TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Askofu wa kanisa la Sayuni International
Pentekoste, Masasi mkoani Mtwara Angelus Mchomanjoma amewataka Watanzania kuilinda amani iliyopo
ambayo ni tunu kwa taifa letu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye
uchaguzi mkuu oktoba 25 mwaka huu.
Wito huo ameutoa jana wakati anaongea na "Blog ya Mtazamo Mpya" kuhusu maandalizi ya tamasha la kuombea amani mkoa wa Mtwara
litakalofanyika oktoba 11, 2015 kwenye viwanja vya Boma mjini Masasi.
Alisema lengo kuu la tamasha hilo ni kuombea
amani ili matokeo ya uvunjifu wa amani yasijitokeze kipindi hiki cha kampeni na
baada ya matokeo kutangazwa na kwamba Rais atakayechaguliwa na hatimaye
kutangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi ndie chaguo la mungu.
Alisema tamasha hili la kuombea amani mkoani
Mtwara ambalo litashirikisha maaskofu,wachungaji pamoja na waimbaji kutoka
kwenye kwaya mbalimbali za makanisa hayo ya kipentekoste kutoka ndani na nje ya
mkoa wa Mtwara litaanza majira ya saa 8:00 mchana na kumalizika 12:30 jioni.
Kwa mujibu wa askofu huyo alisema tamasha
hilo linakuja kwa kuzingatia matokeo ya uvunjifu wa amani yaliyotokea mkoani
Mtwara ambayo kwa kiasi kikubwa yaligharimu maisha na mali za wananchi na
kusababisha hasara kubwa ya mamilioni ya fedha.
“Tamasha hili si la kunadi sera za wagombea…na
ninatoa wito kwa wananchi wote na hata wagombea ambao tumewaalika watakaohudhuria
kutovaa sare za vyama vyao vya siasa na
pia tumewaelekeza kutoshangilia kwa kuonesha ishara ya vyama vyao vya siasa”alisema
Mchomanjoma.
Alisema tamasha hilo lenye lenye kauli mbiu
ya “umoja wetu ndio msingi wa amani yetu” ni sehemu muafaka kwa maaskofu na
wachungaji wa umoja wa makanisa ya kipentekoste kuhubiri neno la mungu kwa
ajili ya kulinda na kuitetea amani kipindi chote cha uchaguzi.
Akizungumzia kuhusu ulinzi alisema tayari
wameshawasilisha maombi kwa mkuu wa jeshi la polisi wilaya ya Masasi na kwamba
ni matumaini yao kuwa ulinzi utaimarishwa huku akiwataka wananchi wa wilaya ya
Masasi na mkoa wa Mtwara kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwani hakutakuwa na
kiingilio.
Kwa mujibu wa Kiongozi huyo wa Kanisa,
alisema haoni mantiki ya baadhi ya wanasiasa wanaotafuta kuchaguliwa kwa
kuwaahidi Watanzania kuwapatia huduma bure,kama za afya,elimu na maji;badala ya
kuwahimiza wafanye kazi ili kujiinua kiuchumi.
Tamasha hilo la kuombea amani mkoa wa Mtwara
limeandaliwa na askofu Mchomanjoma kwa ushirikiano na umoja wa makanisa ya
pentekoste mkoani humo huku maaskofu,wachungaji na kwaya mbalimbali zikialikwa.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD