TANGAZO
SERIKALI imepokea
majina matatu ya mahujaji wengine wa Tanzania, waliokufa kutokana na tukio la
kukanyagana lililotokea eneo la Mina, katika mji Mtakatifu wa Makka, Saudia
Arabia Septemba 24, mwaka huu, hivyo kufanya idadi ya mahujaji wa Tanzania
waliopoteza maisha nchini humo kufikia 11.
Hayo
yalithibitishwa jana na Serikali kupitia taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari. Taarifa hiyo
iliwataja watatu zaidi waliokufa kuwa ni Yusuf Ismail Yusuf kutoka kikundi cha
Khidmat Islamiya, Rahma Salim Suweid kutoka kikundi cha Ahlu Daawa na Issa Amir
Faki.
Ilisema
mahujaji hao walitambuliwa baada ya kupitia taarifa zao za vidole zilizotolewa
na Serikali ya Saudi Arabia. Serikali ilisema vifo hivyo vinaendelea kuwa pigo
kwa taifa na kwamba, vimepokelewa kwa masikitiko makubwa.
“Aidha,
Ubalozi unaendelea kushughulikia taratibu za maziko kwa mahujaji ambao
wamefariki dunia na miili yao kutambuliwa. Tunapenda kufafanua kuwa mali za
marehemu ikiwemo mizigo waliyokuwa nayo wakati wa Hijah zitawasilishwa nyumbani
Tanzania na vikundi walivyokuja navyo na kukabidhiwa kwa jamaa wa marehemu,”
ilieleza wizara.
Pia
ilieleza kuwa Ubalozi unaendelea kufuatilia orodha mpya ya taarifa za vidole,
iliyotolewa na Serikali ya Saudi Arabia kwa ajili ya kuwabaini mahujaji wa
Tanzania ambao hawajatambuliwa. Mpaka sasa zaidi ya mahujaji 30 wa Tanzania
hawajulikani walipo.
CHANZO:HABARI LEO.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD