TANGAZO
Na Mwandishi Wetu,Masasi.
MGOMBEA ubunge kupitia tiketi ya
Chama cha wananchi CUF katika jimbo la Masasi mjini Ismail Makombe maarufu kwa
jina la Kundambanda amechukua rasmi fomu ya kugombea jimbo hilo jana wilayani
Masasi tayari kwa kuanza kuomba ridhaa kwa wananchi ili ateuliwe kuwa mbunge wa
jimbo hilo.
Hatua ya Chama hicho kumsimamisha
mgombea huyo kugombea kiti cha ubunge katika jimbo la Masasi mjini huenda
kukaongeza mvutano uliopo ndani ya umoja wa Ukawa wilayani Masasi kwa kuwa
maamuzi ya Chama hicho yanakinzana na makubaliano ya umoja huo katika vikao
vyao vinavyoendelea kufanyika mjini hapa.
Makombe aliwasili jana majira ya
saa 8:30 katika ofisi za NEC Halmashauri ya mji wa Masasi akiongozana na
uongozi wa wilaya wa Chama hicho akiwemo mwenyekiti,Yusufu Matola na katibu
Hassan Chaliche ili kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa
kugombea ubunge kwenye jimbo hilo.
Katika siku za hivi karibuni
katibu wa Chama hicho,Hassan Chaliche aliweka wazi kuwa hata kama Ukawa
wilayani humo utaamua kumsimamisha mgombea mwingine kwenye jimbo hilo CUF
haitakubaliana na maamuzi hayo na kwamba itachukua hatua ya kumsimamisha
kundambanda kwa sababu ndiye mgombea anayekubalika na wananchi wa jimbo la
Masasi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya
umoja wa Ukawa Masasi zinasema kuwa CUF wamekuwa na mabishano makubwa na vyama
vya Chadema,NCCR mageuzi na NLD kuhusu utaratibu wa kumsimamisha mgombea katika
jimbo la Masasi mjini na kueleza kuwa mgombea wao kundambanda amekuwa
akihujumiwa kwa madai ya kigezo cha elimu aliyonayo.
Mvutano uliyopo ndani ya Ukawa
wilayani Masasi unatokana na taarifa kuwa majimbo ya Masasi mjini,Ndanda na
Lulindi yamekabidhiwa kwa Chama cha NLD ambapo Dkt, Emanuel Makaidi atasimama
kuomba ridhaa katika jimbo la Masasi huku jimbo la Lulindi atasimama mke wa
Makaidi na Ndanda ni Dkt.Mpelumbe taarifa ambazo zimeanza kuzua balaa ndani ya umoja huo wilayani Masasi.
Aidha kundambanda alipoombwa
kuzungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu juu ridhaa yake
ya kuomba kuteuliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo katibu wake chama cha CUF Hassan Chaliche alimkataza asizungumze chochote na waandishi wa habari kwa sasa.
“Msheshimiwa kundambanda
usizungumze chochote kama fomu umeshachukua tayari ingia ndani ya gari twende
tukafanye mambo mengine waandishi nawaombeni mtuache twende,”alisema Chaliche
huku akifunga mlango wa gari kwa jazba.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD