TANGAZO
Dkt.Emanuel John Makaidi enzi za uhai wake
HALMASHAURI YA MJI WA MASASI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Ndugu wananchi kama
mnavyofahamu bado tuko kwenye mchakato wa kampeni na hatimaye uchaguzi wa
kuchagua Rais,wabunge na madiwani utakaofanyika oktoba 25,mwaka huu ambapo kwa
jimbo la Masasi kampeni hizo zimekuwa zikifanyika kwa amani na usalama.
Ndugu wananchi jimbo la
Masasi ni miongoni mwa majimbo nchini yatakayofanya uchaguzi ambapo kwa nafasi
ya ubunge jimbo la Masasi vyama vitano vimesimamisha wagombea ikiwemo CCM, NLD,
CUF,ACT-Wazalendo pamoja na CHADEMA.
Ndugu wananchi kama
mlivyosikia,kusoma na kuona kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini kuwa
mmoja wa wagombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Masasi kupitia chama cha NLD
Dkt.Emanuel Makaidi amefariki dunia oktoba 15 mwaka huu majira ya saa 7:30
Mchana huko katika hospitali ya misheni ya Nyangao mkoani Lindi kutokana na
tatizo la shinikizo la damu.
Ofisi yangu ilipokea
taarifa hiyo ya kuhuzunisha kutoka kwa uongozi wa chama hicho cha NLD kuwa
mgombea wao amefariki dunia ambapo baada ya kupokea taarifa hiyo tulitoa taarifa
ofisi ya tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kuhusu kifo hiko cha mgombea wa nafasi
ya ubunge.
Kwa mujibu wa sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kifo cha Dkt.Emanuel
Makaidi kinafanya, uchaguzi wa ubunge kwa Jimbo la Masasi uahirishwe hadi
utakapopangiwa tarehe nyingine. Masasi linakuwa jimbo la sita litakalofanya
uchaguzi mdogo kutokana na mmoja wa wagombea wake kufariki dunia kabla ya
Uchaguzi Mkuu.
Aidha kwa mujibu wa kifungu
cha 49 cha sheria ya Taifa ya uchaguzi ya mwaka 1985 (Sura ya 343),baada ya
uteuzi na kabla ya mwisho wa upigaji kura,endapo mgombea yeyote
atafariki,Msimamizi wa uchaguzi atasimamisha uchaguzi na kutoa taarifa Tume ili
ipange tarehe nyingine ya uteuzi wa mgombea wa chama husika.
Ndugu wananchi,kutokana na tukio hilo la kifo cha Dkt.Makaidi ambaye
alikuwa ni mgombea wa nafasi ya ubunge wa jimbo la Masasi,nachukua fursa hii
kutamka rasmi kuwa kutoka sasa shughuli zote za kampeni za wagombea wa nafasi
ya ubunge jimbo la Masasi zimesimamishwa hadi hapo Tume ya Taifa itakapotangaza
tena.
Aidha naomba ifahamike
kwamba vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huu kwa jimbo la Masasi viko
huru kuendelea na kampeni ila ni kwa nafasi ya udiwani na Rais pekee na kwamba
pia siku ya upigaji kura Oktoba 25 mwaka huu wananchi wa jimbo la Masasi watamchagua
Rais pamoja na Madiwani pekee.
Tayari vyama vya siasa
vinavyoshiriki uchaguzi huu jimbo la Masasi tumeviandikia barua ya kuwataka
kusitisha shughuli zote za kampeni kwa
nafasi ya ubunge na kwamba kwa kuendelea kufanya kampeni kwa nafasi hiyo ni
kukiuka sheria ya Taifa ya uchaguzi ya mwaka 1985 sura ya 343.
Aidha napenda kutoa taarifa
kwa wananchi wote wa jimbo la Masasi kuwa tayari majina ya wapiga kura
yamebandikwa kwenye vituo vyote vya upigaji kura,hivyo nawaomba wananchi
waliojiandikisha kufika kwenye vituo vyao walivyojiandikishia ili kuhakiki
majina yao kwa lengo la kuondoa malalamiko yoyote yanayoweza kujitokeza siku ya
kupiga kura.
Kwa wale ambao watabaini
kuwepo kwa kasoro kwenye majina yao wapelekea malalamiko yao ofisi ya msimamizi
wa uchaguzi jimbo la Masasi iliyopo Halmashauri ya mji wa Masasi ambapo mwisho
ni Oktoba 19,2015 saa 10:00 jioni.
Mwisho,napenda kutoa
shukrani zangu za dhati kwa wananchi wote pamoja na vyama vya siasa katika jimbo la Masasi ambao mmekuwa
mkishiriki kwa amani na utulivu kwenye mikutano yote ya kampeni ambayo
inaelekea ukingoni,Aidha natumia nafasi hii pia kutoa pole kwa chama cha
NLD kwa kumpoteza mwenyekiti mwenza wa
UKAWA marehemu Dkt.Emanuel Makaidi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza,
Imetolewa na,
Fortunatus
Mathew Kagoro
Msimamizi
wa uchaguzi jimbo la Masasi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD