TANGAZO
Baadhi ya Watia nia wa nafasi ya Ubunge wakiwa kwenye kikao hicho. |
CHAMA Cha Mapinduzi Wilaya ya Masasi
Kimetoa Onyo kali kwa wanachama wa chama hicho ambao wametia nia ya kuomba kuchaguliwa katika nafasi za Ubunge kwa majimbo ya
Lulindi,Masasi na Ndanda kuwa waache Siasa za Chuki,Ubinafsi,Matusi pamoja na dharau
na kwamba watia nia wote wa chama hicho wilayani humo ni sawa.
Onyo hilo limetolewa leo na mjumbe wa Halmashauri kuu ya chama hicho wilaya ya Masasi Ramadhani Pole wakati wa kikao cha Maelekezo kwa watia nia hao kilichohudhuriwa na wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Masasi pamoja na uongozi wa juu wa chama cha mapinduzi wilaya ya Masasi.
Alisema tayari ofisi ya chama hicho imeanza
kupokea malalamiko kuwa baadhi ya wapambe wa watia nia hao wameanza kucheza
rafu kwa kutoa matusi kwa baadhi ya watia nia wa nafasi hiyo huku akiweka wazi
kuwa hata viongozi wa juu wa chama hicho akiwemo yeye mwenyewe,mwenyekiti wake
na katibu kuwa wamekuwa wakitumiwa ujumbe wa vitisho na matusi kutoka kwa
baadhi ya wapambe wa watia nia hao.
Alisema wapambe hao wamefikia hatua
ya kupiga picha za viongozi wa chama hicho wakiwa kwenye mazungumzo ya kawaida
na baadhi ya wagombea na kuzisambaza kwenye mitandao ikiwemo face Book na
WhatsApp kwa madai kuwa viongozi hao wamekuwa wakipanga mikakati ya kuwabeba
baadhi ya watia nia.
Kwa mujibu wa mjumbe wa Halmashauri
kuu ya CCM wilaya ya Masasi alisema watia nia kupitia chama hicho wamekuwa
wakitumia lugha za matusi na zisizo na heshima kwa viongozi na kwa wenzao huku
wengine wakiwadharau watia nia wenzao kuwa hawana elimu na sifa za kutosha kuwa
wabunge wa majimbo hayo matatu ya wilaya ya Masasi yenye ushindani mkubwa.
“Sisi kama viongozi wenu wa chama
hatuna makundi yoyote…na kamwe hatuwezi kumbeba mgombea yoyote tuko hapa kwa
ajili ya kupokea malalamiko kutoka kwa watia nia wengine ambao ni dhahiri
wanadharauliwa na msimamo wetu kama chama ni kwamba mtia nia yoyote
tutakayembaini kufanya vitendo hivyo tutashughulika nae”.alisema Pole.
Alisema wako baadhi ya watia nia
ambao waliwahi kugombea nafasi hizo kwenye uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2010
lakini katika hali ya kusikitisha na kustaajabisha baadhi yao waliacha kupita
ofisi za chama hicho wilaya kutokana na hasira walizokuwa nazo baada ya majina
yao kutopata kura za kutosha kugombea nafasi ya ubunge kwenye majimbo hayo.
MMOJA wa Watia nia wa nafasi ya ubunge jimbo la Masasi Bwana Geoffrey Katali Mwambe.
Alisema ni vyema watia nia wote
wakawa na moyo wa umoja na kuaminiana na watia nia wenzao huku wakiaswa kuwa kurushiana
kwao maneno ya kashfa na matusi kama ilivyo sasa kutatoa nafasi kwa vyama vya
upinzani kushinda kirahisi nafasi hizo kitu ambacho amekiri kuwa chama cha
mapinduzi hakitakuwa tayari kuona upinzani Masasi ukishinda.
“Nimekuwa nikipokea simu za
matusi,kashfa,dharau na vitisho kutoka kwa wapambe wenu …rai yangu kwenu nyie
watia nia waambieni wapambe wenu wawe na adabu kwa viongozi wa chama na waache
makundi kwani mwisho wa siku mgombea anatakiwa kuwa mmoja ambaye wote tutamuunga
mkono ili chama chetu kipate ushindi wa kishindo”.alisema huku akionesha
kukasirishwa na vitendo hivyo.
Aidha pole alisisitiza kuwa
hatokubali kuona wilaya ya Masasi iwe na tabia ya baadhi ya maeneo nchini
ambayo wanachama wa CCM wanaokosa nafasi za kugombea nafasi mbalimbali kwenye
chama hicho ikiwemo udiwani na ubunge kuhama chama hicho na kujiunga na vyama
vingine vya upinzani huku akitoa onyo kwa watia nia hao kuendelea kubaki CCM
hata kama wakikosa nafasi za ubunge na udiwani.
Kwa upande wake katibu wa chama cha
mapinduzi wilaya ya Masasi Mwanamasudi Pazzy alisema lengo la kikao hicho ni
kutoa maelekezo kwa watia nia hao kwa namna watakavyoshiriki kwenye zoezi la
kampeni linalotarajia kuanza julai 25 mwaka huu ambalo litakamilika ndani ya
siku sita ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kutoka kwa wanachama wa chama hicho.
Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara ina
majimbo matatu ya Ndanda,Lulindi na Masasi ambapo hadi sasa jumla ya watia nia
13 wamechukua fomu na kuzirejesha hii leo kwenye ofisi za chama cha mapinduzi
wilaya ya Masasi huku ushindani mkubwa ukiwa kwenye jimbo la Masasi ambalo lina
jumla ya watia nia saba akiwemo mhariri wa gazeti la Mtanzania Mike Mande.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD