Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

Story Kubwa Leo Tz,Arfi Aibukia CCM,Shibuda atimkia TADEA,CCM yazuia Mafuriko kwa Mikono,zote hapa

TANGAZO
 HABARI LEO
MBUNGE wa jimbo la Mpanda Mjini kwa miongo miwili, Said Amour Alfi (Chadema) amejiunga rasmi na CCM. Amekuwa miongoni mwa makada 23 wa chama hicho, waliochukua na kurejesha fomu za kuomba kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Arfi amechukua fomu kuwania ubunge katika jimbo jipya la Nsimbo, wilayani Mlele. Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, chini ya uongozi wa Freeman Mbowe, alitangaza kujivua uanachama wake Chadema hivi karibuni katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi Kashaulili mjini Mpanda, huku akisisitiza kuwa alikotoka alichoshwa na siasa za kinafiki.
Akizungumza na mjini Mpanda, jana, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Katavi, Averin Mushi amethibitisha kuwa Arfi alichukua na kurejesha fomu za maombi ya kugombea ubunge katika jimbo jipya la uchaguzi la Nsimbo kwa tiketi ya CCM .
Hivi karibuni , Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza majimbo mapya ya uchaguzi, ambapo Jimbo la Katavi limegawanywa na kuanzishwa kwa majimbo mawili ya Uchaguzi ya Nsimbo na Kavuu.
Akitangaza idadi ya makada wa CCM waliorejesha fomu za kuomba kugombea ubunge katika majimbo manne ya uchaguzi mkoani humo, Mushi alieleza kuwa hadi pazia lilipokuwa likifungwa Jumapili, makada 23 wa chama hicho, akiwemo Arfi, walikuwa wamerejesha fomu zao .
Alisema kuwa katika Jimbo la Nsimbo makada waliorejesha fomu ni pamoja na Arfi, Shaaban Hassanali “Dallah”, Richard Mbogo, Manamba Emmanuel na Mapesa Frank.
Alitaja makada waliorejesha fomu jimbo la Katavi kuwa ni Isaack Kamwele, Meneja wa Tanroads mkoa wa Katavi na Shafi Mpenda ambaye ni Mhasibu wa kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha gazeti hili na magazeti dada ya Daily News, Sunday News, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo.
Wengine ni Maganga Kampala na Oscar Albano. Alisema katika jimbo jipya la Kavuu, waliorejesha fomu ni Zumba Emmanuel Mselem, Abdallah Saida ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Katavi na Prudencia Kikwembe, Mbunge Viti Maalumu.
Kwa mujibu wa Mushi katika jimbo la Mpanda Mjini, waliorejesha fomu ni Sebastian Kapufi, Gallus Mgawe na Gabriel Mnyele. Katika jimbo la Mpanda Vijijini waliochukua na kurudisha fomu ni Moshi Kakoso, Abdallah Sumry (mbunge wa zamani wa jimbo hilo) , Willy Makufe, Elizabeth Sultan, Godfrey Nkuba, Rock Mgeju na Chifu Charles Malaki.
Arfi aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, kabla ya kujiuzulu wadhifa huo na baadaye kujivua uanachama hivi karibuni aliwahi kutuhumiwa na Chadema kumsaidia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kupita bila kupingwa katika Jimbo la Katavi (CCM) kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010 kwa kuwashawishi baadhi ya wagombea kuondoa majina yao.
Hata hivyo, Arfi amekuwa akikanusha tuhuma hizo na kusababisha kutokuelewana na baadhi ya viongozi wenzake ambapo alifikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa Novemba 22, mwaka 2013 kwa kile alichosema amechoshwa na siasa za kinafiki ndani ya chama hicho.
Aidha, katika waraka wake wa kujiuzulu Umakamu Mwenyekiti, alisema hakuwa tayari kubanwa na hata kuchaguliwa aina ya marafiki. Sehemu ya waraka huo inasomeka:
“Kwa kipindi kirefu zimekuwepo shutma dhidi yangu na kutiliwa mashaka mahusiano yangu na Mheshimiwa Pinda (Mizengo), Waziri Mkuu pamoja na kulijadili katika vikao kadha Mpanda na Dar es Salaam, bado yapo mashaka kwa nini alipita bila kupingwa hayo yalikuwa maamuzi ya Wanampanda kwenu imekua ni tatizo, lakini hamsemi kwa nini majimbo mengine 16 nchini yalipita bila kupingwa.
Mlikuwa wapi na nani alaumiwe? huu ni unafiki wa kupindukia. “Aidha mmechukizwa sana kwa nini nilihoji kauli ya Mwasisi wa Chama Mheshimiwa Mtei (Edwin) kutuchagulia viongozi naomba ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo wangu na utabakia hivyo siku zote kwa chama cha demokrasia kutoruhusu uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya waasisi ambao huvigeuza vyama kuwa mali binafsi.”
MWANANCHI
Baadhi ya wabunge wa Chadema wamezungumzia taarifa zinazosambaa zikieleza kuwapo mkakati wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia katika chama hicho, wengi wao wakimkaribisha.
Wakati wabunge hao wakikubali kumpokea, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa amesema wananchi wasubiri mambo yatakapokuwa tayari badala ya kutegemea mitandao ya kijamii.
“Nitazungumza pale mambo yatakapokuwa sawa, siwezi kuzungumza sasa, subirini… sasa hivi mambo mengi yanazungumzwa kwenye mitandao,” alisema Dk Slaa ambaye pia anatajwa kuwa mgombea wa chama hicho ndani ya Ukawa.
Msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa mpango huo alisema hawezi kulizungumzia hilo kwa kuwa ni suala la mtu binafsi. Hata hivyo, jitihada za kumpata Lowassa jana hazikufanikiwa kwani simu yake iliita pasi na kupokewa.
Hivi karibuni, idadi kubwa ya madiwani wa CCM walirudisha kadi zao na kujiunga na Chadema wakisema sababu ni kutoridhishwa na kukatwa kwa jina Lowassa kati ya wagombea urais wa CCM.
Kadhalika, mtandao wa kijamii uliokuwa ukimuunga mkono mbunge huyo wa Monduli unajulikana kwa jina la 4U Movement ulitangaza kuhamia Chadema hali inayoashiria kuwa kuna dalili ya Lowassa pia kujiunga nao.
Wakiandika katika akaunti ya Twitter ya 4U Movement, wafuasi hao walisema: “Ukimya ni hekima na ukimya ni busara. Ukimya wa Edward Lowassa ni kutafakari Safari ya Matumaini... Tuungane kuyapata mabadiliko nje CCM.”
Chadema ni kanisa la wokovu
Akizungumzia taarifa hizo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alikifananisha chama hicho na kanisa ambalo kwa kawaida halikatai mtu, bali linawapokea wenye dhambi na kuwaongoza kufanya toba.
“Chadema ni kama kanisa, hakataliwi mtu, tunahubiri habari njema ya wokovu, ukija hapa unatubu unaendelea kufanya kazi,” alisema.
Kuhusu viongozi wa CCM kuhamia Chadema, Msigwa alisema inawezekana kasi hiyo inachagizwa na Lowassa kukosa nafasi aliyoitaka ndani ya chama hicho.
“Unapokuwa mwanasiasa unakuwa na wafuasi, inawezekana wengine wanaohamia Chadema ni watu wake ambao wameona mtu wao amekosa nafasi aliyoitaka ndiyo maana wanakihama chama,” alisema.
Msigwa alisema Chadema ilikuwa inakusanya wanachama wapya kwa muda mrefu hata kabla ya vuguvugu la Lowassa na chama chake kuibuka na ushindi na wanaohamia wanafanya hivyo kwa sababu wanakipenda chama na wameichoka CCM.
Huenda akatimiza safari ya matumaini
Akizungumzia ujio wa Lowassa kwenye chama hicho, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema iwapo Lowassa atahamia Chadema anakaribishwa na huenda akaitimiza safari yake ya matumaini.
“Namkaribisha Lowassa Chadema, huenda safari yake ya matumaini ikaishia huku, akawa mwanachama au hata kiongozi,” alisema.
Alisema hakuna shaka kuwa mbunge huyo wa Monduli ana nguvu ndani ya CCM ndiyo maana viongozi wengi wa chama hicho wanakihama wakati huu.
“Hiyo ilijionyesha kuanzia kwenye Kamati Kuu ya CCM, Halmashauri Kuu, Lowasa amekamata wajumbe kwa asilimia 80 na hiyo ni ishara kuwa ameishika CCM,” alisema.
Lema aliongeza kuwa wanaoihama CCM hawaihami kwa bahati mbaya, bali wameona mtu wao waliyemtarajia ameondoka.
“Ni wengi wanaohamia Chadema, kwa sasa kadi zimetuishia na hiyo ni ishara kuwa CCM inakufa, ripoti za mikoa yote tunazo,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya alisema  wanaoihama CCM kwa sasa wamegundua kuwa chama pekee kinachoweza kutetea wananchi ni Chadema.
“Sisi tunawakaribisha kwa mikono miwili, waje tuchape kazi, ilimradi wanafuata kanuni na taratibu za chama, basi.  Wamejionea wenyewe kuwa CCM hakuna chochote,” alisema.
 Alisema CCM waliamua kupitisha katiba bila kuwapo kwa Ukawa, lakini sasa wameona kuwa walichokifanya ni makosa na wameanza kurudi Chadema ambako wanaamini kuna demokrasia ya kweli.
Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso alisema: “Tunamkaribisha kwa mikono miwili. Tumekinyooshea CCM vidole kwa muda mrefu kuwa kuna rushwa na makundi na hilo linajidhihirisha sasa. Lakini wale wote wanaokuja Chadema, tunawakaribisha ili mradi wafuate kanuni na taratibu zetu.”
Paresso alisema hana tathmini ya kina kuhusu wafuasi wa Lowassa wanaoihama CCM, bali wanaokihama chama hicho wameona kina matatizo.
Atakiwa akidhi vigezo na masharti
Licha ya kuonyesha kumkaribisha, katika chama hicho, baadhi ya wabunge walimtaka Lowassa afuate kanuni ili awe mwanachama mwenye sifa.
Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde alisema anakaribishwa lakini hana budi kufuata sheria na kanuni za chama... “Anatakiwa afuate taratibu za chama, milango ipo huru, lakini afuate kanuni… asije akafikiri ataleta taratibu zake hapa, sitakubali.”
Silinde alisema wanaohamia Chadema hawajapendezwa na mwenendo mzima wa uteuzi wa mgombea wa urais na hivyo wameifuata demokrasia ya kweli ndani ya chama hicho.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo lakini alisema endapo atajiunga, chama hicho kitampokea kulingana na vigezo na taratibu.
“Akihamia Chadema nitatoa maoni yangu lakini ninachoweza kusema ni kuwa kila mtu ana haki ya kwenda chama chochote ili mradi ana tija,” alisema.
Mdee alisema wanaCCM wanaohamia Chadema wamesoma alama za nyakati na kuona kuwa CCM haiendani na ahadi zake.
Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo alisema, Lowassa ni binadamu wa kawaida kwa hiyo kuhamia kwake Chadema si kitu cha ajabu ilimradi afuate kanuni... “Cha muhimu afuate masharti ya chama, kanuni na  taratibu, kama watu wanahama vyama vingine yeye ni nani asihame CCM?”
Lyimo alisema wanaCCM wengine wanakaribishwa kujiunga kwa sababu kwenye siasa hakuna rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu.
Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul, aliwataka wana CCM na Lowasa kuhamia zaidi  Chadema ili kuunganisha nguvu na kuichukua nchi.
 “Mfikishie salamu Lowassa mwambie karibu kwenye jeshi la ukombozi,” alisema.
Katibu wa CCM amuonya
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma, Katibu wa CCM mkoa huo, Albert Mgumba alisema ingawa kuhama chama ni hiari ya mtu, Lowassa hapaswi kuchukua uamuzi wa hasira kiasi hicho badala yake awe mstari wa mbele kuhamasisha umoja ndani ya chama.
Alimtaka kutothubutu kuihama CCM na endapo afanya uamuzi huo atambue kuwa hawezi kukisababishia pengo lolote zaidi ya kujipunguzia hadhi yake ya kisiasa.
“Mgombea tuliyempata sasa ni makini kuliko, anapendwa, utendaji wake unajulikana kila mahali,” alisema Mgumba.
Mgumba alisisitiza kuwa badala ya Lowassa kuwa na mawazo ya kuihama CCM, anapaswa kutuliza fikra na kuonyesha ukomavu wake kisiasa kwa kuwa mstari wa mbele kuwaonya na kuwatuliza wote waliokuwa wakimuunga mkono ili wabaki kwa utulivu ndani ya chama na si vinginevyo.
“CCM siyo Mgumba, ni taasisi iliyosimama. Lowassa anapaswa kutambua hilo, atulie na awe mstari wa kwanza kuwaonya wanachama wachanga kisiasa, wasiokuwa na uzalendo ndani ya chama kwa kumfikiria mtu badala ya chama na masilahi ya Taifa” alisema Mgumba.
MAJIRA
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limefanikiwa kukamata majambazi watano waliohusika kwenye tukio la uvamizi
wa Kituo cha Polisi Sitakishari, Julai 12, mwaka huu.

Katika tukio hilo, majambazi hao wanaokadiriwa kufikia 16 hadi 18, waliua askari polisi wanne, raia watatu, kujeruhi watu wanne akiwemo polisi mmoja, kupora silaha ambazo idadi yake haifahamiki.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, alisema baada ya tukio hilo, jeshi hilo lilianza operesheni maalumu likishirikisha vikosi mbalimbali.

Alisema Julai 17, mwaka huu, zilipatikana taarifa za kuaminika kuwa maeneo ya Tuangoma, Mkoa wa Kipolisi Temeke, kulikuwa na majambazi waliohusika kwenye tukio la ujambazi wa Kituo cha Sitakishari ambao walikuwa wakijiandaa kufanya uhalifu.

Jeshi hilo kupitia kikosi chake maalumu, kilikwenda eneo la tukio na kuweka mtego ili kuwanasa majambazi hao ambapo askari wa kikosi hicho, waliwasimamisha watu watano waliokuwa wamepakizana katika pikipiki mbili; lakini walikaidi kusimama na kuanza kurushiana risasi na polisi.

"Polisi waliwazidi nguvu watu hao na wote walikamatwa; watatu kati yao walikuwa wamejeruhiwa vibaya na kufariki dunia wakiwa njiani kukimbizwa hospitali ambao ni Abbas Hashim (mkazi wa Mbagala), Yassin (mkazi wa Kitunda Kivule) na Said (mkazi wa Kivule, Kijiji cha Mandimkongo Mkuranga).

"Watuhumiwa wawili, Ramadhani Ulatule (15), mkazi wa Kijiji cha Mandimkongo Mkuranga na Omary Amour (24), mkazi wa Mbagala Kimbangulile, walipatikana na kuhojiwa...katika tukio hilo ambapo ilipatikana bunduki moja aina ya SMG ambayo namba zake zilifutwa ikiwa na risasi 25," alisema Kamishna Kova.

Aliongeza kuwa, Julai 19, mwaka huu, jeshi hilo lilipata habari za kuaminika juu ya silaha zilizoporwa Kituo cha Sitakishari; kufichwa Mkoa jirani wa Pwani zikiwa porini katika eneo lisilofahamika vizuri.

Kundi kubwa linaloundwa na vikosi mbalimbali vya polisi, lilienda mkoani humo na kufanya msako katika Kijiji cha Mandimkongo, Kata ya Bupu, wilayani Mkuranga, katika msitu, kikosi hicho kilifukua kwenye shimo na kufanikiwa kupata bunduki 15 kati ya hizo, saba aina ya SMG, saba aina ya SAR, magazine moja ya SMG na risasi 28.

Kamishna Kova alisema, kati ya silaha zilizokamatwa, 14 ni za Kituo cha Sitakishari na mbili za majambazi wenyewe ikiwemo silaha moja aina ya Norinko ambayo inafanyiwa uchunguzi ili kujua iliibwa wapi.

Katika shimo hilo pia zilipatikana fedha taslimu za Tanzania sh. milioni 170 ambazo zilifungwa kwenye sanduku maalumu ambapo Kamishna Kova aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kulitokomeza kundi linalovamia vituo vya polisi, kuua askari, kupora silaha kwa kutumia usafiri wa pikipiki.

Aliongeza kuwa, jeshi hilo linawatafuta watu wengine waliotajwa kwa majina ya Abdulazizi Abdulrashid au Ustaadhi Abdulaziz, mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni kiongozi wa kundi la wahalifu hao.

Wengine ni Shaban Mtumbuka au Amir Shaban Ndobe, Hannafi Kapela kwa jina maarufu Mkamba au Shekhe Hannafi, Hassan Issa (Dk. Shujaa), Zahaq Ngai (Mtu Mzima), Abubakar Ngindo (Abu Muhammad) na Khamis Ramadhan.

Alisema mbali na jeshi hilo kutoa donge nono la sh. milioni 50 kwa mtu ambaye atatoa taarifa ambazo zitafanikisha kukamatwa kwa majambazi wengine na silaha, jeshi hilo limeahidi kuongeza dau zaidi likiwataka wananchi waendelee kutoa taarifa hizo.

MAJIRA
KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe, leo ataongoza mapokezi makubwa ya Mbunge wa Kasulu Mjini, mkoani Kigoma, Bw. Moses Machali (NCCR-Mageuzi), ambaye atatambulisha rasmi kuwa mwanachama wa ACT- Wazalendo.

Bw. Machali ataambatana na Madiwani wawili, Kamishna wa Mkoa mmoja, Katibu wake, Wenyeviti na Makatibu wa kata 12 zilizo kwenye Jimbo la Kasulu Mjini.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na ACT-Wazalendo, ilisema katika mapokezi hayo, Bw. Kabwe pia atawapokea Makatibu Uenezi tisa wa jimbo hilo lenye jumla ya kata 15 za uchaguzi.

Mbali na viongozi hao, wengine ambao wataambatana na Bw. Machali kujiunga ACT-Wazalendo ni Wenyeviti 101 wa Matawi na Makatibu 98 na wanachama 648 wote kutoka NCCR-Mageuzi, jimboni humo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya mapokezi hayo, Bw. Kabwe atakwenda mkoani Shinyanga kuwapokea viongozi, madiwani kutoka vyama mbalimbali Julai 25, mwaka huu.

Julai 26, mwaka huu, Bw. Kabwe atakutana na watia azma wa nafasi ya ubunge katika majimbo ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuweka mikakati ya ushindi wa kishindo.

Wakati Bw. Kabwe akiwa mkoani kwa ajili ya kuwapokea wanachama wapya, jijini Dar es Salaam Julai 22, mwaka huu, viongozi wengine watakuwa na jukumu la kuwapokea wanachama na waliokuwa madiwani katika vyama tofauti vya siasa nchini.

MAJIRA

HATIMAYE Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, mkoani Shinyanga,  kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. John Shibuda ametangaza rasmi kugombea tena ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Tanzania Democratic Alliance (TADEA).

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Bw. Shibuda alisema ameamua kugombea kwa tiketi ya TADEA ili aendeleze shughuli mbalimbali za maendeleo alizozianza jimboni humo akiamini wapigakura wake wataendelea kumuunga mkono kama ilivyokuwa mwaka 2010.

Alisema suala la kuwatumikia wananchi haliangalii chama cha siasa; bali mgombea na wanachozingatia wapigakura ni kuangalia kiongozi gani ana maono ya kusukuma mbele maendeleo ya jimbo lao.

"Nimeamua kutetea tena kiti changu cha ubunge kwa tiketi ya TADEA ambacho nimejiunga nacho hivi karibuni, bado nina deni la kuwatumikia wananchi wangu wa Maswa Magharibi, wanachohitaji ni maendeleo si chama cha siasa ninachopitia kugombea ubunge.

"Nawaomba wapigakura wa jimbo langu, waendelee kuniunga mkono kama walivyofanya katika Uchaguzi Mkuu 2010 nilipohama CCM na kugombea kwa tiketi ya CHADEMA kilichojaa mizengwe; sasa nimehamia TADEA, wasiangalie chama, waangalie uchapaji kazi wangu," alieleza Bw. Shibuda.

Wakati Bw. Shibuda akitangaza rasmi kutetea kiti chake cha ubunge, aliyekuwa mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa 2010 kwa tiketi ya CCM, Bw. Robert Kisena, inadaiwa ameshindwa kujitokeza  ili kuchukua fomu ya kuwania ubunge wa jimbo hilo.

Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka Ofisi ya CCM, wilayani Maswa, zimewataja makada watano wa chama hicho waliojitokeza kuomba kugombea ubunge ambao ni Marco Bukwimba, Mashimba Ndaki, Benjamin Tungu, Aron Mboje na Henry Nditi.

Jimbo la Maswa Mashariki linatetewa na Sylivestor Kasulumbayi (CHADEMA), ambapo hadi sasa, wanachama wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Peter Bunyongoli na Jonathan Ngela.

Wengine ni mwanasiasa mkongwe, George Nangale ambaye ni mmiliki wa Kituo cha Redio Sibuka FM, Stanslaus Nyongo, Ally Ntegwa na George Lugomola.
 

JAMBO LEO
MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ametoa siri ya moyoni kwamba kashfa ya sakata la fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow lilimkutanisha na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilali ili kumueleza ukweli wa sakata hilo.
Vilevile, amesema Dk. Bilal ndiye kiongozi pekee wa Serikali ambaye alionesha dhahiri kuwa aliguswa kutokana na wizi huo wa fedha za umma.
Kafulila alisema hayo wakati akipokea tuzo ya Mtanzania mwenye maono mapevu iliyotolewa juzi na Taasisi ya Dream Success Enterprises, jijini Dar es Salaam.
Alisema ametoa siri hiyo sasa kutokana na ukweli kuwa kiongozi huyo wa pili kwa madaraka nchini kumuita na kufanya mahojiano naye kwa saa nne kuanzia saa nne usiku hadi saa nane ili kumueleza kuhusu sakata hilo hiyo ikiwa ni baada ya kupotoshwa na watendaji wa Serikali.
Mbunge huyo alisema, baada ya kuitwa alipata wasiwasi mkubwa kwani haijawahi kutokea, akalazimika kuwataarifu ndugu zake kuwa ameitwa na makamu wa rais hivyo asiporejea wajue kwamba aliitwa na kiongozi huyo.
Kafulila alisema baada ya kufika makamu wa rais alitaka kujua nini kipo katika sakata hilo hiyo ikiwa ni baada ya viongozi wanapokutana na mataifa yaliyoendelea, wahisani na mashirika ya fedha wanashindwa kuelewana hali ambayo ilichangiwa na upotoshaji wa watendaji.
Alisema alipofika alimueleza kila kitu kuhusu sakata hilo la Escrow ndipo Dk Bilal akapata ufahamu na kukiri kuwa alikuwa anadanganywa na watendaji wake hivyo kupatwa na huzuni kubwa kwa kuongea uongo mbele ya wahisani ambao walikuwa wanajua kila kitu.
“Katika sakata la Escrow kuna jambo ambalo sijawahi kulisema leo (juzi) nasema kwa sababu naona watu waadilifu hawathaminiwi, nakumbuka siku moja saa nne usiku niliitwa na Makamu wa Rais Dk. Bilal hadi sa nane ambapo alitaka nimueleze kila kitu ninachokijua kuhusu Escrow ili aweze kujieleza mbele ya watu mbalimbali jambo ambalo hakuna kiongozi mwingine wa Serikali alifanya hivyo.
“Nilikuwa na taarifa yenye takribani kurasa 600 nilitumia saa nne kumueleza kila jambo, ambapo kimsingi alionekana kuumia sana na aliniuliza hivi kweli rais anajua haya au na yeye yupo kama mimi huku akitikisa kichwa,” alisema Kafulila.
Mbunge huyo alisema kilichoonekana ni wazi kuwa watendaji wa Serikali waliamua kumdanganya au nao walikuwa hawajua jambo ambalo lilimsukuma kutaka kujua ukweli ulivyo.
Alisema pamoja na maelezo yote ambayo aliyatoa kwa Makamu wa Rais saa tisa usiku alifuatwa na watu ambao walikuwa na magari matatu wakimtaka asiseme yote ambayo yapo katika taarifa yake kwani mengine ni makubwa na hatari.
Mbunge huyo alisema siku hiyo umeme ulikatika, lakini watu hao walimpigia simu muda wote na kumtaka waonane aligoma ila baadae alikubali pamoja na ukweli kuwa umeme haukuwepo.
Kafulila alisema kutokana na uzalendo huo ambao Dk. Bilal alionesha aliamini kuwa ni mmoja wa Watanzania wazalendo na waadilifu, lakini katika jambo la kushangaza katika mchakato wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitisha majina ya wagombea walimkata bila kuingia hata tano bora.
“Kutokana na uadilifu wa yule mzee nilibakiwa na mshangao pale, ambapo CCM kupitia kamati yake ya maadili kumkata sijui wanatumia kigezo gani kuangalia uadilifu,” alisema.
Sakata la Escrow liliibuliwa na Kafulila ndani ya bunge, ambapo baadae lilifikishwa katika Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo ilifanyia uchuguzi na kutoa taarifa iliyosababisha bunge kutoka na maazimio nane ili Serikali itekeleze.
Baadhi ya maazimio hayo ni Serikali kuwawajibisha Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira (VIP), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania(Tanesco) walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda kwa makampuni ya Pan African Power Solutions Ltd. (PAP), na VIP Engineering & Marketing (VIP).
Pia, azimio lingine lilikuwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi watu wote waliotajwa na taarifa maalum ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea;
Bunge pia liliazimia Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Fredrick Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao;
Aidha azimio lingine la bunge lilikuwa ni Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka, na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao Wenyeviti tajwa wa Kamati husika za Kudumu za Bunge ambao walikuwa ni Andrew Chenge, William Ngeleja na Victor Mwambalaswa.
Azimio lingine lilikuwa ni kumtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Pia, azimio lingine lilikuwa ni mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi ziitaje Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. na benki nyingine yoyote itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (institutions of money laundering concern).
Bunge liliazimia pia, Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya Sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Aidha Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.
Azimio la nane la Bunge ni Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme jambo ambalo halikufanyika na kusababisha Kafulila kuomba muongozo ndani ya bunge kila mara kuhusu lini taarifa hiyo itawasilishwa.
NIPASHE
Wasira apata wapinzani Saba, Mwakyembe 9, Juma Nkamia 13, Wamo pia Kilango, Nyalandu, Nagu, Masele, Kamani.
Mawaziri kadhaa wa Rais Jakaya Kikwete wamekutana na upinzani mkali majimboni kutokana na kujitokeza kwa wanachama wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majimbo yao kuomba uteuzi wa kugombea ubunge kupitia chama hicho.

Aidha, baadhi ya wabunge wa CCM wamekutana na upinzani mkali pia baada ya makada wenzao wengi kujitokeza majimboni kuomba kuteuliwa.

WASIRA- BUNDA MJINI (8)
Katika jimbo lililomegwa upya la Bunda mjini, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, amepata wapinzani kupitia CCM ili waweze kupimana bana ubavu kuwania fursa ya kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. 
                                                                                              
Waliochukua fomu na kurejesha katika jimbo hilo ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya, mfanyabiashara Robert Maboto, Magesa Julius Magesa, Simoni Odunga, Peles Magiri, Isack Maela na Exvery Rugina.

FENELA MUKANGARA
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara, atachuana na makada sita katika jimbo jipya la Kibamba. Makada hao ni George Shayo, Mashaka Sabaya, Rashid Mrisho, Issa Jumanne, Felix Mdeka na Goodvido Shayo.

DK. MWAKYEMBE
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, mkoani Mbeya, atakabiliana na ushindani kutoka kwa makada tisa wa chama hicho.

Makada hao ni Gabriel Kipija, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, John Mwaipopo, Prof.Leonard Mwaikambo, Gwakisa Mwandembwa, Vincent Mwamakingula, George Mwakalinga, Benjamin Richard, Asajile Mwambambale na Ackim Jackson.

DK. MARY NAGU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu), Dk. Mary Nagu, anayemaliza muda wake wa kiliongoza Jimbo la Hanang’ atakutana na upinzani kutoka kwa Peter Nyalandu, Aliamani Sideyeka  na Mayomba Dankani.

CHIZA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Cristopher Chiza, atakabiliana na makada sita waliojitokeza katika jimbo lake la Buyungu. 

ANNE KILANGO
Mbunge wa Same Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango, anakabiliwa na kibarua kugumu baada ya makada nane kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge.

Hao ni Michael Kadeghe, Dk. Eliji Kibacha, Semi Kiondo, Abraham Shakuri, Nyangasu Werema, Daudi Mambo na Ombeni Mfariji.

PROF. MAGHEMBE
Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mwanga, Prof. Jumanne Maghembe, waliojitokeza kumpinga ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec), Anania Thadayo, Karia Magaro, Baraka Lolila, Amani Kidali, Ramadhan Mahuna na Japhari Mghamba.

DK. KAMANI 
Mbunge aliyeangushwa na ndugu yake katika kura za maoni 2010, Dk. Raphael Chegeni ni miongoni mwa watia nia saba waliojitokeza kumrithi mbunge wa Jimbo la Busega, Dk. Titus Kamani.

Licha ya Dk. Chegeni na Dk. Kamani kuchukua na kurejesha fomu, pia wapo wanachama wengine wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambao ni Benard Kibese, Igo Shing’oma, Dasias Sweya, Robert Nyanda, Nyangi Msemakweli na Josephat Kwamba.

JUMA NKAMIA
Naibu wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, anakabiliwa na upinzani kutoka kwa makada 13.

Makada hao ni mwanahabari mwandamizi, Khamis Mkotya, Fredi Duma, Juliana Magembe, Juliana Maghembe, Juma Ilando, Yusuph Ibrahim, Idd Kisisa, Raphael Kelesa, Francis Julius, Godfrey Mayo, Pascal  Degera, Athman Hotty na Pascal Afa.

NYALANDU 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, anachuana na wagombea saba akiwamo Justine Monko, Michael Mpombo, Othman Mungwe, Amos Makiya, Yohana Eliyasini Too, Aron Mbogo na Sabasaba Manase.

MAJIMBO YA KIFO

BUKOBA MJINI
Jimbo la Bukoba Mjini lina ushindani mkali kutokana na makada nane kujitokeza wakiwamo Mbunge aliyemaliza muda wake, Balozi Khamis Kagasheki na hasimu wake mkubwa wa kisiasa, Dk. Anatory Amani. 

Wengine ni Josephat Kaijage, George Rugahyuka, Filbert Katabazi, Elieth Projestus, Christina Rwezaura na aliyewahi kuwa Mbunge wa  jimbo hilo, Mujuni Kataraiya.

MULEBA KUSINI
Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleio ya Makazi, Prof. Anne Tibaijuka, ambaye ni Mbunge anayemaliza muda wake, Prof. Anne Tibaijuka, anakabiliwa na upinzani mkali baada ya makada tisa kujitokeza kuwania nafasi yake.

Mbali na Prof. Tinaijuka, wengine waliochukua na kurejesha fomu ni Dk. Adam Nyaruhuma, Stephen Tumain, Flavius Kahyoza, Buruan Rutabanzibwa, Muhaji Bushako, Kaino Mendes, Mnawaru Amoud na Erick.

IRINGA MJINI
Makada 13 wamejitosa kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini.

Wamo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mahamudu Madenge.

Pia wamo Dk. Yahaya Msigwa, Nuru Hepautwa, Addo November Mwasongwe,  Adestino Mwilinge, Frank Kibiki, Aidani Kiponda,

Peter Mwanilwa, Fales Kibasa, Michael Mlowe na aliyetia nia ya kuwania urais, , Balozi Mstaafu Dk. Augustine Mahiga.

SHINYANGA MJINI
Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Stephen Masele, amekutana na upinzani mkali, baada ya makada sita wa CCM kujitokeza kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho.  

Wanaochuana na Masele ni Willy Mzanvas ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Shinyanga na Kamanda wa Vijana wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.

Wengine ni Dk. Charles Mlingwa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Siha; Hatibu Kazungu,Talla Mzeimana ,Abdallah Seni na Mussa Ngagara.

Wamo pia Hussein Fatu na Charles Shingino ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.

JIMBO LA KONGWA
Anayeongoza Jimbo la Kongwa kwa sasa ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai. Anakabiliwa na upinzani kutoka kwa makada nane hivyo kufanya idadi ya wanaogombea nafasi ya kuwakilisha CCM katika kuwania ubunge wa jimbo hilo kufikia tisa.

Makada hao ni Samwel Chimanyi, Dk. Eliezer Chilongano, Epafra Mtango, Paschal Mahinyila, Hussein Madeni, Simon Katunga na Joseph Palingo.

DODOMA MJINI
Kwa sasa anayewakilisha Jimbo la Dodoma mjini ni Dk. David Malole.

Jumla ya wapinzani 10 wanashindana ili kupata ridhaa ya CCM kugombea nafasi ya kuliwakilisha.

Pamoja na Dk. Mallole, wengine ni Anthony Kanyama, Anthony Mavunde, Emmanuel Kamara, Haidary Gulamali, Mohammed Mgoli, Muruke Muruke, Mussa Luhamo, Robert Mtyani na Steven Masangia.

JIMBO LA MTERA
Livingiston Lusinde, almaarufu Kibajaji ndiye mwakilishi wa Jimbo la Mtera kwa sasa.

Anakabiliwa na makada tisa, akiwamo mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela, Samwel Malecela.
Wengine wanaowania kumng’oa Kibajaji ni Richard Masimba, Essan Mzuri, Lameck Lubote, Dk. Michael Msendekwa na Philip Eliezer.

SAME MAGHARIBI
Jimbo la Same Magharibi nalo lina ushindani mkali. Waziri wa zamani wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo, atavaana na makada wenzake 13.

Waliojitosa kutaka kumng’oa Dk. Mathayo David ni John Chaggama, Daniel Mkemi, Alfred Ngelula, David Mawa, Amon Shahidi, Gerald William, Katery Daniel, Yusuph Singo, Michael Mrindoko, Ahadi Kakore, Jordan Mmbaga na Mwalimu John Singo.

NKENGE
Katika Jimbo la Nkenge makada sita watachuana ambao ni Mbunge wa zamani, Balozi Dk. Deodorus Kamara na Mbunge anayemaliza muda wake, Asumpta Mshama. Wengine ni Julius Rugemalira, Dk. Joachim Mazima, Dk. William Nyagwa na Frolence Kyombo.

MTAMA
Katika Jimbo la Mtama lililoachwa wazi na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, makada wanne wanachuana ambao ni Selemani Mathew Luhongo, Rukia Abdallah Mandindi, Ismail Selemani Mbuni na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) wa Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye.

CHATO
Katika Jimbo la Chato lililokuwa likiongozwa na mbunge aliyemaliza muda wake ambaye pia ni mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli, limepata washindani 13 waliochukua na kurejesha fomu.

Katibu wa CCM Wilaya ya Chato, Khamis Mkaruka, aliwataja washindani hao ni Dk. Medard Kalemani, Deusdedit Katwale, Simon Bulenganija, Alexus Kagunze, Abdallah Mussa na Ismail Luge.

Wengine ni Dk. Alphonce Chandika, Ng'aranga Magai, Majura Kasika, Nassoro Yahaya, Aman Abeid, Mkinga Babuna Michael Wanjara, huku Francis Fredrick akishindwa kurejesha.

BUKOBA VIJIJINI
Kwa upande wa Jimbo la Bukoba Vijijini, waliojitokeza kurudisha fomu ni aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo na waziri wa zamani wa  Nishati na Madini, Nazir Karamagi; Mbunge anayemaliza muda wake, Jasson Rweikiza na Nelson Sospeter.

SITTA- URAMBO 
Baada ya kutochukua fomu za kutetea kiti cha ubunge Jimbo la Urambo, Samuel Sitta, ameliacha jimbo hilo huku kinyang’anyiro kikiwa kwa wanachama wanne akiwamo mkewe, Magreth Sitta.

Wengine waliochukua fomu za kulitaka jimbo hilo ni Ally Maswanya, Filbert Macheyeki na Hamis Kalaye ambao wote wamechukua na kurejesha kupitia CCM.

BARIADI MASHARIKI
Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, ni miongoni mwa watia nia wanne waliochukua fomu na kurejesha katika jimbo jipya la Bariadi.

Wengine waliochukua na kurejesha fomu hizo ni Masanja Kadogosa, Cosmas Chenya na Joram Masanja, ambao wote wanawania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, Katibu wa chama hicho mkoa wa Simiyu, Hilda Kapaya, alisema hao ni miongoni mwa wanachama 44 wa chama hicho waliochukua fomu katika majimbo yote saba ya mkoa huo, kati yao 11 kwa ajili ya viti maalum.

 NYAMAGANA
Makada 17 wamejitosa kuwania Jimbo la Nyamagana,  jijini Mwanza.

MGOMBEA AZIMIA
Mgombea ubunge kupitia CCM katika Jimbo la Peramiho, Lazaro Bunungu, ameanguka ghafla chooni nyumbani kwake eneo la Seedfarm, Manispaa ya Songea wakati alipokuwa ameenda kujisaidia.

 Habari zilizopatikana jana mjini Songea ambazo zimedhibitishwa na mke wake Judith Mlelwa, zilisema kuwa tukio hilo lilitokea  jana saa 5:00 asubuhi nyumbani kwake na kwamba baada ya kuona  hali yake ni mbaya walilazimika kumkimbiza hospitali kwa matibabu.

 “Leo (jana) asubuhi aliamka akiwa salama na baada ya kupata kifungua kinywa alikwenda kwenye ofisi za CCM wilaya ya Songea kuangalia ratiba ya kampeni ya uchaguzi ndani ya chama katika kata ya Maposeni Peramiho.” alisema.

 Mlelwa alisema baada ya kutokea tukio hilo waliwasiliana na Katibu wa CCM wilaya ya Songea kumjulisha kuwa Bunungu hali yake ni mbaya baada ya kuanguka chooni.

 Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Rajabu Uhonde aliiambia NIPASHE kuwa ofisi yake imepokea taarifa za tukio hilo na kwamba kwa sasa wanasubiri utaratibu wa kwenda kumuona licha ya kuwa wameambiwa alikuwa anafanyiwa mpango wa kusafirishwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Uhonde alifafanua zaidi kuwa katika jimbo la Peramiho makada watatu akiwamo aliyekuwa waziri wa wizara ya sera na uratibu Bungeni Jenista Mhagama walichukua fomu kwa ajili ya kugombea ubunge kwenye jimbo hilo lakini mmoja kati ya hao fomu yake ilikatwa kwa kuwa haikusainiwa na mgombea.

 Aliwataja waliochukua fomu kwenye jimbo hilo kuwa ni Jenista Mhagama, Razalo Bunungu ambaye ni mtumishi wa Tanroads Tanga na mfanyakazi wa Bank ya NMB tawi la Tunduru Cremence Makabuli Mwinuka  ambaye fomu yake ilitupiliwa mbali kwa kosa la fomu yake ya kuomba kugombea ubunge kusainiwa na mtu mwingine.

 Hata hivyo Uhonde alisema kuwa licha ya kuwa mgombea Bunungu anaumwa ratiba ya kampeni inabaki kama ilivyopangwa na inatarajiwa kuanza leo asubuhi katika kata ya Maposeni Peramiho.

Imeandikwa na Daniel Limbe (Chato); Ahmed Makongo (Bunda); Anceth Nyahore (Shinyanga); Halima Ikunji (Tabora); Happy Severine (Simiyu); Shushu Joel (Busega); Rose Joseph (Mwanza)

JAMBO LEO
Wakamatwa na bunduki 15, risasi 53,Wakutwa Mkuranga na fedha taslamu sh milioni 170
SIKU chache baada ya Kituo cha Polisi Stakishari kuvamiwa na majambazi na kuua watu saba wakiwamo polisi wanne, operesheni ya Jeshi la Polisi iliyokuwa ikifanyika kuwasaka imepata mafanikio baada ya kuua majambazi watatu na kujeruhi wawili.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova zinaeleza kuwa majambazi hao waliuawa eneo la Tuangoma Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kutokea mapambano ya kutumia risasi na askari polisi Julai 17 mwaka huu.
Kova alisema mbali ya kuuawa kwa majambazi hayo pia walijeruhi wawili na kukamata bundiki 15 na risasi 53 kati yake 28 zilizoibwa Kituo cha Stakishari.
Alisema majambazi hao walinaswa katika eneo la Tuangoma wakati wakijiandaa kufanya uhalifu mwingine ndipo wasamaria wema wakatoa taarifa.
Kova alisema baada ya kupata taarifa kikosi maalum kilienda eneo hilo la tukio na kuweka mtego ili kuwanasa watu hao.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa kabla ya kuuawa kwa majambazi hayo, polisi walizingira Msikiti mmoja Mkuranga na kukamata watu kadhaa kuhusinana na tukio la uvamizi Stakishari.
Alisema kutokana na taarifa zilizokuwepo askari wa kikosi hicho walisimamisha watu watano waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki mbili, lakini walikaidi kusimama ndipo mapambano ya kurushiana risasi yalipoanza.
“Wakati mpambano huo ukiendelea watuhumiwa watano walikamatwa na kati yao walikuwa wamejeruhiwa na hivyo walifariki dunia wakiwa njiani kukimbizwa hospitalini,” alisema.
Alitaja majina ya waliokufa ni Abbas Hashim, Mkazi wa Mbagala, Yasini, Mkazi wa Kivule na Said, Mkazi wa Kitunda Kivule katika Kijiji cha Mandimkongo, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Kamishna huyo alisema watuhumiwa wawili waliobakia, mkazi wa Kijiji cha Mandimkongo Mkuranga na mkazi wa Mbagala Kimbangulile ambao walipatikana na kuhojiwa.
Pia, katika operesheni ya kuwasaka majambazi hao polisi walikamata bunduki aina ya SMG ambayo namba zake zilifutwa ikiwa na risasi 25.
Alisema katika mwendelezo wa operesheni hiyo Julai 19 zilipatikana habari za kuaminika kwamba silaha zilizoporwa Stakishari zimefichwa mkoa wa jirani wa Pwani katika sehemu isiyofahamika ambapo ni porini.
“Katika ufuatiliaji kundi kubwa linaloundwa na vikosi mbalimbali vya polisi lilienda Mkoa wa Pwani na kufanya msako, ambapo mafanikio yalionekana,” alisema.
Alisema katika Kijiji cha Mandimkongo Kata ya Bupu, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani katikati ya msitu baada ya taarifa za kuaminika kikosi maalum kilifukua ardhini bunduki 15 kati ya hizo saba ni aina ya SMG, nyingine saba ni aina ya SAR, Magazine moja ya SMG yenye risasi 28.
Kova alisema zote zimetambuliwa kwamba ni silaha za Kituo cha polisi Stakishari zilizoporwa Julai 12.
Alisema pia katika shimo hilo ilipatikana silaha moja aina ya Norinko ya kichana ambayo inafanyiwa uchunguzi kujua wapi ilipoibwa.
Kova alisema pia katika shimo hilo zilipatikana fedha taslim za Tanzania shilingi milioni 170 ambazo zilifungwa katika sanduku.
Vilevile, jeshi hilo lilifanikiwa kukamata pikipiki nne zilizokuwa zikitumiwa na majambazo hao kufanyia uhalifu.
Kutokana na tukio hilo, Kova ametangaza kiama kwa wafanyabishara wenye tabia ya kuuza pikipiki kubadilisha majina na kwamba ni kichocheo cha uhalifu.
Pia, Kova alitoa mwito kwa viongozi wa dini kutokubali nyumba za ibada kutumika kama sehemu ya kufanyia mazoezi au kuhifadhia silaha kutokana na kuwa kichocheo cha uhalifu.
Wakati huohuo jeshi hilo linawatafuta watuhumiwa wengine nane ambapo mmoja wapo ni kiongozi wa kundi la majambazi hao, ambaye ni mkazi wa jijini Dar es salaam.

NIPASHE
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana alikana kutoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwamba mtoto, hana akili na mpuuzi.

Askofu Gwajima alikanusha tuhuma hizo wakati akisomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo, alidai kuwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers, vilivyopo Kawe jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alitoa lugha ya matusi kwamba ‘mimi Askofu Gwajima nasema askofu Pengo ni mpuuzi mmoja yule, mjinga mmoja, amekula nini yule, sijui amekula nini yule mtoto hana akili yule’ alinukuu maneno hayo.

Alidai kuwa Askofu Gwajima alitoa maneno hayo yakufadhaisha dhidi ya Askofu Pengo na kwamba yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa Machi 27, mwaka huu mshtakiwa alifikishwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.

Ilidaiwa kuwa alifunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma hizo.

Hata hivyo, Askofu Gwajima alikana mashitaka hayo lakini alikiri majina yake, wadhifa wake, kuhojiwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kweli kanisa lake liko Kawe na kushitakiwa mahakamani hapo.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa unatarajia kuita mashahidi saba na watawasilisha vielelezo vitano.

Wakati huo huo, mahakama hiyo imepiga kalenda kusoma maelezo ya awali ya kesi inayomkabili askofu huyo na wenzake watatu, baada ya mshtakiwa wa nne kuwa mgonjwa.

Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Hakimu Dyansobela Agosti 10, mwaka huu.

Mbali na Gwajima wengine ni anayedaiwa kuwa mlinzi wake George Mzava,Yekonia Bihagaze  na Georgey Milulu. 

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Machi 29, 2015 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakimiliki bastola aina ya Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.

Alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 32 (1) na cha 34 (1)(2) na(3) cha sheria ya Silaha na Milipuko sura ya 223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.

Upande wa Jamhuri, uliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio Mzava akiwa na wenzake hao walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun. Washtakiwa walikana mashitaka yao kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana.
 NIPASHE
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimejigamba kwamba kimeweza kuzuia ‘mafuriko’ kwa mikono huku kikiwatakia kila la kheri baadhi ya makada wake waliotangaza kutogombea kupitia chama hicho pamoja na wale waliokihama na wanaotaka kukihama.

Mwishoni mwa wiki iliyopita waliokuwa madiwani jimbo la Monduli kupitia CCM mkoani Arusha, walitangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku wabunge wa viti maalum, Ester Bulaya na James Lembeli aliyekuwa Mbunge wa Kahama wakitangaza kutogombea kupitia chama hicho.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akizungumza na NIPAHE jana alisema CCM hakina uwezo wa kuzuia mtu anayetaka kukihama kwa sababu hiyo ndiyo demokrasia.

Aidha, Nape alisema vyombo vya habari vilimnukuu aliyekuwa mgombea urais kupitia CCM, Edward Lowassa akisema kuwa watu hawawezi kuzuia ‘mafuriko’ kwa mikono na kwamba CCM imeweza kufanya hivyo, lakini habari hizo haziandikwi.

Alisema wanachama wanaotaka kuhama hawawezi kuzuiwa kwa namna yoyote na kwamba hilo ni jambo la kawaida kufanyika kwa kada yoyote.

Akizungumzia mchakato wa kumpata mgombea urais, ulivyokuwa ndani ya CCM, alisema ulifuata utaratibu na kanuni zote na kwamba kama maneno mengi yataendelea kusemwa atatoa video inayoonyesha kila kitu kilivyokuwa ndani ya kikao cha Kamati Kuu (CC).

Kuhusu makada waliokihama chama hicho na kujiunga na CCM, Nnauye alisema baada ya Baraza la Madiwani kuvunjwa hapakuwa tena na wawakilishi wa aina hiyo.

Alisema watu waliojiunga na Chadema huko Monduli mkoani Arusha hawakuwa Madiwani kwa kuwa Baraza la Madiwani likishavunjwa hakuna tena nafasi hizo za uwakilishi.




TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top