TANGAZO
Mgombea wa nafasi ya urais kupitia ACT-Wazalendo Mama Anna Mghwira akiwa kwenye moja ya mikutano yake.
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Mgombea wa nafasi ya
Urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo Anna Mghwira amesema endapo atachaguliwa
na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atahakikisha anajenga viwanda
vya ubanguaji wa korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Aliyasema
hayo jana wakati akiomba kura kwa wananchi wa mji wa Masasi kwenye mkutano wake
wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Terminal two mjini humo ambapo
alisema ili kurudisha thamani ya zao la korosho serikali yake itajenga viwanda
vya kubangua zao hilo na kufufua vile ambavyo kwa sasa havifanyi kazi.
Alisema
ili nchi iwe na maendeleo serikali yake itahakikisha kuna kuwa na uchumi
shirikishi ambao hutoa fursa kwa wananchi wote kushiriki kwenye maamuzi magumu
ya serikali ikiwemo ujenzi wa viwanda,ubinafsishaji wa rasilimali za taifa na
kwamba ni lazima serikali yake itawashirikisha wananchi wenyewe waweze kukubali
ama vinginevyo.
Alisema
maeneo mengi aliyopita kwenye mikoa ya kusini wakati wa kampeni zake amejionea ardhi
nzuri yenye rutuba inayofaa kwa kilimo na kwamba endapo watanzania watampa
ridhaa ya kuongoza nchi serikali yake itaboresha kilimo kwa mikoa ya kusini kwa
kuleta pembejeo na zana za kilimo kwa wakati na kwa gharama ndogo.
Kwa
mujibu wa mgombea huyo wa nafasi ya urais alisema sekta ya kilimo imekuwa
haipewi kipaombele mazingira yanayosababisha wakulima bado kuendelea kutumia
zana duni za kilimo ambapo amehaidi kushughulikia kero hizo endapo watanzania
watampa ridhaa ya kuongoza.
Aidha
Mghwira alisema ataboresha mifuko ya hifadhi ya jamii ili kila mwananchi awe na
akiba tofauti na ilivyo sasa kwamba ni watumishi wa umma pekee ndio wenye akiba
kupitia mifuko hiyo sambamba na kutoa huduma bora kwa wazee ili nao wanufaike
na matunda ya uhuru wa nchi yao.
Mghwira
alivitaja vipaombele vyake kuwa ni pamoja na hifadhi ya jamii,uchumi
shirikishi,afya,elimu,miundombinu na maji huku akijinasibu kuwa serikali yake
itakuwa ya uadilifu,utu na uzalendo kwa wananchi wote na kwamba wafanyakazi wa
umma wanapaswa kutenda haki kwa wananchi wanaowahudumia.
Kwa
upande wake mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo
Ahmad Yusuph alisema watasimamia rasilimali za nchi zilizopo ili ziweze kuleta
manufaa kwa taifa na kwa wananchi kwa ujumla na kwamba moja ya mipango yao ni kuboresha bei za mazao ya
wakulima nchini.
Alisema
nchi ya Tanzania ina rasilimali za kutosha kinachokosekana ni usimamizi wa
rasilimali hizo ili kila Mtanzanzia aweze kunufaika na mgawanyo wa rasilimali
hizo na kwamba serikali yao chini ya chama cha ACT-Wazalendo kitafanya
mapinduzi katika sekta hiyo kwa kutoa fursa sawa kwa watanzania wote.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD