TANGAZO
Mbunge mteule wa jimbo la Lulindi wilayani Masasi Bwanaus Dismas Jerome akionesha fedha alizopewa na wananchama wa chama hicho kata ya Mbuyuni kwa ajili ya kuchukulia Fomu ya kugombea nafasi hiyo ya ubunge.
Na Clarence Chilumba, Lulindi.
Mgombea ubunge jimbo la Lulindi, wilayani Masasi mkoani Mtwara kupitia
chama cha Mapinduzi (CCM) Jerome Bwanausi Dismas ameibuka kidedea kwa kupata
ushindi wa kishindo na huku akimgaragaza kwa mbali mshindani wake wa karibu wa
chama cha NLD.
Akitangaza matokeo hayo jana msimamizi wa uchaguzi jimbo la Lulindi ambaye
pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi Beatrice Dominic alisema
katika uchaguzi huo jumla ya wananchi 59,027 walijitokeza katika zoezi la
kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura huku watu 20,580 sawa na
asilimia 34.87 walijitokeza kupiga kura.
Kura halali katika uchaguzi huo zilikuwa 20,552 na kura zilizoharibika
ni 228 huku idadi ya wapiga kura ikipungua kutokana na wananchi wengi
kutojitokeza kwenye zoezi hilo la upigaji kura.
Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi alisema Jerome Bwanausi Dismas wa
chama cha mapinduzi alipata kura 17,715 sawa na asilimia 87.04, Modesta Ponela
Makaidi wa chama cha NLD alipata kura
1638 sawa na asilimia 8.05.
Wagombea wengine ni Amina Thomas Mshamu wa chama cha wananchi CUF
aliyepata kura 714 sawa asilimia 3.51 na Francis Alexander Ngaweje wa chama cha
ACT- Wazalendo akiambulia kura 285 sawa na asilimia 1.40 ya kura zote halali.
Akizungumzia kuhusu matokeo ya udiwani msimamizi wa uchaguzi wa jimbo
hilo,Dominic alisema kata zote 19 zilizopo katika jimbo hilo katika uchaguzi
huo zilinyakuliwa na chama cha mapinduzi huku mgombea wa chama hicho kwa nafasi
ya urais Dk.John Pombe Magufuli akipata kura 31,603 sawa na asilimia 71.28 katika
uchaguzi uliofanyika oktoba 25, mwaka huu.
Aidha msimamizi wa uchaguzi huo alisema uchaguzi umefanyika kwa amani na
utulivu licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa ambazo zilitatuliwa na ofisi yake
mara moja huku akiwapongeza watendaji wote waliofanikisha zoezi hilo.
Kwa upande wake mbunge mteule wa CCM Bwanausi aliwashukuru wananchi wa
jimbo la Lulindi kwa kumuamini na kumchagua tena kwa awamu ya pili ili aweze
kuendelea kuwatumikia katika kuleta maendeleo ya jimbo hilo.
Alisema anatambua kuwa ana deni kubwa mbele yake kwa wananchi wa jimbo
hilo na kwamba atafanya kazi kufa na kupona katika kuhakikisha wananchi wa
jimbo hilo wanapata maendeleo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD