TANGAZO
Kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo Zito Zuberi Kabwe
KIONGOZI Mkuu wa Chama cha
ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto, amemshauri Rais John Magufuli atekeleze mambo 10
ili kuweka misingi ya mabadiliko nchini, ikiwemo serikali yake kuweka wazi
mikataba yote ya rasilimali za nchi.
Alibainisha mikataba
hiyo kuwa ni pamoja na ile ya mgawanyo wa mapato yanayotokana na uzalishaji
(PSAs) na ya madini (MDAs). Katika taarifa yake aliyoitoa Dar es Salaam jana,
kiongozi huyo alimnukuu aliyekuwa Rais wa Burkina Faso anayeamini katika mrengo
wa kushoto, Thomas Sankara ambaye aliwahi kusema kuwa hakuna mabadiliko yoyote
yanayoweza kufanyika bila kuwa na kiasi kidogo cha uendawazimu.
“Kama alivyowahi
kusema Thomas Sankara, huwezi kufanya mabadiliko ya msingi bila kuwa na kiasi
kidogo cha uendawazimu,” alisema Zitto. Zitto alisema ili Serikali ya Awamu ya
Tano ifanye mabadiliko ya msingi, ni vyema Dk Magufuli akahakikisha kuwa pamoja
na kuweka wazi mikataba, pia anafuta posho za makalio katika mfumo mzima wa
Serikali kama Mpango wa Maendeleo unavyotaka.
Aidha, alisema
Serikali hiyo, pia inaweza kufuta tiketi za ndege daraja la kwanza kwa
watendaji wa Serikali na wanasiasa isipokuwa viongozi kama Rais, Makamu wa Rais
na Waziri Mkuu.
“Ni vyema pia Dk
Mafuguli akafuta matumizi ya mashangingi ambapo tayari taasisi kama Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), imeanza kuonesha mfano,” alisisitiza Zitto ambaye pia ni
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo).
Alisema pia suala
lingine ambalo Rais Magufuli anaweza kulifanya ni kufuta uagizaji wa sukari
kutoka nje na kuanzisha miradi ya miwa ili Tanzania nayo iuze sukari yake nje
ya nchi. Suala la sita, ambalo mbunge huyo wa Kigoma Mjini amelisisitizia kwa
Serikali ya Awamu ya Tano ni kuweka wazi taarifa ya Serikali kuhusu utoroshaji
wa fedha na kufungua mashtaka kwa wahusika mara moja.
“Lakini pia ni vyema
akaipatia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), mamlaka ya kukamata
na kushtaki mtu atakayebainika na kuthibitika kujihusisha na vitendo vya
rushwa,” alisisitiza.
Alisema suala
lingine ni kuhakikisha kila Mtanzania mwenye mali, ahakikishe anathibitisha
namna alivyoipata mali hiyo, na kuhakikisha mali na madeni ya viongozi
yanawekwa wazi kwa umma na wananchi waruhusiwe kuhoji.
Kutokana na hali
uchaguzi ilivyo Zanzibar, mwanasiasa huyo, pia amemshauri Dk Magufuli, kuruhusu
mshindi wa uchaguzi visiwani humo, atangazwe na akubali kufanya naye kazi.
Uchaguzi huo ulifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutokana na
ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.
Pamoja na hayo,
kiongozi huyo pia amemshauri Rais Magufuli, kuanza mchakato wa Katiba kwa
kuanzia alipoishia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba na kuachana na Katiba pendekezwa.
Tayari Rais
Magufuli, ameanza mchakato wa kuleta mabadiliko nchini ambapo katika muda
mchache, aliokaa Ikulu, amepitia na kufanya ziara za kushtukiza katika maeneo
nyeti, ikiwemo Wizara ya Fedha na kukutana na viongozi wakuu wa Serikali, na
kutoa maagizo yanayohamasisha utendaji wa kasi na kuwaweka pembeni wavivu.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD