Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU: MAASKOFU WILAYANI MASASI WATAKA AMANI ILINDWE,WATAKA WAGOMBEA KUKUBALI MATOKEO.

TANGAZO

Na Hamisi Nasiri,Masasi.

MAASKOFU na wachungaji wa makanisa mbalimbali wilayani Masasi mkoani
Mtwara wameitaka Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kutenda haki kwa
kusimamia kanuni na sheria ya uchaguzi kwa vyama vyote bila kuonyesha
kukibeba chama kingine,jambo ambalo litasaidia kudumisha amani kwenye
uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu.


Aidha maaskofu hao wamewataka wagombea wote wa vyama vya siasa nchini
wawe tayari kukubali matokeo yatakayotangazwa na tume ya uchaguzi na
kwamba mgombea atakayeshinda ndio chaguo la mungu ndani ya taifa hili.


Maaskofu na wachungaji hao walipaza sauti zao mwanzoni mwa wiki  walipokuwa wamekusanyika katika
viwanja vya Boma wilayani hapa katika tamasha maalumu la kuliombea
taifa amani katika kuelekea uchaguzi mkuu ujao Oktoba 25 mwka huu
ambapo tamasha hilo lilihusisha viongozi wa makanisa mbalimbali mjini
hapa.


Akizungumza kwa niaba ya waumini hao, Askofu wa kanisa la Pentekoste
la Lukuledi Masasi Angelus Mchomanjoma alisema kuwa katika kipindi
hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu tume ya taifa ya uchaguzi inapaswa
itende haki kwa vyama vyote katika kusimamia sheria ya uchaguzi ndipo
taifa liendelee kuwa na amani pamoja na utulivu.


Askofu huyo alisema viongozi wa dini nchini hawapaswi kufungamana na
vyama vya siasa bali wao wanachoweka mbele kwa sasa ni suala la amani
na utulivu katika uchaguzi mkuu na kusisitiza kuwa jambo la amani
linapaswa kuwa endelevu.


Mchomanjoma aliongeza kuwa mara nyingi amani hutoweka unapofika wakati
wa uchaguzi hivyo vyombo vya ulinzi na usalama pia vizingatie sheria
na maadili ya kazi yao na kwamba wasidhubutu kutimia nguvu kubwa ili
kuweza kudumisha amani aidha wananchi wajitokeze kupiga kura.


“Natumia fursa hii kukanusha kuwa baadhi ya watu na hasa wanasiasa
wanaosema kwamba serikali haijafanya maendeleo yoyote tangu miaka 50
nasema sio kweli yapo mambo mengi yamefanyika hasa katika utawala wa
Rais Mkapa na Kikwete ninawapongeza sana,”alisema Mchomanjoma.


Wakizungumzia kuhusu amani na utulivu baadhi ya washiriki wa tamasha
hilo, Diana Alfred pamoja na mchungaji wa kanisa la Pentekoste
uinjilisti Masasi, Dickson Misanjo walisema amani ndio msingi wa taifa
la Tanzania hivyo viongozi wawe makini katika kudumisha amani.


“Hawa viongozi wasiwe na uchu wa madaraka wa kutaka kila mmoja apate
nafasi ya kuongoza wajuwe amani ya taifa hili ipo mikononi mwao
tunaomba amani isitoweke ndio lengo la tamasha letu leo hii,”alisema
Diana.


Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Masasi, Danford Peter kwa
niaba ya mkuu wa wilaya hiyo, alisema suala la amani linapaswa
kuzungumziwa wakati wote na sio wakati wa uchaguzi pekee,kwani amani
ndio kila kitu katika taifa linalotaka kupiga maendeleo.


Alisema viongozi wa dini na wadau wengine wanayo nafasi kubwa ya
kutangaza amani ili kulinusuru taifa kuingia katika machafuko hasa
katika kipindi hiki cha uchaguzi hivyo kila mtanzania anatakiwa
kudumisha amani na utulivu.



TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top