TANGAZO
Na Christopher Lilai,Nachingwea.
Kiwango cha unyonyeshaji wa maziwa ya mama wilayani Nachingwea
mkoani Lindi kimetajwa kuwa chini ya
kiwango ambapo ni wanawake wanane tu
kati ya 100 ndio wanaonyonyesha watoto wao ipasavyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Mratibu msaidizi wa afya
ya mama na mtoto wilayani Nachingwea Candida Mwambe wakati wa
maadhimisho ya kilele cha wiki ya unyosheshaji maziwa ya mama Duniani
iliyofanyika kiwilaya kijijini Mchonda mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema kutokana na tatizo hilo na matatizo mengine kumekuwa na ongezeko
la vifo vya watoto na akina mama wajawazito ambapo tangu mwaka 2011 hadi 2014
idadi ya watoto waliofariki imefikia 672 huku idadi ya vifo vya akina
mama wajawazito kwa kipindi hicho ikiwa ni vifo 35.
Mwambe alitaja mambo mengine yaliyochangia vifo hivyo kuwa
ni pamoja na upungufu wa wekundu wa damu ,udumavu, ukosefu wa vitamini A,uzito
mdogo wa watoto wakati wanapozaliwa na matumizi madogo ya chumvi
yenye madini joto.
Alitaja madhara mengine kuwa ni ongezeko la
watoto wagonjwa,matokeo mabaya shuleni,uzalishaji mdogo wa mazao ya
biashara na chakula hivyo kuathiri wananchi wa wilaya kwa jumla.
Akihutubia kwenye maadhimisho hayo,Katibu Tawala wa wilaya ya
Nachingwea,Saidi Moka ambaye alimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo Karole
Mgema,aliwaomba wananchi kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu watoa
huduma za afya ili kuwezesha kukabiliana na kuyashinda
matatizo hayo.
Alisema tafiti zinaonesha kuwa asilimia 60 ya vifo vya
watoto wachanga na wadogo chini ya miaka mitano vinachangiwa na lishe duni
ikiwemo ya kutonyonyesha maziwa ya mama kwa usahihi kunakotokana na ukosefu wa
elimu ya unyonyeshaji.
Aliwaomba wananchi kutumia chumvi iliyotiwa madini joto na
kuzingatia uhifadhi ulio mzuri ili madini joto hayo yasiharibike kwani madini
joto hayo uharibika kwa urahisi kama chumvi haikuhifadhiwa vizuri.
Alimwagiza mratibu wa mama na mtoto kuhahakikisha elimu ya
afya inayohusu ulishaji wa watoto kama wanawake wote wanapohudhuria
kliniki au kupata huduma nyingine.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD