TANGAZO
Na Mwandishi wetu,Ruangwa.
Maelfu ya wananchi Wilayani
Ruangwa wamejitokeza kwa wingi kumsindikiza Mgombea Ubunge
kupitia Chama cha Wananchi (CUF) jimboni
humo Omari Makota alipokwenda kuchukua
fomu ya Ubunge.
Msafara huo ulioanzia ofisi za CUF wilayani Ruangwa ulizunguka mji
wote huku kukiwa na Matarumbeta,Mavuvuzela, ngoma, magari 30,matrekta matatu
pamoja na umati mkubwa wa watembea kwa
miguu huku Jeshi la Polisi likiimarisha ulinzi.
Tukio hilo la aina yake kuwahi kutokea katika medani za siasa
wilayani humo limetokea juzi majira ya saa 8:30 alasili wakati mgombea huyo
anayeonekana kuwa na mvuto kwa wananchi wengi wilayani Ruangwa alipowasili
kwenye viwanja vya ofisi za msimamizi wa uchaguzi.
Mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo kutoka kwa msimamizi wa
uchaguzi jimbo la Ruangwa Nicholas Kombe, Makota aliyeambatana na mwenyekiti wa
CUF wilayani Ruangwa Omari Likiwila aliwaomba wakazi wa Jimbo la Ruangwa
kumuunga Mkono katika harakati zake za kugombea ubunge .
Alisema anatambua kuwa wananchi wana kiu ya mabadiliko na
kiu hiyo itaondolewa na yeye huku akijinasibu kuwa anao uwezo wa kuleta mabadiliko ya kimaendeleo
wilayani Ruangwa kwani anatambua fursa
mbalimbali zilizopo wilayani humo ambazo kwa sasa hazitumiki.
Kwa mujibu wa Makota alisema anazifahamu njia sahihi za kufika kwenye kilele cha mafanikio
na kwamba kwa muda wa miaka 16 aliyokuwa mtumishi wa umma amejifunza
mengi kubwa likiwa ni namna ya kupata maendeleo ya wananchi.
“Wilaya ya Ruangwa ni miongoni mwa wilaya zenye Rasilimali nyingi
kama vile madini,ardhi yenye Rutuba,Misitu… lakini imekosa viongozi
wa kuzisimamia fursa hizo na endapo mtanipa nafasi ya kuwatumikia
nitahakikisha fursa hizo zinatumika kwa manufaa ya Umma”. alisema Makota.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha Wananchi CUF Wilaya ya
Ruangwa Omari Liwikila alisema jimbo la
Ruangwa kwa kipindi cha takribani miaka
15 limekosa mwakilishi makini mwenye kuwatetea wakulima hasa katika suala zima
la soko na bei nzuri ya mazao yao.
“Tangia mwaka 2005 zao la Korosho limekosa bei nzuri badala yake
gharama za uendeshaji wa zao hilo zimekuwa kubwa ukilinganisha na bei ndogo ya shilingi
1000 ya Korosho inavyouzwa.
Akizungummzia kuhusu zao la
ufuta alisema mwaka 2013 kulikuwa na matumaini makubwa kwa wakulima wa zao hilo
wilayani humo baada ya zao hilo kuuzwa kwa kilogramu moja shilingi 2000
hadi 2500.
Alisema kutokana na usimamizi mbovu wa viongozi waliopewa dhamana
na wananchi kwa sasa matumaini yameanza
kutoweka kuanzia msimu wa mwaka 2014 /2015 baada ya zao hilo kuuzwa kwa bei ya
shilingi 1800 hadi 1500 kwa kwa
kilogramu moja.
“Wananchi wilayani Ruangwa huu ni mwaka wa mabadiliko…nawaomba
tuchague viongozi ambao watakuwa watetezi kwa kusimamia maslahi ya umma”.alisema
Liwikila.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD