TANGAZO
Meneja wa PSPF mkoa wa Mtwara Omari Kaliko akizungumza na watumishi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi mkoa wa Mtwara ambavyo ni Mtawanya,Newala na Masasi wakati wa mkutano wa baraza la wafanyakazi wa vyuo hivyo uliofanyika jana kwenye ukumbi wa chuo cha maendeleo ya wananchi Masasi.
Na Clarence
Chilumba; Masasi.
Mfuko wa pensheni kwa
watumishi wa umma PSPF umedhamiria kutoa huduma bora kwa wanachama wake kwa lengo la kuboresha
maisha yao pindi wanapokuwa kazini na hata mara baada ya kustaafu ikiwa ni
utekelezaji wa sera na mikakati ya serikali katika kuboresha maisha ya
wafanyakazi wake.
Akizungumza jana wakati
anawasilisha mada ya majukumu ya mfuko wa PSPF kwenye mkutano wa baraza la wafanyakazi wa vyuo vya maendeleo ya
wananchi mkoa wa Mtwara,meneja wa PSPF mkoa wa Mtwara Omari Kaliko alisema kwa
sasa mfuko huo unatoa mikopo ya nyumba na viwanja kwa wanachama wake.
Alisema PSPF inatambua
umuhimu wa wanachama wake kumiliki nyumba ambapo mwanachama atakuwa analipa
kidogo kidogo kwa muda wa miaka 25 mkopo utakaomwezesha mwanachama kuishi
kwenye nyumba yake mara tu makato ya mkopo huo
yatakapoanza.
Alisema kwa sasa PSPF
tayari imeshajenga nyumba kwa ajili ya kukopesha wanachama wake katika maeneo ya Chanika
jijini Dar es salaam nyumba ambazo hukopeshwa kwa shilingi 60 hadi 84 milioni na
kwamba kwa upande wa mikoani nyumba moja
hukopeshwa kwa shilingi milioni 60 hadi 70.
Aidha Kaliko alisema licha
ya mikopo ya nyumba pia PSPF inatoa mikopo mbalimbali kwa wanachama wake ikiwemo
mikopo ya viwanja,elimu,mikopo kwa waajiriwa wapya pamoja na mikopo kwa
wastaafu yenye masharti nafuu ambapo kwa
mkoa wa Mtwara PSPF tayari wana viwanja vilivyopimwa katika eneo la Mitengo na
mji Mwema mkoani humo.
Kwa mujibu wa meneja huyo
wa mkoa wa Mtwara alisema PSPF inathamini michango ya wanachama wake kwa kuwekeza
katika maeneo mbalimbali huku akijinasibu kuwa mfuko huo ni tofauti kabisa na
mifuko mingine ya hifadhi ya jamii kwa kuwa mwaka 2013 mfuko ulipata tuzo ya
kuwa mfuko wa kwanza nchini kutoa huduma ya mikopo ya nyumba za makazi kwa
wanachama wake.
Alisema ili kulipa mafao
bora PSPF imekuwa ikihakikisha michango ya wanachama wake inalindwa dhidi ya
mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi kwa kuwekeza kwenye vitega
uchumi vya muda mrefu ikiwemo majengo,hisa na dhamana za serikali na kwamba kwa
sasa baadhi ya vitega uchumi hivyo ni pamoja na jengo lenye ghorofa 35 ambalo
ni refu kuliko yote Afrika mashariki na kati lililozinduliwa hivi karibuni na
Rais Kikwete.
“Ndugu zangu wanachama na
msio wanachama mfuko wetu wa PSPF
umekuwa ukiimarika siku hadi siku…kiasi kwamba tumeweza kuwekeza katika maeneo
mengi nje na ndani ya nchi ninachowaomba ni kuendelea kutuunga mkono na
muachane na uvumi wa kuwa PSPF inaelekea kufilisika”.alisema Kaliko.
Akizungumzia kuhusu mpango
mpya wa kuchangia kwa hiyari alisema mpango huo umeanzishwa ili kukidhi haja
kwa watanzania wote ambao ni waajiriwa na wasioajiriwa na kwamba anayehitaji
kujiunga na utaratibu huo anaweza kuchangia kiasi chochote alichonacho
kinachoanzia shilingi 10,000 ambapo anaweza kuchangia kwa siku,mwezi na hata
mwaka kadri anapopata pesa.
Mkutano wa baraza la
wafanyakazi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi
mkoani Mtwara umefanyika jana mjini Masasi kwenye ukumbi wa chuo cha
maendeleo ya wananchi Masasi na kuhudhuriwa
na wajumbe kutoka katika vyuo vya Mtawanya,Newala na Masasi wakiwa wenyeji huku
mada mbalimbali kutoka kwa watalamu mbalimbali zikiwasilishwa.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD