TANGAZO
Mwenyekiti wa tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Wananchi wa majimbo ya
Masasi,Ndanda,Nanyumbu na Lulindi mkoani Mtwara hii leo wamejitokeza kwa wingi
kwenye vituo vya kupiga kura ambapo wamefanikiwa kupiga kura kwa amani na
utulivu licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto kwenye vituo mbalimbali ndani
ya majimbo hayo ya uchaguzi.
Wakizungumza na Blog ya Mtazamo Mpya, kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye zoezi hilo la
upigaji kura mapema leo walielezea kuridhishwa kwa namna zoezi hilo lilivyoendeshwa
kwa kuwa vifaa vya upigaji kura vililetwa vituoni kwa muda muafaka na upigaji
kura ulianza saa 1:00 asubuhi kama ilivyoelekezwa na NEC.
Sophia Hamisi (20) mkazi wa
mtaa wa Nyasa kituo cha Nyasa B alisema katika uchaguzi wa mwaka huu kumekuwa
na mwamko mkubwa kwa vijana ambao wamejitokeza kwa wingi katika kushiriki zoezi
hilo muhimu kwa mustakbari kwa Taifa.
Alisema vituo vya kupigia
kura vilifunguliwa kwa muda uliopangwa na tume ya Taifa ya Uchaguzi na kwamba
wamepiga kura kwa amani na utulivu tofauti na awali walivyokuwa wakifikiri juu
ya kutokuwapo na amani katika vituo hivyo vya upigaji kura.
Alisema wasimamizi walifika
kwenye vituo hivyo kwa muda muafaka mara kadhaa walikuwa wakitoa maelekezo ya
jinsi mwananchi anavyotakiwa kupiga kura hali iliyochangia kuwafanya wananchi
wengi walikuwa wamepanga foleni kwa ajili ya zoezi hilo kuweza kupiga kura kwa
usahihi na kwa amani na utulivu.
Nae mkazi wa kata ya Nyasa
kituo cha Nyasa B jimbo la Masasi Jailes Nyamba (21) alisema amepiga kura kwa
amani katika kituo hicho na kusisitiza kwamba suala la kukaa mita 200 baada ya
kupiga kura halina mashiko na ni vema kila mwananchi baada ya kupiga kura
wakaondoka kwenye vituo ili kwenda kuendelea na shughuli zao za kujiingizia
kipato.
Alisema anapinga vikali
suala la wananchi kutaka kukaa mita 200 kwa madai ya kulinda kura na kusema
kuwa ni jambo ambalo linashangaza kwa sababu kama suala la uibaji wa kura
linatokea wanaopaswa kutupiwa lawama ni mawakala wa vyama ambao wao ndiyo
wamepewa dhamana ya kuhesabu na kulinda kura za vyama vyao.
“Awali wakati tunakuja
kwenye vituo vyetu vya kupiga kura tulikuwa na hofu kwamba zoezi hili leo huenda
likagubikwa na vurugu ama vituo kuchelewa kufunguliwa lakini hali haipo hivyo
tumepiga kura kwa amani na utulivu na hakuna changamoto zilizokwamisha upigaji
kura kwa upande wangu,”alisema Nyamba.
Blog ya Mtazamo Mpya pia ilipata
fursa ya kufanya mahojiano na baadhi ya wagombea udiwani wa kata mbalimbali
ndani ya majimbo hayo matatu akiwemo diwani wa kata ya Napupa jimbo la Masasi
Moses Chiwinga (Chadema) ambapo yeye alidai kuwa kwa ujumla uchaguzi umeenda
kwa amani licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa ambazo alikiri kutatuliwa
baadae na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Masasi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD