TANGAZO
MGOMBEA wa nafasi ya ubunge jimbo la Masasi Rashid Chuachua akiwahutubia wananchi na wanachama wa chama cha mapinduzi waliojitokeza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge pamoja na udiwani katika jimbo la Ndanda zilizofanyika leo kwenye viwanja vya shule ya msingi Sululu.
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
MGOMBEA wa nafasi ya
ubunge kupitia chama cha mapinduzi jimbo la Masasi Rashid Chuachua amewaomba
wanachama na wananchi wa jimbo hilo kumchagua ili aweze kuboresha sekta ya
kilimo kwa kurasimisha ardhi ya wakulima waweze kupata hati za kimila
zitakazowawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha nchini.
Pia ametoa matumaini
mapya kwa wafanyakazi wa sekta ya umma hususani walimu kwa kuwaahidi kuwa
endapo watamchagua na kuwa mbunge wa jimbo hilo atahakikisha wanalipwa stahili
zao ikiwemo malimbikizo ya mishahara kwa wale walimu waliopanda madaraja
sambamba na kutoa mafunzo kazini kwa walimu hao.
Aidha katika mkutano
huo uliohudhuriwa na viongozi pamoja na wanachama wa chama cha mapinduzi wakiongozwa
na katibu wa chama hicho mkoa wa Mtwara Shaibu Akwilombe,mgombea huyo aliweka
wazi vipaombele vyake kuwa ni pamoja na uchumi na uzalishaji,huduma za jamii
pamoja na namna atakavyoshughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa
jimbo la Masasi.
Akihutubia leo maelfu
ya wanachama wa CCM na wananchi wakati
wa uzinduzi wa kampeni za chama cha mapinduzi kwa nafasi ya ubunge na udiwani
kwa jimbo la Masasi zilizofanyika katika kijiji cha Sululu halmashauri ya mji
wa Masasi alisema anafahamu kero walizonazo wananchi wa jimbo la Masasi ikiwemo
maji,elimu na afya na kwamba wakimchagua kero hizo zitabaki kuwa historia.
Alisema sekta ya
elimu ambayo yeye ameifanyia kazi kwa takribani miaka 15 akiwa mwalimu ina
changamoto nyingi jimboni humo kama vile kuwepo kwa idadi ndogo ya wanafunzi
wanaojiunga kidato cha tano pindi wanapomaliza kidato cha nne huku akitolea
mfano kuwa kila mwaka wanafunzi 1800 humaliza elimu ya sekondari na wengi wao
hushindwa kuendelea ma masomo ya kidato cha tano.
Alisema ili
kukabiliana na tatizo hilo la wanafunzi wengi kutojiunga na kidato cha tano
atahakikisha kwa kushirikiana na wizara yenye dhamana ya elimu baadhi ya shule
za sekondari za kata zikarabatiwe na kuongeza majengo na miundo mbinu ya kisasa
ikiwemo maji na umeme ili ziweze kuwa za kidato cha tano na sita ili kupunguza
wimbi la wanafuzni wanaomaliza sekondari na wakishindwa kuendelea na masomo ya
kidato cha tano.
Aidha amehaidi
kushughulikia matatizo ya watumishi wa sekta ya afya ambao wamekuwa wakishindwa
kupewa stahili zao kwa wakati licha ya umuhimu wa kazi yao kwa jamii huku
akiweka wazi dhamira yake ya kuwa mbunge mwenye nia thabiti ya kupambana na
umaskini wa kipato unaowakabili wananchi wa jimbo la Masasi.
Akizungumzia mikakati
yake ya kuinua sekta ya kilimo Chuachua alisema atahakikisha pembejeo za kilimo
zinawafikia wakulima kwa wakati,kusimamia bei ya mazao kwa wakulima pamoja na
kutafuta masoko yenye tija sambamba na kujenga maghala makubwa na ya kisasa ya
kuhifadhia chakula kama akiba ili wakati wa upungufu wa chakula jimboni humo
wananchi waweze kununua kwa bei nafuu.
Alisema kwa
kushirikiana na mtandao wa wakulima vijijini MVIWATA atahakikisha wakulima
waliojiunga pamoja kwenye vikundi vya uzalishaji mali wanapatiwa mafunzo yenye
tija kwao yatakayosaidia kuinua kipato chao mazingira yakayosaidia kuondokana
na umaskini ambao amejinadi endapo atapewa ridhaa na wana Masasi basi suala
hilo kwao litamalizika.
BAADHI ya viongozi waandamizi wa chama cha mapinduzi wilaya ya Masasi wakiwa kwenye uzinduzi wa mkutano wa kampeni za nafasi ya ubunge na udiwani wa chama hicho uzinduzi uliofanyika hii leo kwenye viwanja vya shule ya msingi Sululu,Halmashauri ya mji wa Masasi.
Wanachama wa chama cha mapinduzi wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe wakiwa kwenye viwanja vya shule ya msingi Sululu wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge na udiwani wa chama hicho.
“Nafahamu kuwa wakulima
wengi wa jimbo la Masasi hawana uwezo wa kukopa fedha kwenye taasisi zinazotoa
mikopo kwa sababu hawakopesheki kwa kuwa wamekosa sifa…nitahakikisha mashamba
yote ya wakulima yanarasimishwa ili mpate hati miliki za kimila zitakazowawezesha
kukopa fedha benki ili mboreshe maisha
yenu na ya familia zenu”.alisema Chuachua aliyeshangiliwa na wananchi hao
wakati wote.
Aidha ameonya endapo
wananchi wa jimbo la Masasi watamchagua
na kuwa mbunge wao basi atakula sahani moja na maofisa wa ushirika ambao kwa
namna moja ama nyingine wanasababisha kero za wakulima jimboni humo huku
akisisitiza umuhimu wa kufanya ukaguzi wa hesabu za mara kwa mara kwa vyama vya
ushirika kwani hivyo ndivyo vinavyochangia kuzorotesha maendeleo ya wakulima.
BAADHI ya wanachama wa CCM wakifuatilia kwa makini vipaombele vya mgombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Masasi Rashid Chuachua wakati wa uzinduzi wa mkutano wa kampeni.
Rashid Chuachua akimwaga sera kwa wananchi wa jimbo la Masasi waliojitokeza kumsikiliza hii leo katika kijiji cha Sululu.
Kuhusu sekta ya
uchumi Chuachua alisema mji wa Masasi ni kitovu cha biashara kwa sasa huku
baadhi ya wakazi wa mji huo wakifanya biashara ndogondogo zisizo na tija kwao wakiwemo
madereva bodaboda pamoja na mama lishe na kwamba nia yake ni kuboresha biashara
hizo kwa kuwapa mafunzo ya ujasiliamali ili waweze kuunda vikundi
vitakavyowawezesha kupata mikopo ya kuboresha biashara zao.
Jimbo la Masasi lina
kata 14 likiwa ndani ya halmashauri ya mji wa Masasi huku jumla ya wagombea wanne kutoka kwenye vyama vya CUF,
NLD, CHADEMA pamoja na CCM wamejitokeza kwenye mtifuano huo wa kutafuta mgombea
mmoja atakayekuwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo hilo.
Bibi akifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM kwa nafasi za ubunge na udiwani kwa jimbo la Masasi kwenye viwanja vya shule ya msingi Sululu halmashauri ya mji wa Masasi.
WANACHAMA wa chama cha mapinduzi wakiwa kwenye viwanja vya uzinduzi wa kampeni
Wanachama wa CCM wakiwa kwenye viwanja vya shule ya msingi Sululu wakisikiliza sera kutoka kwa mgombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Masasi Rashid Chuachua.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD