TANGAZO
Dkt.Emanuel Makaidi enzi za uhai wake (picha ya maktaba)
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Mwanasiasa mkongwe ambaye
ni mwenyekiti mwenza wa umoja wa Ukawa Dkt.Emanuel Makaidi amefariki dunia
katika hospitali ya misheni ya mtakatifu Walburger Nyangao mkoani Lindi kutokana
na tatizo ya shinikikizo la damu.
Aidha licha ya kuwa
mwenyekiti mwenza wa ukawa marehemu Dkt.Emanuel Makaidi pia alikuwa ni mwenyekiti
wa Taifa wa chama cha NLD na mgombea wa
nafasi ya ubunge jimbo la Masasi kupitia chama cha NLD.
Tukio hilo la kusikitisha na lililoacha simanzi kwa wakazi wa wilaya ya
Masasi ambako makaidi alizaliwa limetokea leo majira ya saa 7:30 mchana katika
hospitali hiyo ya Nyangao baada ya
kulazwa kwa muda hospitalini hapo akitokea nyumbani kwao mjini Masasi majira ya
saa 5:30 asubuhi akiwa amepoteza fahamu.
Akithibitisha kutokea kwa
tukio hilo kaimu mganga mkuu wa hospitali ya misheni ya Nyangao mkoani Lindi
Betram Makotha alisema walimpokea marehemu Dkt.Emanuel Makaidi leo majira ya
saa 5:30 asubuhi akiwa amepoteza fahamu kutokana na tatizo hilo la shinikizo la
damu(BP).
Alisema marehemu alifika
hospitalini hapo akiwa hajitambui huku vyeti vyake alivyokuja navyo hospitalini
hapo vikionesha siku ya jumanne asubuhi alipata vipimo vya shinikizo na damu na
kuonesha kuwa lilipanda hadi kufikia kiwango cha 200.
Alisema mara baada ya kupatiwa
matibabu ya awali hali yake iliendelea kubadilika na kuwa mbaya zaidi na
hatimaye ilipofika majira ya saa 7:30 mchana alifariki dunia kutokana na tatizo
hilo la shinikizo la damu lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu.
Kwa upande wake mke wa
marehemu Makaidi,Modesta Makaidi ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya ubunge
jimbo la Lulindi wilayani Masasi kwa tiketi ya chama cha NLD alisema mumewe
amefariki hii leo majira ya saa 7:30 kutokana na shinikizo la damu ambalo ni
kwa muda mrefu limekuwa likimsumbua.
Alisema tayari mwili wa
marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitaili hiyo
ya Nyangao huku taratibu zingine za mazishi zikiendelea ingawa alishindwa
kusema ni lini na ni wapi marehemu Dkt.Makaidi atazikwa kutokana na kushindwa
kuvumilia na kuangua kilio.
Kwa upande wake mkurugenzi
wa kituo cha zahanati cha Best kilichopo wilayani Masasi ambako kabla ya kifo
chake Dkt.Makaidi alipatiwa vipimo Dina Marumbwe alisema ni kweli siku ya jumanne
oktoba 13 mwaka huu marehemu akiambatana na mke wake walifika kituoni hapo kwa
ajili ya kupatiwa vipimo na matibabu kutokana na tatizo hilo la shinikizo la
damu.
Alisema vipimo vilionesha
wazi kuwa marehemu alikuwa na kiwango kikubwa cha shinikizo la damu hadi
kufikia 200 kitu ambacho si kizuri kiafya ambapo baada ya vipimo alipatiwa dawa
na aliomba apumzike kwa muda kituoni hapo kwa kuwa si kituo kinacholaza
wagonjwa kwa muda mrefu.
Alisema ilipofika majira ya
saa 1:00 usiku hali yake ilirejea kama kawaida na yeye mwenyewe akaomba
aruhusiwe kuondoka kurudi nyumbani na kwamba aliondoka yeye pamoja na mke wake
huku akisema kuwa baada ya kuondoka hakupata tena taarifa za maendeleo yake
hadi umauti unampata.
Akizungumza kwa sharti la
kutotajwa kwa jina lake kutokana na sababu za kiusalama na kwa kuwa yeye sio
msemaji wa chama mmoja wa watu waliomfahamu Dkt.Makaidi alisema tatizo hilo
lilianza kuwa kubwa mwanzoni mwa wiki hii wakati wa mkutano wake wa kampeni
alioufanya eneo la Jida mjini Masasi.
Dkt. Emmanuel
Makaidi alizaliwa Aprili 10, 1941 huko
wilayani Masasi mkoani Mtwara. Baba yake mzazi alikuwa ni katekista wa Kanisa
la Anglikana.
Alianza elimu katika
Shule ya Msingi Namalenga wilayani Masasi kati ya mwaka 1948 – 1952, mwaka 1953
– 1954 alisoma katika Shule ya Kati (Middle school) iitwayo Luatala hukohuko
Masasi. Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph na
kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne kati ya mwaka 1953 hadi 1956.
Makaidi alisoma darasa
la 13 na 14 (kidato cha tano na sita) katika Shule ya Sekondari Luhule, Uganda
kati ya mwaka 1957 – 1958. Alipelekwa Uganda si kwa sababu ya kipato cha baba
yake, la hasha, alisaidiwa na Askofu wa Anglikana baada ya kuona anafaulu mitihani
yake kwa alama za juu sana.
Makaidi aliendelea
kufadhiliwa na askofu huyo ambaye alimuunganisha na mashirika mengine na
kumtafutia chuo Afrika ya Kusini. Akapelekwa Chuo Kikuu cha Witwatersrand na
kuhitimu Shahada ya Uendeshaji na Usimamizi kati ya mwaka 1958 – 1960.
Baada ya kuhitimu
vizuri pale Witts, aliendelea kupata ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili,
mara hii alielekea Marekani na kusoma masuala ya Menejimenti na Utawala kwa
ngazi ya uzamili kati ya mwaka 1960 – 1962. Alisoma pia katika Chuo Kikuu cha
Howard kilichoko jijini Washington, Marekani.
Baada ya kurejea nchini
akiwa mhitimu wa M.A, Makaidi alianza kazi serikalini mwaka 1966 hadi mwaka
1973 akiwa mchambuzi kazi mkuu, katika kitengo cha Utumishi.
Kati ya mwaka 1974 na
1975 (miaka miwili). Alirudi tena Marekani na kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD)
katika Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Howard akipata kuwa karibu na
mmoja wa maprofesa nguli duniani, Wamba Dia Wamba. Makaidi ameniambia kuwa hata
tabia ya kuandika vitabu na kutunga mambo ya ubunifu, alifundishwa na profesa
huyu mahiri.
Aliporejea nchini kwa
mara ya pili mwaka 1976 aliendelea na kazi yake pale Utumishi hadi mwaka 1985
alipopewa kazi nyingine kubwa zaidi, akawa Mkurugenzi wa Miundo na Mishahara
kwenye kamati iliyokuwa inashughulikia mashirika ya umma nchini.
Wakati anaendelea na
kazi utumishi, alipata fursa nyingine ya kusomea stashahada ya Kuchakata
Taarifa za Kielektoniki katika Chuo Kikuu cha Trinity, Ireland. Alikwenda huko
na kuhitimu mwaka huohuo 1977.
Dkt. Makaidi alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza mwaka
2010 katika Jimbo la Masasi, Mtwara akipambana na Mariam Kasembe wa CCM
(aliyeibuka mshindi wa jumla kwa asilimia 63.7) na Clara Mwatuka wa CUF
(aliyepata asilimia 15.2). Katika uchaguzi huo Dk. Makaidi alishika nafasi ya
tatu kwa kupata kura 5,384 sawa na asilimia 11.7 ya kura zote zilizopigwa.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD