TANGAZO
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakifanya mazoezi katika Uwanja wa Uhuru jana ikiwa ni matayarisho kwa ajili ya hafla ya kuapishwa kwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli itakayofanyika uwanjani hapo keshokutwa.
Viongozi Wakuu kutoka Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), na wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc),
wamethibitisha kuhudhuria sherehe za kumuapisha Rais Mteule, Dk. John Magufuli
keshokutwa jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Balozi Liberata Mulamula, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Nipashe
kuhusu maandalizi ya kuwapokea wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi
wanaotarajia kuhudhuria sherehe hiyo.
“Mialiko imeshakwenda, lakini mpaka sasa hakuna aliyewasili, ila
tumeshaanza kupokea majibu ya viongozi mbalimbali wa kanda kuwa watafika katika
sherehe hiyo,” alisema Balozi Mulamula.
Alisema nchi jirani kama Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, Kenya, Uganda, zimethibitisha kushiriki sherehe za kumuapisha Dk.
Magufuli. Alisema orodha kamili na idadi ya wageni watakaokuja, bado
haijapatikana, lakini Wizara imeshajiandaa kupokea idadi yoyote ya wageni
watakaokuja.
Alisema licha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kusimamia sherehe hiyo,
lakini Wizara nayo imejipanga katika suala zima la malazi kwa wageni
watakaofika nchini.
Aliongeza kuwa pia wanatarajia kupokea wageni kutoka China, nchi
za Nordic, Marekani na Uholanzi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD