TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Mkurugenzi wa biashara, Uwekezaji na
Sekta za Uzalishaji wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Geoffrey
Mwambe amesema wana CCM wenzake pamoja na wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama
hicho jimbo la Masasi watakaoketi
kuchagua jina moja la mgombea wa chama hicho wanapaswa kufanya maamuzi sahihi
katika kumpata mgombea huyo.
Geoffrey ambaye ni miongoni mwa wagombea
wa nafasi ya ubunge ndani ya CCM jimbo la Masasi, aliyasema hayo jana wakati anazungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ndani
ya chama cha mapinduzi jimbo la Masasi.
Alisema kiongozi bora anapaswa
kupimwa kwa vigezo vya utendaji bora na uliotukuka kazini na kusema kuwa endapo wana CCM jimboni humo watampa
ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho na hatimaye kushinda kwenye
uchaguzi mkuu ujao atahakikisha jimbo la Masasi linarudi katika hadhi yake.
Alisema ameamua kugombea nafasi hiyo
kwa kuwa jimbo la Masasi kwa sasa limerudi nyuma kimaendeleo mazingira
yanayopelekea kukosa kuwa na miundombinu bora ikiwemo barabara za mitaa na maeneo
mazuri ya kufanyia biashara huku akiweka wazi vipaombele vyake kuwa ni elimu,Afya,Maji,
Kilimo,Viwanda pamoja na miundo mbinu
itakayosaidia kuchangia upatikanaji wa fursa za ajira kwa kundi la vijana.
Kwa mujibu wa mgombea huyo wa ubunge
jimbo la Masasi alisema wananchi wa
jimbo la Masasi kwa sasa wanamuhitaji mgombea mwenye uzalendo na mwenye nia
thabiti ya Kupambana na Umaskini wa kipato unaowakabili wana Masasi kwa kujenga
viwanda vidogo vidogo,kuimarisha mfumo wa ununuzi wa zao za Korosho na
kuanzisha Benki ya Maendeleo ya wananchi wa Masasi.
“Jimbo la Masasi limekuwa kama kichwa
cha mwendawazimu…nadhani wana Masasi kwa hapa tulipofikia tuseme inatosha
wakati wa mabadiliko makubwa ya uongozi ni sasa,tunahitaji mwakilishi anayeumwa
na umasikini wetu,mwenye muono wa mbali na atakayepigania maendeleo ya wananchi
wote wa Masasi hivyo rai yangu kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya ni kuepuka
kurudia makosa”alisema Geoffrey.
Alisema endapo atachaguliwa na chama
chake na hatimaye kushinda na kuwa mbunge wa jimbo hilo atasimamia na kuboresha
kikamilifu sekta ya elimu ambayo kwa sasa ni dhahiri imeshuka jimboni humo kwa
kusaidia upatikanaji wa fedha za kusomesha vijana wa mikoa ya kusini shahada za
ualimu wa masomo ya sayansi vyuo vikuu ili baadae waje kufundisha kwenye shule
za sekondari jimboni Masasi na mikoa wa kusini kwa ujumla.
Bwana Geoffrey Katali Mwambe mgombea wa Ubunge jimbo la Masasi.
Alisema kwa sasa yeye ni mwenyekiti
wa taasisi ya South Eastern Development Organization (SEDO) ambayo imekuwa
ikifanya kazi nyingi za maendeleo kwa mikoa ya kusini ikiwemo kusaidia upatikanaji
wa vifaa vya ujenzi shule ya sekondari ya SABODO mkoani Mtwara,kuleta walimu wa
masomo ya sayansi wilayani Masasi kutoka vyuo vikuu pamoja na kuishauri
serikali kuhusu mambo mbalimbali ya maendeleo kwa mikoa ya kusini huku akikiri
kuwa SEDO imefanya kazi nyingi za maendeleo.
Aidha Geoffrey alibainisha nia yake
thabiti ya kuitoa Masasi pale ilipo sasa kwa kuipelekea kwenye uchumi wa kati
utakaoenda sambamba na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo jimboni humo
ikiwemo viwanda vya ubanguaji korosho,alizeti pamoja na kiwanda cha kutengeneza
juisi ya matunda yatokanayo na zao la
korosho maarufu mabibo ambayo kwa sasa yemekuwa yakitumika kutengeneza pombe
pekee.
“Nimefanya mambo mengi sana ndani ya nchi hii
nikiwa pale Benki kuu kama mchumi mwandamizi na sasa kwenye wizara ya Afrika
Mashariki nikiwa mkurugenzi…si rahisi kuzungumza mambo yote lakini ukweli ni
kwamba wana CCM jimbo la Masasi wanapaswa kuwapima wagombea wa kiti cha ubunge
kwa vigezo na nadhani kwa sasa Geoffrey Katali Mwambe anafaa kuwa mbunge wa
jimbo la Masasi”.alisema Geoffrey.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa ununuzi
wa mazao kwa njia ya stakabadhi ghalani
alisema si mfumo mbaya ili kwa sasa unapaswa kuangaliwa upya na kuboreshwa ili
basi uweze kuleta tija kwa wakulima ambao ni kwa miaka mingi wamebaki kuwa
maskini na kwamba endapo atapewa ridhaa hiyo atahakikisha matatizo ya wakulima
jimboni humo yanabaki kuwa historia.
Geoffrey Mwambe anakuwa mgombea wa tano hadi jana kuchukua fomu ya
kuomba ridhaa kwa wana CCM wa jimbo la
Masasi ili aweze kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao
oktoba mwaka huu,wengine ni Rashid Chuachua, Margreth Mtaka, Joseph Nkata na Regnald Kombania.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD