TANGAZO
Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Lindi Mhashamu Bruno Ngonyani
Na Clarence Chilumba,Mtwara.
Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Lindi
Mhashamu Bruno Ngonyani amewataka Watanzania kudumisha amani iliyopo kwa
kuchagua viongozi wenye uadilifu na watakaotenda haki na usawa kwa watanzania
wote.
Wito huo ameutoa wakati anaongoza Ibada ya
kufunga mwaka kwa familia za kikristo iliyofanyika kwenye viwanja vya chuo
kikuu cha SAUTI tawi la Mtwara na
kuhudhuriwa na waumini wa kanisa hilo kutoka kwenye majimbo saba yanayounda
kanda ya kusini,mwishoni mwa juma hili.
Alisema amani ni kitu muhimu kwa ustawi wa
Taifa na kwamba amani hiyo hutoweka pindi yanapotokea machafuko huku waathirika
wakubwa wa machafuko hayo wakiwa ni akinamama pamoja na watoto.
Alisema mwaka huu ni wa kipekee katika
historia ya siasa za Tanzania kwani wananchi wa rika mbalimbali wamekuwa
wakijitokeza kwa wingi kushiriki kwenye mikutano ya kampeni huku akiwaomba
kuchagua kiongozi yule ambaye atakuwa na sera nzuri kwa taifa.
“Wananchi mnapaswa kupima ahadi zinazotolewa
na wagombea wa vyama vyote vya siasa kama zinatekelezeka au hazitekelezeki ili
siku ya kupiga kura mfanye maamuzi sahihi kwa kumchagua kiongozi aliyetoa ahadi
zinazotekelezeka”.alisema Ngonyani.
Kwa mujibu wa Kiongozi huyo wa Kanisa, aliwaomba
wananchi wenyewe watendeane haki huku akiiomba serikali pia kutenda haki kwa
raia wake katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuwa ni jukumu la serikali
kutenda haki kwa raia wake.
Kwa upande wake kaimu mkuu wa mkoa wa Mtwara
Johansen Bukwali alisema jambo muhimu ni kudumisha familia na amani kwa kutii utawala uliopo na kutekeleza
kanuni zilizopo ili uchaguzi uwe huru na wa amani kwani baada ya uchaguzi
maisha yanaendelea.
Maadhimisho hayo ya mwaka wa familia
yalitangazwa na kanisa katoliki septemba 27,2014 ambapo kwa kanda ya kusini
yalifanyika jimbo la Mtwara na kuhudhuriwa na majimbo ya
Songea,Iringa,Tunduru-Masasi,Mbeya,Njombe, pamoja na jimbo la Mbinga.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD