TANGAZO
kikosi cha Timu ya watumishi wa idara mbalimbali katika Halmashauri ya wilaya ya Masasi ambayo ilishiriki mchezo wa mpira wa miguu katika bonanza maalumu lililofanyika kwenye viwanja vya sekondari ya Ndanda mwishoni mwa wiki.
Na Clarence Chilumba,
Masasi.
MKURUGENZI mtendaji
wa halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara Beatrice Dominick amewaomba
wakurugenzi wa halmashauri pamoja na taasisi zingine nchini kutekeleza kwa
vitendo sera ya elimu kuhusu michezo ili kudumisha ushirikiano miongoni mwa
watendaji wa serikali.
Aliyasema hayo jana
wakati anafanya mahojiano maalumu na habari leo kwenye uzinduzi wa bonanza la
michezo lililofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari Ndanda ambapo
alisema lengo la bonanza hilo ni kundeleza mahusiano ya kada mbalimbali kwenye
halmashauri hiyo.
Katika bonanza hilo
kuwahi kutokea kwa siku za hivi karibuni wilayani Masasi liliwashirikisha wakuu
wa idara na vitengo wa halmashauri hiyo,maofisa watendaji wa kata tano zilizo jirani na shule hiyo,wanafunzi,walimu
pamoja na watumishi wa shule ya
sekondari ya Ndanda huku michezo mbalimbali ikishindaniwa.
Alisema bonanza hilo
ni mwanzo mzuri kwao kwani hata wale watumishi ambao kwa namna moja ama
nyingine walitofautiana wakiwa kazini walipata muda wa kushirikiana pamoja
kwenye michezo mbalimbali na kwamba kwa kufanya hivyo ni dhahiri bonanza hilo
limesaidia kuzika rasmi tofauti za baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo.
Mgeni rasmi katika Bonanza la michezo la watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi ambaye ni Ofisa wa Kikosi cha kuzuia na kupambana na Rushwa wilaya ya Masasi Bw.Nestory Gatawa(kulia) akimkabidhi kikombe mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi Beatrice Dominick kwenye bonanza hilo.
KAMANDA wa kikosi cha kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU wilaya ya Masasi Nestory Gatawa akizungumza wakati anafunga bonanza la michezo lililofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Ndanda.
Akizungumza kamanda
wa kikosi cha kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Masasi Nestory
Gatawa alisema wadau wa michezo wanapaswa kuiga mfano uliooneshwa na mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Masasi kwa kufanya matamasha na mabonanza
ya michezo yenye lengo la kuimarisha ushirikiano.
Alisema kupitia
bonanza hilo watendaji wa serikali wa halmashauri hiyo wamepata fursa ya kuwa
pamoja na maofisa kadhaa wa Takukuru wilayani humo huku akikiri kuwa watendaji
wengi wa serikali wamekuwa na dhana kuwa Takukuru ni maofisa ambao hupaswi kuwa
nao karibu.
Kwa mujibu wa Gatawa
alisema Takukuru ni kama taasisi zingine za serikali na kwamba watendaji wa
serikali na wananchi waondoe hofu na mashaka juu ya taasisi hiyo huku
akisisitiza kuwa michezo nao husaidia harakati za kupoambana na rushwa kwa
kutoa elimu kupitia klabu za wapinga rushwa zilizopo mashuleni.
Kwa upande wake mkuu
wa shule ya sekondari ya Ndanda Morega Mongate ambaye ndiye muandaaji wa
bonanza hilo alisema serikali imekuwa ikihimiza michezo mashuleni katika
kutekeleza dhana nzima ya michezo mashuleni iliyopo kwenye sera ya elimu ili
kuibua vipaji vya michezo nchini.
Alisema licha ya
changamoto ya rasilimali fedha iliyopo kwenye shule nyingi nchini lakini wakuu
wa shule wanapaswa kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanapata fedha za kuandaa
mabonanza kama hayo kwa kuwa kupitia michezo wanafunzi hupata fursa ya
kujifunza masuala mbalimbali ya msingi ikiwemo kudumisha ushirikiano.
Aidha aliwaomba wakuu
wa shule nchini kuwa na mpango maalumu kuhusu michezo ili wanafunzi waweze
kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali huku akitiolea mfano kuwa katika
shule yao wamekuwa na utaratibu wa kuandaa mashindano ya mabweni, madarasa
pamoja nay a kutafuta vipaji vya wanafunzi katika michezo mbalimbali.
Ofisa elimu sekondari Halmashauri ya wilaya ya Masasi Paula Nkane (kushoto) akicheza mchezo wa "MDAKO' na Ofisa elimu Msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi Bi.Editha Fue wakati wa bonanza la michezo lililofanyika huko Ndanda mwishoni mwa wiki.
Mwalimu Jane Mbunda
ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Njenga halmashauri ya wilaya ya
Masasi alikuwa ni miongoni mwa washiriki wa bonanza hilo alisema amefarijika
kushiriki kwenye bonanza hilo kwani limesaidia kujenga mahusiano mazuri
sambamba na kuimarisha afya za watumishi wa halmashauri hiyo.
Timu za mpira wa miguu zikiwa zinajiandaa kabla ya kuanza mchezo huo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD