu siyo kwa mapenzi ya Chama na sasa nimeamua kurudi nyumbani CCM… kuanzia sasa nitashirikiana na viongozi wa CCM ili mbunge wetu ashinde kwa kishindo katika jimbo hili,”alisema Mangochi
Akizungumzia kuhusu uamuzi wa katibu huyo wa Chadema mwenyekiti wa jimbo la Masasi wa Chadema Musa Mwadewa alisema katibu huyo wa Chadema alishafukuzwa uanachama tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu oktoba 25 mwaka huu baada ya kubainika kwamba anatoa siri za Chama na kupeleka ndani ya Chama cha mapinduzi.
“Tulipata taarifa kutoka kwa baadhi ya wanachama wetu kuwa
katibu huyo wa jimbo amekuwa akishiriki mikutano ya kampeni wakati ule wa
uchaguzi mkuu…na baada ya siku tatu kupita tulimuita lakini hakuja lengo likiwa
ni kumyang’anya kadi yetu” alisema Mwadewa na kuongeza kuwa,
“Sisi kama chama hatujaathirika chochote kwani kuhama kwake ni
kutimiza demokrasia ambayo kila mtu anao uhuru wa kujiunga na chama chochote
cha siasa anachokipenda…tunamtakia safari njema na mafanikio huko aendako”.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa CCM wa jimbo la Masasi Chuachua ameendelea kuomba ridhaa kwa wananchi wa jimbo hilo kwa kuahidi kwamba akiwa mbunge atahakikisha anakutana na waziri wa kilimo kumuelezea changamoto za kilimo zilizopo ndani jimbo hilo ili zipatiwe ufumbuzi.
Chuachua alisema jambo lingine ambalo atalifanyia kazi akiwa bungeni ni afya,elimu na mikopo kwa vijana na kwamba katika eneo la mikopo ataishawishi halmashauri kupima viwanja na kuwapatia hati miliki wananchi ili hati hizo wazitumie katika taasisi za fedha kwa ajili kupatiwa mikopo.
Uchaguzi huo mdogo wa ubunge katika jimbo la Masasi unatarajia kufanyika Disemba 20 mwaka huu kutokana na kushindwa kufanyika oktoba 25 baada ya mgombea ubunge wa jimbo hilo wa Chama cha NLD Dk.Emmanuel Makaidi kufariki dunia oktoba 15 katika hospitali ya Misheni ya Nyangao mkoani Lindi kutokana na tatizo la shinikizo la damu.
Katibu wa jimbo la Masasi (CHADEMA) Faraji Mangochi akionesha kadi ya chama chake mbele ya katibu wa CCM mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe wakati wa uzinduzi wa mkutano wa kampeni za chama cha mapinduzi jana mjini Masasi.
Mgombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Masasi kupitia CCM Rashid Chuachua akikumbatiana na aliyekuwa katibu wa jimbo la Masasi CHADEMA Faraji Mangochi baada ya kujiunga na chama cha mapinduzi.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Masasi mzee Kazumari Malilo (Simba wa Yuda) akimpongeza Faraji Mangochi mara baada ya kutangaza kukihama chama cha Chadema na kujiunga na CCM hapo jana kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za nafasi ya ubunge.
Katibu wa CCM mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe akimnadi mgombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Masasi kupitia chama hicho Rashid Chuachua kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika jana kwenye viwanja vya Nyasa Magengeni mjini Masasi.
Kutoka kushoto waliokaa....Katibu wa CCM mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe,Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Masasi Kazumari Malilo na aliyesimama na mgombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Masasi Rashid Chuachua.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD