TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Mtwara.
WAANDISHI wa habari
nchini wametakiwa kujiepusha kuandika au kutangaza habari za uchochezi ili
kujiepusha na migogoro isiyokuwa ya lazima kwani jamii imekuwa ikiwaamini waandishi
wa habari kuliko mtu mwingine yeyote.
Pia wameonywa
kutoegemea upande wowote kwa kuandika kwa upendeleo habari za baadhi ya
wagombea wakati wa mchakato wa kampeni
na siku ya upigaji kura na kwamba wanapaswa kutoa habari za wagombea wote wa
vyama bila kujali itikadi zozote za vyama vyao.
Ushauri huo umetolewa
na mkufunzi wa mafunzo kutoka shirika lisilo la kiserikali la Internews Wenceslaus
Mushi wakati wa mafunzo ya siku tano kwa waandishi
wa mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo alisema Taifa linawategemea waandishi wa
habari katika kutoa taarifa za uchaguzi mkuu oktoba mwaka huu.
Alisema waandishi wa
habari wanapaswa kupima habari gani inapaswa kutolewa kwa jamii ambapo pia
wanapaswa kuweka mazingira rafiki itakayosaidia kutokuwa na upande wowote wa
chama cha siasa.
Kwa mujibu wa Mushi
alisema ziko taarifa kwamba wako baadhi ya waandishi wa habari wanatumika
vibaya na wanasiasa kwa lengo la kutoa habari zao kwa kuhaidiwa nafasi za
uongozi ama fedha pindi watakapofanikiwa kuingia madarakani.
“Vyombo vya habari ni
lazima vijiandae kwa kutenga bajeti kwa waandishi wao wa habari wakati huu wa
uchaguzi…hii itasaidia kwa wanasiasa kutoa hongo kwa waandishi wa habari ili
waandike habari zao hata kama zikiwa mbaya na zisizo na faida kwa wananchi”.alisema
Mushi.
Alisema
katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye
uchaguzi mkuu waandishi wa habari wanapaswa kuripoti habari zenye uhakika
na usahihi zenye kuzingatia usawa kitu
ambacho kitawafanya wananchi kufanya maamuzi sahihi.
Kwa upande wake Christopher Lilai mmoja wa washiriki wa
mafunzo hayo alisema uamuzi wa shirika la Kimataifa la habari la Internews kutoa mafunzo hayo kwa waandishi
wa habari kutawasaidia wanahabari kutoa habari sahihi na zenye kuifahamisha
jamii.
Nae
Brigita Kambona mkufunzi kutoka Internews
kanda ya kusini alisema wanahabari watoe habari kwa kuzingatia makundi yote
ikiwemo wanawake,vijana,wazee pamoja na walemavu kwa kuwa makundi hayo mara
nyingi yamekuwa yakisahaulika.
Mafunzo
hayo ya siku tano yanafanyika mkoani Mtwara kwenye ukumbi wa Laso View na kushirikisha jumla ya waandishi wa habari 20 kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi lengo
likiwa ni kuwajengea uwezo kuelekea uchaguzi
mkuu oktoba mwaka huu.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD