TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Wananchi wa jimbo la Lulindi,wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara wameshindwa kupiga kura kumchagua
mbunge wao kutokana na hitilafu iliyojitokeza kwenye karatasi ya kupiga kura ya
mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo kupitia
Chama cha Wananchi (CUF).
Akizungumza na waandishi wa
habari kwa njia ya simu msimamizi wa uchaguzi jimbo la Lulindi Beatrice
Dominick alikiri kutokea kwa kasoro hiyo na kuahidi kulitolea ufafanuzi suala
hilo baada ya wananchi kumaliza zoezi la upigaji kura hii leo.
Kasoro iliyojitokeza kwenye
karatasi hiyo ya kupiga kura ni kukosewa kwa jina hilo kwa kuandikwa Thomas Mshamu
badala ya jina sahihi la mgombea huyo Amina Thomas Mshamu ambalo lilistahili
kuandikwa kwenye karatasi hizo.
Wakizungumzia kasoro hiyo
mmoja wa wagombea wa nafasi ya ubunge jimbo hilo Modesta Makaidi kupitia chama
cha NLD ameshangazwa na kasoro hiyo na kwamba imetokana na usimamizi
usioridhisha wa tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushindwa kurekebisha kasoro hiyo
mapema.
Alisema wao kama wagombea
wanaendelea kusubiri ufafanuzi kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la
Lulindi ni lini uchaguzi huo utafanyika.
"Ni kweli uchaguzi wa nafasi ya ubunge jimbo la Lulindi umehairishwa kutokana na jina la mgombea wa CUF kukosewa...tunachosubiri ni maelekezo kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la Lulindi".alisema Modesta.
Jitihada za kumtafuta
mgombea huyo wa CUF ambaye jina lake limekosewa ili atoe ufafanuzi wa kasoro
hiyo ziligonga ukuta baada ya simu yake ya mkononi kutokuwa na majibu.
Hata hivyo Blog ya Mtazamo Mpya ilifanya
jitihada ya kumtafuta mwenyekiti wa CUF
wilaya ya Masasi Selemani Matola
ambapo alieleza kuwa ni kweli kasoro hiyo imejitokeza kwa mgombea wao na kwamba
wao kama uongozi wa wilaya wanaendelea kusubiri maelekezo kutoka kwa msimamizi
wa uchaguzi wa jimbo hilo ni lini uchaguzi utafanyika.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD