Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

HALMASHAURI YA MJI WA MASASI,TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU SIKU YA KUPIGA KURA

TANGAZO
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Masasi ambaye pia ni Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Masasi Fortunatus Mathew Kagoro.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wananchi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza hadi sasa kwa utulivu  na amani iliopo kwenye Kampeni za Udiwani katika Jimbo letu la Masasi Mjini. Leo naona tukumbushane mambo machache kwa kipindi hiki sadi siku ya kupiga kura tarehe 25.10.2015.
Kwanza nizungumzie juu ya Wapiga Kura WENYE ULEMAVU. Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia Kifungu cha 6 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, inaelekeza kuwa, Waratibu wa Mikoa na Wasimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo kuwapa KIPAUMBELE WATU WENYE ULEMAVU. Hivyo basi inabidi tuwape kipaumbele. Sambamba na hilo Wazee, akina mama wajawazito nao wapewe kipaumbele hapa naomba sana BUSARA ITUMIKE katika hili.
Wapiga kura wasioweza kupiga kura wenyewe, wasiojua kusoma na wasioona watasaidiwa na watu watakaowateua wao wenyewe. Kwa kawaida mtu mmoja atamsaidia Mpiga kura mmoja. Pale ambapo kutakuwa na Mpiga kura zaidi ya mmoja asiyeweza kupiga kura mwenyewe kutoka katika Kaya moja basi mtu mmoja ataruhusiwa kuwasadia wote.

KUFUNGUA KIKAO
Kituo cha Kupigia Kura kitafunguliwa Saa 1.00 asubuhi.

KUFUNGA KITUO
Kituo cha kupigia Kura kitafungwa Saa kumi kamili (10.00) jioni. Iwapo wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya wakati wa kufunga Kituo na hawajapiga kura, itabidi Msimamizi wa Kituo na hawajapiga kura, itabidi Msimamizi wa Kituo awape nafasi ya kupiga kura zao. Lakini asimruhusu mtu yeyote kujiunga katika mstari wa Wapiga Kura baada ya Saa kumi kamili (10.00) jioni. Njia bora ya kuwazuia watu waliochelewa, ni kumwamuru Mlinzi wa Kituo kusimama nyuma ya mtu wa mwisho katika mstari huo wa Wapiga Kura.

2. Tume ya Taifa ya uchaguzi inatoa ushauri ufuatao.
(i)           Vyama vya Siasa vihakikishe kuwa vitatimiza wajibu wake kama ilivyoelekezwa katika Katiba ya Nchi, Sheria, Kanuni za Uchaguzi, Maadili ya Uchaguzi na  Maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

(ii)          Vyama vinakumbushwa kwa Mujibu wa Kifungu cha 85 cha Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 (Sura ya 343) na Kifungu cha 86 cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Na. 4 ya mwaka 1979 (Sura ya 292), kutokuwepo kwa Wakala au Mgombea   mahali ambapo  wanaruhusiwa kuwepo katika hatua yoyote ya Uchaguzi, hakutazuia wala kubatilisha shughuli ya Uchaguzi, iliyofanywa kwa Mujibu wa Sheria. Kwa Mfano.

(a)  Saa ya kuanza upigaji kura itakapofika,  hata kama Wakala hayupo Upigaji Kura utaanza.

(b) Saa ya Kujumlisha Kura itakapofika, hata kama Wakala hayupo Upigaji Kura utaanza.

(c)  Saa ya Kutangaza Matokeo itakapofika, hata kama Wakala hayupo, Matokeo yatatangazwa kwa Mujibu wa Sheria.

(iii)        Vyama vya Siasa viwaelimishe Wagombea na Mawakala wao kuhusu taratibu zote za Uchaguzi  kwa gharama zao.

(iv)        Vyama vya Siasa viwahamasishe wanachama wao na wananchi kwa ujumla umuhimu wa Kujitokeza na kushiriki kwenye Uchaguzi.

(v)          Baada ya Wapiga Kura kumaliza Kupiga Kura zao, Tume inawashauri waondoke kurudi nyumbani na wasikaribie eneo la Upigaji Kura.

NDUGU  WANANCHI  SIKU HII MUHIMU NAOMBA SANA TENA SANA TUZINGATIE YAFUATAYO.

  1.  MAMBO YASIYORUHUSIWA KUFANYIKA SIKU YA KUPIGA KURA

(i)           Kufanya Kampeni ya aina yoyote

(ii)          Kuva Sare au alama za Chama, kubeba au kubandika matangazo au kuimba nyimbo za Vyama na

(iii)        Kuendelea kuwepo katika Vituo vya Kupigia Kura bila ya sababu yeyote.
 2. WANAORUHUSIWA KUINGIA KATIKA KITUO CHA KUPIGIA KURA

Watu wanaoruhusiwa kisheria kuwepo ndani ya Kituo cha
Kupigia Kura.

(i)           Msimamizi wa Kituo.
(ii)          Msimamizi Msaididizi wa Kituo
(iii)        Mgombea
(iv)        Wakala
(v)          Mpiga Kura kwa ajili ya Kupiga Kura tu.
(vi)        Mtu anayemsaidia Mpiga kura asiyeweza Kupiga Kura mwenyewe.
(vii)       Mtazamaji wa Uchaguzi aliyeidhinishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa maandishi.
(viii)      Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
(ix)        Mkurugenzi wa Uchaguzi.
(x)          Afisa wa Tume
(xi)        Msimamizi wa Uchaguzi na Msimamizi Msaidizi  wa Uchaguzi.
(xii)       Askari Polisi au Mlinzi wa Kituo na
(xiii)      Mratibu wa Uchaguzi wa Mkoa.

Waandishi wa Habari wataruhusiwa kwa Idhini ya Msimamizi wa Uchaguzi.
 3. MAELEZO YA NYONGEZA KWA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI KUHUSU UPIGAJI KURA KATIKA UCHAGUZI MKUU, 2015

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaelekeza kwamba.

1.    Mpiga kura ambaye atakuwa na kadi ya Mpiga kura ila namba ya kadi yake ni tofauti na namba iliyo kwenye Daftari la Kituo ataruhusiwa kupiga kura.

2.    Wapiga kura ambao picha zao hazionekani vizuri au hazionekani kabisa kwenye kadi za wapiga kura wataruhusiwa kupiga kura.

3.    Wapiga kura walioandikishwa na Tume na wanaishi katika maneo mapya ya kiutawala yaliyogawanywa wakati au baada ya zoezi la Uandikishaji kukamilika hivyo majina ya maeneo hayo kutofautiana na majina yaliyopo kwenye kadi zao wataruhusuwa kupiga kura.

4.    Wapiga kura walioandikishwa na kupata kadi lakini majina yao hayaonekani kwenye Daftari wataruhusiwa kupiga kura.
5.    Kwa mujibu wa Sheria, Mpiga kura ni lazima awe na kadi ndiyo, aruhusiwe kupiga Kura. Hivyo, Mpiga Kura asiye na Kadi hataruhusiwa kupiga kura.

6.    Wapiga kura ambao  wana kadi ya  kupigia kura lakini hawamo katika Daftari la kudumu  la Wapiga kura Kituoni hawataruhusiwa kupiga kura.
 MWISHO:
Wito wangu kwa Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi ni kujitokeza kwa wingi siku hiyo ya tarehe 25.10.2015 ili tutumie nafasi yetu ya kumchagua Kiongozi atakayetuongoza miaka 5 ijayo. Sambamba na hilo naomba tupige Kura, turudi nyumbani wakati tukisubiri matokeo kwa kufanya hivyo tutalinda heshima zetu na Uchaguzi utakuwa umefanyika kwa haki na Amani.
 Asanteni sana.
 MUNGU IBARIKI MASASI, MUNGU IBARIKI TANZANIA

IMETOLEWA NA:
FORTUNATUS MATHEW KAGORO
MKURUGENZI WA MJI
HALMASHAURI YA MJI
MASASI







TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top