TANGAZO
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Masasi,Kazumari Malilo (Simba wa Yuda) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nanganga,kata ya Nanganga wilayani Masasi wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge jimbo la Ndanda ambapo amekanusha yeye kujiunga na Ukawa.
Na Mwandishi Wetu:Masasi.
MWENYEKITI wa chama
cha mapinduzi wilaya ya Masasi Kazumari Malilo (Simba wa Yuda) amekanusha
vikali uongo na uzushi uliokuwa umezagaa kwa siku za hivi karibuni wilayani
humo kuwa yuko mbioni kujiunga na umoja wa vyama vinavyounda ukawa kwa madai ya
kumfuata rafiki yake aliyehamia huko baada ya kubwagwa kwenye mchakato wa kura
za maoni ndani ya chama.
Aliyasema hayo jana
wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho kwenye jimbo la Ndanda mkutano
uliofanyika kwenye kijiji cha Nanganga wilaya ya Masasi ambapo alisema taarifa
hizo zilizosambazwa na wale aliowaita ni wapinzani wake wa muda mrefu kwenye medani za
kisiasa kuwa ni za uongo na uzushi zenye lengo la kudhoofisha harakati zake za kukirudisha
chama cha mapinduzi madarakani.
Alisema ni kwa muda
mrefu sasa amekuwa akisikia uzushi huo mitaani wa yeye kutaka kuhama CCM na
kuhamia Ukawa baada ya mgombea wa jimbo hilo aliyekuwa anaomba ridhaa kutoka
kwa wana CCM aweze kupeperusha bendera ya chama hicho Cesil Mwambe kubwagwa
kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya chama na Mariam Kasembe.
Alisema ni kweli
Cesil Mwambe alikuwa mtu wake wa karibu lakini ukaribu huo ulitokana na yeye kuwa
mwanachama wa chama cha mapinduzi lakini urafiki huo umekufa na kuzikwa rasmi
baada ya yeye kuhamia Chadema huku
akifananisha kitendo kilichofanywa na mgombea huyo kuwa ni sawa na “Kuuza panya
msikitini” ambapo alimtaka kusahau ndoto
zake za kuwa mbunge wa jimbo la Ndanda na kwamba atahakikisha haibuki kidedea
kwenye uchaguzi huo.
“Watu wamekuwa
wakinizushia uongo kuwa mimi Malilo nataka kuhama CCM na kuhamia Chadema
kumfuata Cesil Mwambe…natangaza rasmi mbele yenu kuwa sikuwahi kufikiria kuwa
na mpango huo na sina mpango huo yeye kama amehama ni uroho wake wa madaraka na
naomba kwa mungu wote waliotumika katika kusambaza uongo huo walaaniwe duniani
na mbinguni”.alisema Malilo huku akiomba dua kwa dini yake ya kiislam.
Alisema wako baadhi
ya wanachama wa chama cha mapinduzi walioenda kwa mgombea wa nafasi ya ubunge
jimbo la Ndanda kwenda kutoa taarifa kuwa yeye mwenyekiti wa CCM wilaya ya
Masasi hawezi kumuunga mkono Mariam Kasembe kitendo ambacho amekilaani
hadharani na kwamba yupo tayari kumpigia debe mgombea huyo wa CCM huku
akijinasibu kuwa chama chake kitaibuka kidedea.
Aidha Malilo alionesha
wazi kuchukizwa na vitendo alivyoviita kuwa ni vya kihuni na kejeli kutoka kwa
mwanachama wa chama hicho Constancia Ng’ombo aliyebwagwa kwenye kura za maoni
kwa nafasi ya udiwani kata ya Ndanda ambaye amekuwa akisambaza uvumi kuwa
uongozi wa CCM wilaya ulichangia yeye kuangushwa kwenye nafasi hiyo mazingira
yaliyopelekea kuhamia Chadema.
Alisema wanachama
wote wilayani humo waliohamia chadema akiwemo mwenyekiti wa umoja wa vijana
kata ya Nanganga Sadati Muhidini pamoja na wagombea wawili walioangushwa kwenye
mchakato wa kura za maoni ndani ya chama akiwemo Cesil Mwambe na Constancia Ng’ombo
wamefilisika kisiasa na kilichowapeleka huko ni uroho wa madaraka.
Alisema chama cha
mapinduzi wilaya ya Masasi kitashinda kwa kishindo kwa nafasi zote za ubunge na
udiwani na kwa kudhihirisha hilo tayari CCM imeshapita bila kupingwa kwenye
kata mbili za Chikoropola na Lupaso na kwamba kwa kata zote zilizobaki uwezo wa
kushinda ni mkubwa ambapo aliwaomba wanachama wa chama hicho kushikamana hasa
katika kipindi hiki cha uchaguzi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD