TANGAZO
Mwenyekiti wa tume ya Taifa ya uchaguzi Jaji mstaafu Damian Lubuva (Picha ya Maktaba)
SIKU 12 kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi
Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani nchini, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imebainisha idadi kamili ya Watanzania wanaostahili kupiga kura siku ya Oktoba,
25, mwaka huu), kuwa ni milioni 22.7 na si milioni 23.7 ya awali.
Hayo yamebainika baada
ya tume hiyo kumaliza uhakiki na uchakataji wa Daftari la Wapiga Kura kupitia
mfumo wa Biometric Voters Registarion (BVR). Kutokana na idadi hiyo mpya, tume
hiyo imefuta na kuengua katika daftari hilo watu 1,031,266 kutokana na kukosa
sifa za kuwepo kwenye daftari hilo.
Waliofutwa ni pamoja na
wananchi 181, 452 waliojiandikisha zaidi ya mara moja hadi mara nane kwa mtu
mmoja. Aidha tume hiyo, imevitaka vyama vya siasa nchini katika ngwe ya mwisho
ya kampeni, kutumia majukwaa ya siasa kunadi sera ili wananchi waweze
kushawishika na kuwachagua.
Vimetakiwa kuacha
kutumia vibaya majukwaa, kuchafuana na kuichafua tume hiyo kwa kutoa taarifa
zisizo sahihi. Hayo yalibainishwa na viongozi wa tume hiyo, ambao ni Mwenyekiti
Jaji Damian Lubuva na Mkurugenzi wa tume hiyo, Kailima Kombwey, wakati tume
hiyo ilipokutana na viongozi wa vyama vya siasa, kujadili mwenendo wa kampeni
na maandalizi ya uchaguzi.
Akizungumza katika
mkutano huo, Kombwey alisema kwa sasa tume hiyo imekamilisha maandalizi ya kuboresha
daftari la wapiga kura. Alisema baada ya uhakiki na uchakataji wa taarifa za
wapiga kura, Tume imebaini kuwa wapigakura milioni moja, hawakustahili kuwemo
kwenye daftari hilo.
Alisema idadi ya wapiga
kura milioni 23.7 ya awali, ilipatikana kutokana na taarifa zilizopatikana moja
kwa moja kwenye vituo vya kupigira kura ; na baada ya uhakiki na uchakataji
huo, idadi kamili ya wapiga kura wanaostahili kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu
ni milioni 22.7.
Alisema kati ya wapiga
kura hao milioni moja, ambao taarifa zao zimeondolewa, wananchi 181,452
walibainika kuwa walijiandikisha zaidi ya mara moja hadi mara nane kwa mtu
mmoja.
Aidha alisema baada ya
uhakiki huo, tume hiyo ilibaini wananchi 845,944 ni wale waandikishaji wa mfumo
wa Biometric Voter Registration (BVR), ambao jumla yao walikuwa 74,502
waliokuwa wakifanya mafunzo ya vitendo kabla ya kuanza uandikishaji wenyewe.
“Pia wananchi 3,870
wamebainika kuwa waliandikishwa wakiwa si raia wa Tanzania na hivyo
vitambulisho vyao vimerejeshwa na taarifa zao kufutwa kwenye kanzidata ya
Daftari la Kudumu,” alisema Kombwey.
Mkurugenzi huyo alisema
katika maandalizi ya uchaguzi ambayo bado yanaendelea, tume hiyo imeandaa vituo
vya kupigia kura 65,105. Kati ya hivyo, vituo vilivyopo Tanzania Bara ni vituo
63,525 na Zanzibar vituo 1,580, ambapo kila kituo kitakuwa na uwezo wa
kuhudumia wapigakura 450 na wasiozidi 500.
“Kituo kitakapokuwa na
wapigakura zaidi ya 500 kitagawanywa katika vituo viwili kwa idadi sawa kwa
kila kituo. Wapiga kura wanashauriwa kwenda katika vituo walivyojiandikisha
kupiga kura siku nane kabla ya siku ya kupiga kura ili kujua vituo vyao halisi
vya kupigia kura,” alisisitiza.
Pia alisema wananchi
wataweza kupata taarifa zao, zilizoko kwenye kanzidata kwa kutumia simu zao za
kiganjani kupitia ujumbe mfupi wa maneno, bila wao kulazimika kufika vituoni
kupitia namba *152*00# na kufuata maelekezo.
Alisema kupitia uteuzi
uliofanywa na tume hiyo, wagombea wa kiti cha urais waliopitishwa na tume hiyo,
watakaoshindanishwa katika uchaguzi huo ni nane, ambapo mgombea mwanamke ni
mmoja na wengine saba wanaume.
Alisema idadi ya
wagombea ubunge, waliopitishwa kuwania majimbo 264 yaliyopitishwa na NEC ni
wagombea 1,218, kati yao wanaume ni 985 na wanawake ni 233. Wagombea udiwani
wanaowania kata 3,957 ni 10,879, ambapo wanaume ni 10,191 na wanawake 679.
Katika orodha hiyo,
vyama vilivyosimamisha wagombea wengi katika nafasi za udiwani ni CCM, Chadema,
ACT, CUF, ADC na NCCR-Mageuzi. Kombwey alisema tume hiyo imeteua na kuwapatia
mafunzo watendaji 30 ngazi ya mikoa, 972 ngazi ya jimbo na 9,914 ngazi ya kata,
ambao kazi yao ni kuratibu na kusimamia uchaguzi , wasimamizi wa vituo na
makarani waongozaji.
Kwa upande wake, Jaji
Lubuva alisema tume hiyo inasikitika kutokana na baadhi ya vyama vya siasa
kutumia majukwaa yao vibaya na kuwaomba katika kipindi hiki cha kuelekea
ukingoni mwa kampeni, kusisitizia zaidi sera zao na kutoa taarifa sahihi
ikiwemo elimu ya uchaguzi kwa wananchi.
“Tume inawaomba kuepuka
kutoa taarifa za shutuma zisizo sahihi kuhusu tume na badala yake mjikite
katika kufikisha taarifa zilizo sahihi na zilizokusudiwa kwa wafuasi wenu na
wananchi wote kwa ujumla,” alisema.
Alisema tume hiyo
imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa za kupiga kura, anapiga kura
yake bila kubughudhiwa. “Tumesikia baadhi ya vyama vinashawishi wapiga kura
wake kutoondoka vituoni baada ya kupiga kura, kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya mkutano, kuvaa sare au kuwa na kadi
ya chama anachokiunga mkono katika sehemu ya kupigia kura,” alisema.
Akijibu hoja ya baadhi
ya viongozi wa vyama vya siasa waliotaka mfumo mpya wa matokeo uhakikiwe
kwanza, Lubuva alisema mfumo huo ni bora na una lengo la kuondoa dhana nzima ya
wizi wa kura. “Lakini pia mfumo huu umeletwa kwetu na watu huru wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), “ alisema.
CHANZO:HABARI LEO.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD