Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

NIMEKUWEKEA STORY KUBWA ZILIZOVUTA HISIA ZA WATU MAGAZETI YA LEO TANZANIA

TANGAZO
MWANANCHI
Baada ya mchakato wa kuwania urais, sasa vita ya Uchaguzi Mkuu imehamia kwenye ubunge na udiwani hasa kutoka katika vyama vikubwa vya CCM kinachotawala na Chadema kinachoongoza upinzani.
Hadi jana, ambayo ilikuwa ni siku ya mwisho kwa vyama hivyo kuchukua na kurejesha fomu, jambo moja lilijidhihirisha katika baadhi ya majimbo kwa upande wa CCM; baadhi ya majina makubwa katika siasa za ubunge yanachuana hivyo kufanya mchakato wa kumpata mteule mmoja kuwa mgumu.
Mchuano huo na kuimarika kwa Chadema mikoani hasa kutokana na majeraha ya mchakato wa urais ndani ya CCM, vinaufanya upinzani wa kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuwa sawa na vita.
Nzega Vijijini
Makada wawili wa chama hicho, Lucas Selelii na Dk Hamisi Kigwangalla wamechukua fomu kuwania ubunge wa Nzega Vijijini.
Katika uchaguzi uliopita wa 2010, makada hao walivaana katika Jimbo la Nzega lakini wote wakaangushwa na Hussein Bashe aliyeibuka wa kwanza akifuatiwa na Selelii.
Hata hivyo, matokeo hayo yalibatilishwa na Halmashauri Kuu ya CCM na kumchukua Dk Kigwangalla aliyekuwa mshindi wa tatu.
Mgawanyo wa majimbo uliofanywa wiki iliyopita na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), umerahisisha mpambano wa makada hao, hivyo wawili hao wakamwachia Bashe Nzega Mjini. 
Akichukua fomu hiyo jana, katika ofisi za CCM za Wilaya ya Nzega, Dk Kigwangalla akiwa ameambatana na wazee wa jimbo hilo, alisema shinikizo la kugombea Nzega Vijijini limetoka kwa wananchi wanaotambua umuhimu wake.
Selelii aliyekuwa Mbunge wa Nzega kwa miaka 15 hadi 2010, alichukua fomu kimyakimya bila kuzungumza na vyombo vya habari.
Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega,  Empimark Makuya alithibitisha kuwa kada huyo alishachukua fomu. Wawili hao watakabiliana na upinzani mkali kutoka kwa wengine wawili waliochukua fomu, John Dotto na Paul Kabelele.
Maiga aibukia Iringa
Baada ya kukwama katika harakati za kuwania urais kupitia CCM, Balozi Dk Augustine Mahiga amejitokeza kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini.
Dk Mahiga aliyechukua fomu jana na kurudisha, atapambana na Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Jesca Msambatavangu, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela na mwandishi wa habari, Frank Kibiki ambao tayari wamechukua na kurejesha fomu zao.
Mchuano katika jimbo hilo unatarajiwa kuwa mkali wakati na baada ya kura za maoni ndani ya CCM hasa ikizingatiwa kwamba Mwakalebela alikuwa amechukua namba moja katika kura za maoni za chama hicho mwaka 2010 kabla ya jina lake kukatwa na NEC.
Mshindi atakuwa na wakati mgumu kukabiliana na kishindo cha upinzani hasa kutoka Chadema ambako Mchungaji Peter Msigwa aliyeshinda katika uchaguzi uliopita, jana alipokewa na umati mkubwa wa watu alipowasili mjini hapo.
Profesa Maghembe na Thadayo tena
Mshikemshike mwingine unatarajiwa kuibuka katika Jimbo la Mwanga ambako Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe anatarajiwa kupambana tena na hasimu wake mkubwa katika kiti hicho, Joseph Thadayo.
Katika uchaguzi wa 2010, Profesa Maghembe alimshinda Wakili huyo ambaye alionekana kuungwa mkono na wanasiasa wengine wenye nguvu katika jimbo hilo. Mbali yao wengine waliojitokeza ni Aminieli Kibali na Karia Magaro.
Wasira, Bulaya wavaana
Mchuano mwingine mkali unatarajiwa kuwapo katika Jimbo la Bunda Mjini ambako Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira atavaana na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya.
Wabunge hao wa CCM wamekuwa wakitambiana muda mrefu na wakati mwingine waliwahi kurushiana maneno hadi bungeni, lakini mwisho wa tambo zote ni kwenye kura za maoni.
Mamia warejesha fomu
Hadi muda wa mwisho wa kurejesha fomu unakamilika saa 10 jioni jana, mamia ya makada wa Chadema na CCM walikuwa wamejitokeza na kudhihirisha kuwa mchuano utakuwa mkali katika kura za maoni na hata kwenye uchaguzi wenyewe.
Kawe 22: Elias Nawera, Dk Walter Nnko, Jumaa Muhina, Kippi Warioba, Atulinda Barongo, Tegemeo Sambili, Kiganga George, Edmund Lyatuu, Charles Makongoro Nyerere, Mtiti Butiku, Yusuf Nassoro, John Mayanga, Dickson Muze, Dk Wilson Babyebonela, Colman Massawe, Amon Mpanji, Amelchiory Kulwizira, Gabriel Mnasa, Abdallah Majura na Jerry Murro, wote wakikabiliana na Halima Mdee aliyejitokeza pekee Chadema, hasa iwapo atasimama pekee kupitia Ukawa.
Kinondoni 12: Idd Azan, Wagota Salum, Tonny Kalijuna, Goodchange Msangi, Emmanuel Makene, Lusajo Willy, Mage Kimambi, Mussa Mwambujule, Stevew Nengere (Steve Nyerere), Joseph Muhonda, Michael Wambura na Macdonald Lunyiliga.
Ubungo 12: Vincent Mabiki, Timoth Machibya, Jordan Baringo, Emmanuel Mboma, Zangina Zangina, Kalist Ngalo, Hawa Ng’umbi, Jackson Millengo, Didas Masaburi, Joseph Massana, wote wa CCM wakitarajiwa kumkabili John Mnyika wa Chadema.
Ilala watatu: Mussa Azzan Zungu, Mrisho Gambo na Waziri Kindamba.
Ukonga 16: Jerry Silaa, Jacob Katama, Hamza Mshindo, Frederick Rwegasira, Anthony Kalokola, Ramesh Patel, Peter Majura, Amina Mkono, Edwin Moses, Robert Masegese, John Bachuta, Edward Rabson, Nickson Tugale, Elly Ballas, Asia Msangi, Lucas Otieno, Fredrick Kabati, Mwanaidi Maghohe, Mwita Waitara, Deogratius Munishi, Deogratius Kalinga, Deogratius Mramba, Salanga Kimbaga, James Nyakisagana, Lameck Kiyenze na Gaston Makweta.
Segerea 13: Zahoro Lyasuka, Apruna Humba, Bona Kalua, Nicholaus Haule, Baraka Omary, Benedict Kataluga, Dk Makongoro Mahanga na Joseph Kessy.
Kigamboni 10: Aron Othman, Kiaga Kiboko, Abdallah Mwinyi, Dk Faustine Ndugulile, Ndahaye Mafu, Flora Yongolo, David Sheba, Mohammed Ally Mchekwa, Khatib Zombe na Adili Sunday.
Mbagala 23: Lucas Malegeli, Mindi Kuchilungulo, Kazimbaya Makwega, Adadius Richard, Tambwe Hiza, Issa Mangungu, Ingawaje Kajumba, Siega Kiboko, Peter Nyalali, Mwinchumu Msomi, Dominic Haule, Aman Mulika, Banda Sonoko, John Kibasso, Ally Makwiro, Alvaro Kigongo, Maesh Bolisha, Kivuma Msangi, Deus Sere, Abdulrahim Abbas, Salum Seif Rupia, Ally Mhando, Fares Magessa, Stuwart Matola.
Moshi: Priscus Tarimo, Amani Ngowi, Patrick Boisafi, Davis Mosha, Buni Ramole, Halifa Kiwango, Michael Mwita, Daud Mrindoko, Shanel Ngunda, Innocent Siriwa, Edmund Rutaraka, Omari Mwariko, Basil Lema, Jaffar Michael na Wakili Elikunda Kipoko.
Busokelo:  Suma Mwakasitu , Dk Stephen Mwakajumilo, Ezekiel Gwatengile, Mwalimu Juma Kaponda, Ally Mwakibolwa, Issa Mwakasendo, Aden Mwakyonde na Lusubilo Mwakibibi.
Kilombero: Kanali mstaafu Harun Kondo, Vitus Lipagila, Abdullah Lyana, Oscar Mazengo,  Japhet Mswaki, Paul Mfungahema, John Guninita, Abubakari Asenga na Abdul Mteketa.
Mlimba: Dk Frederick Sagamiko, Senorina Kateule, Godwin Kunambi, Augustino Kusalika, George Swevetta, Castor Ligallama, Profesa Jumanne Mhoma, Fred Mwasakilale, Dismas Lyassa.
Namtumbo: Edwin Ngonyani, Edwin Milinga, Mwinyiheri Ndimbo, Vita Kawawa, Anselio Nchimbi, Julius Lwena, Fitan Kilowoko, Balozi Salome Sijaona, Mussa Chowo, Salum Omera, Ally Mbawala na Charles Fussi.
Tunduru Kaskazini: Mhandisi Ramo Makani, Omary Kalolo, Michael Matomola, Hassan Kungu, Issa Mpua, Rashid Mandoa, Athuman Mkinde, Shaban Mlono na Moses Kulawayo.
Tunduru Kusini: Abdallah Mtutura, Daim Mpakate na Mtamila Achukuo.
Nyasa: Christopher Chale, Bethard Haule, Adolph Kumburu, Alex Shauri, Frank Mvunjapori, Dk Steven Maluka, Stella Manyanya, Cassian Njowoka, Jarome Betty na Oddo Mwisho.
Serengeti: Dk Stephen Kebwe, Dk James Wanyancha, Juma Kobecha na Mabenga Magonera.
Sumbawanga Mjini: Aeshi Hilaly, Anyosisye Kiluswa, Fortunata Fwema, Mathias Koni, Gilbert Simya, Frank Mwalembe, Selis Ndasi, Mbona Mpaye, Sospeter Kansapa, Paschal Sanga na Victor Vitus.
Korogwe Vijijini: Stephen Ngonyani (Profesa Majimarefu), Cesilia Korassa, Allan Bendera, Ali Mussa Moza, Abdallah Nyangasa, Christopher Shekiondo, Andrew Matili, Edmund Mndolwa, Ernest Kimaya, Peter Mfumya na Stephen Shetuhi.
Kilindi: Beatrice Shellukindo, Abdallah Kidunda, Fikirini Masokola na Dk Aisha Kigoda.
Bariadi Mashariki: Masanja Kadogosa na Joram Masaga.
Mbulu: Mary Margwe amechukua fomu ya kugombea ubunge wa viti maalumu
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye na yule wa Kilosa Kati, Mustafa Mkulo hawakujitokeza kuchukua fomu.
Imeandikwa na Julius Mathias,  Bakari Kiango, Godfrey Kahango, Ngollo John, Salim Mohammed, Joseph Lyimo, Faustine Fabian, Joyce Joliga, Daniel Mjema, Burhani Yakub, Antony Mayunga, Mussa Mwangoka na Mustapha Kapalata

MWANAHALISI:
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Dream Success Enterprises, waasisi wa Tuzo ya Shujaa Kati Yetu, wamewatunuku tuzo Saed Kubenea, David Kafulila na Vick Mtetema kwa mchango wa kazi zao zilizotukuka katika maendeleo na ujenzi wa taifa. 
Kubenea, mwandishi wa habari za uchunguzi, mmiliki wa mtandao wa MwanaHALISI Online na gazeti la MwanaHALISI lililosimamishwa na serikali kwa muda usiojulikana ametunukiwa tuzo ya “Uwazi na Ukweli.” 
Naye Kafulila, mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR – Mageuzi), ametunukiwa tuzo ya “Maono Mapevu,” huku Mtetema, akitunukiwa tuzo ya “ubunifu.”
Mtetema ni murugenzi mtendaji wa shirika la Under The Same Sun, linalofanya kazi za utetezi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Kafulila ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na kuibua na kusimamia ufisadi wa zaidi ya Sh. 300 Bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ndani ya Bunge la Jamhuri.
Tuzo hizo zinalenga katika kuleta mapinduzi ya kimaadili na kifikra nchini.
Akizungumza wakati akikabidhi tuzo hizo jijini Dar es Salaam, mwasheria mkuu wa kwanza nchini, Jaji Mark Bomani, alisema ni heshima kubwa kwake kutoa tuzo kwa Kubenea, Kafulila na Mtetema, kutokana na machango wao mkubwa kwa taifa.
“Ni watu makini. Wanafanya kazi nzuri kwa taifa lao. Kubenea amefanya kazi nzuri. Gazeti lake ni moja ya magazeti yanayoandika na kusema ukweli bila kuogopa, kujipendekeza, kutoonea wala kupendelea. Hicho ndicho kinachohitajika,” amesema Jaji Bomani.
“Kafulila ni mbunge kijana, lakini ametoa mchango mkubwa katika kutetea rasilimali za taifa kwa kufichua maovu yanayoendelea serikalini. Kazi ambayo inahitaji uelewa, umakini, ujasiri na kusema kweli,” ameeleza.
Naye Mtetema, Jaji Bomani amesema, amejitolea kutetea na kuzungumzia kwa undani suala la mauji ya Albino, hali inayotia moyo mapambano hayo.
Amesema, “Wote ambao wamejitahidi kufikisha ujumbe kwa wananchi, lazima wapongezwe na kupewa tuzo kwa jitihada zao. Juhudi kubwa ifanyike kuwasaka wengine mabao wamejitahidi kufichua maouvu ili nchi iwe ya amani.
“Tumezoea kuona watu wakitunukiwa Tunu za taifa kila mwaka katika sherehe za Muungano au Uhuru. Hiyo haitoshi. Hizo ni kazi za serikali. Lazima na watu nao wawe na vyombo vyao ambavyo vinawatambua watu ambao wasingetambukika huko serikalini,” amesema.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo,  Kubenea amesema, “…nikiri kwamba nilishutuka sana nilipopata taarifa ya kutunukiwa tuzo hii.”
Alisema, “tuzo hii, ni faraja kwangu. Sijutii kuwa mkweli. Gazeti langu la MwanaHALISI limefungiwa na serikali. Jingine linaweza kufungiwa kesho. Karamu yangu inaweza kuvunjwa. Mdomo wangu unaweza kuzibwa, lakini sitanyamaza.”
Ameifananisha jina la tuzo hiyo la “Uwazi na Ukweli” na kauli ya serikali ya awamu ya tatu ambayo amesema, “…baadae iligeuka na kuficha ukweli na kukumbatia usiri.”
“Nyumba zote za serikali zimeuzwa katika kipindi ambacho serikali hii, ilikuwa madarakani. Mgodi wa Kiwila, nyumba za serikali kwa wasiostahaili na kwa bei ya kutupwa, mashamba ya mkonge, ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania na Benki (NBC).
Kwa upande wake Kafulila amesema, “…nimejisikia fahari kubwa kuwa miongoni mwa watu ambao wamechangia chochote katika taifa letu, hata kupewa tuzo hii. Nikifa kesho duniani wanangu, wajukuu, ndugu zangu na watu wengine watanikumbuka kwamba nilifanya chochote.”
Naye Kafulila amesema, “taifa letu lina tatizo kubwa la watu kukosa uadilifu na kujaa uoga. Hii inatokana na ukosefu wa bidii na maarifa….nachoweza kuwaahidi watu, nitaendelea kuwatumikia. Nakwenda kugombea tena. Nikishidwa, nikishinda sitoacha kutumikia nchi yangu.”
Kwa upande wake, Vicky Mtetema amesema, “….ni heshima kubwa kutunukiwa hii tuzo. Vitendo vya albino kuuwawa vinakithiri wakati huu wa uchaguzi. Naomba nimteue David Kafulila awe baba na kuwasemea watu wenye albinism bungeni,”
Mtetema amemtaka Kafulila kama atafanikiwa kuchaguliwa katika Bunge la 11 kuhakikisha kunakuwepo na sera ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), Sheria ya kuwaondoa wanganga wanaopiga ramli na mazingira mazuri kwa Albino.
Joshua Lawrence, afisa mikakati toka Dream Success Enterprises amesema maendeleo ya taifa lolote duniani hutengenezwa na raia na viongozi wenye habari, maarifa na maono sahihi. Na ili kufanikisha hayo, uhuru wa kupata habari ndani ya muktadha ni muhimu kuwepo.
“Na, hili linawezekana tu pale raia wanaopewa uhuru wa kuogelea ndani ya bahari ya fikra huru, huku muktadha wa sheria zinazolinda kingo za uhuru huo ukiwa ni kuzinawilisha fikra pevu na kuzinyong’onyeza fikra bwete, wala si vinginevyo,” amesema Lawrence.
Amesema hiyo ni awamu ya pili tuzo hizo kutolewa. Awamu ya kwanza ilikuwa 22 Disemba, mwaka 2014 ambapo Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh alitunukiwa.
MWANANCHI:
Dar es Salaam. Wanasiasa wa upinzani nchini wamepinga kitendo cha mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kutumia ndege ya Serikali kwenye shughuli za kichama za kujitambulisha wakisema hatua hiyo ni matumizi mabaya ya rasilimali za Taifa.
Dk Magufuli, juzi alikwenda Mwanza kwa ziara maalumu ya kujitambulisha akitumia ndege ya Serikali aina ya Fokker F28, jambo ambalo limeibua hisia tofauti.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Kapteni Keenan Mhaiki alisema kitendo cha CCM kutumia ndege ya Serikali hakivunji sheria na taratibu zozote kwa kuwa mbali na kusafirisha viongozi wa Serikali, pia wanaruhusiwa kufanya biashara kwa kuhudumia umma.
Pia, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema walifuata taratibu zote kuikodi ndege hiyo na kwamba chama chake ni kikubwa na hakiwezi kushindwa kukodi usafiri huo.
“Ile ni ndege ya Serikali, yeyote anayetaka kuitumia aende kulipia tu, atapewa. Sisi tumekwenda kama wateja wa kawaida tukalipia, ukitaka kujua ni kiasi gani kawaulize wahusika watakueleza,” alisema Nape.
Kuhusu suala hilo la gharama, Kapteni Mhaiki alisema gharama ya kukodi ndege hizo zipo tofauti kutokana na aina inayohitajika akisema aliyoitumia Dk Magufuli inagharimu Dola za Marekani 4,000 sawa na Sh8.4milioni kwa saa moja.
Akizungumzia suala hilo jana, Kiongozi wa chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe alisema viongozi wa Serikali wamekuwa na utamaduni wa kutumia mali za umma kwa shughuli za kisiasa na kusahau kwamba rasilimali hizo ni za Watanzania wote bila kujali itikadi zao.
Zitto na Mbowe
Zitto alisema jambo hilo halijaanzia kwenye ziara ya Dk Magufuli, bali hata mawaziri wote waliochukua fomu walitumia magari ya Serikali kuzunguka nchi nzima kutafuta wadhamini wao kwa nafasi ya urais.
“Jambo hili si kwa CCM pekee, tunaona pia gari la Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB), likitumika kwenye mikutano yake ya kichama. Lile ni gari la Serikali; kwa hiyo lazima tuupige vita utamaduni huu,” alisema Zitto. Alisema CCM ina wajibu wa kuwaeleza Watanzania sababu za kutumia ndege ya Serikali na kama wamelipia fedha ni kiasi gani kilicholipwa huku akisisitiza kuwa utamaduni huu uliokithiri unaligharimu Taifa.
“Mali za umma lazima zitumike kwa shughuli za Serikali na siyo shughuli za kichama. Hili halina upinzani wala CCM, ni jambo linalotakiwa kupigwa vita kwa nguvu zote ili rasilimali zetu zitumike ipasavyo,” alisisitiza kiongozi huyo.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema limekuwa ni jambo la kawaida kwa CCM kutumia vyombo vya Dola katika kufanikisha mambo yao na kwamba sababu za kwamba ndege za Serikali zipo wazi kwa umma ni ‘danganya toto’ ili kufurahisha wananchi.
“Eti ndege hizo zinaweza kukodiwa na mtu binafsi au chama, nani kakwambia? Nenda kakodi kama utapata. Ukweli ni kwamba Magufuli hakuikodi hiyo ndege, kama ni kweli wamekodi watuonyeshe walilipaje?” alihoji Mbowe na kuongeza. “Chadema haijawahi kwenda kukodi kwa sababu ina uhakika haitaipata, hasa ikizingatiwa “viwanja tu vya michezo vinavyomilikiwa na CCM havijawahi kutolewa vitumike kwa mikutano ya upinzani tangu mfumo wa vyama vingi uanze zaidi ya miaka 20 iliyopita.”
Mwenyekiti huyo wa Chadema, alisema hata polisi, mahakama na vyombo vya habari vya Serikali vimekuwa vikitumika vibaya kuilinda CCM iendelee kukaa madarakani.
Alipoulizwa juu ya gari la Serikali analotumia kuonekana kwenye mikutano yake ya kisiasa alijibu:  “Nilipopewa gari na Serikali lilikuwa ni kwa matumizi ya upinzani, mikutano ya kisiasa ninayohudhuria ni sehemu ya kazi za upinzani… sasa wanaohoji walitegemea nitalitumia gari hilo kwa ajili ya Serikali? Nenda kawaambie habari ndiyo hiyo na Bunge likivunjwa nitalirudisha.”
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Constatine Akitanda alisema ana shaka kubwa iwapo ndege hiyo ilikodiwa na CCM na kulipiwa gharama zinazotakiwa.
“Sisi tuna uhakika gani kuwa CCM walikodi? Hata hizo fedha tukisema twende tukaangalie je, ni kweli wamelipa au wamechukua tu hiyo ndege?… hata ukisema tukafanye ‘auditing’ (ukaguzi) hutakuta kitu pale,” alisema Akitanda.
Ufafanuzi wa wakala
Katika ufafanuzi wake, Kapteni Mhaiki alisema hakuna haja ya suala hilo kuchukuliwa kisiasa... “Jukumu la kwanza ni kubeba viongozi wa Serikali lakini kama kuna muda wa ziada tunawahudumia watu wengine kibiashara na huwa tunasafirisha hata timu za mpira na wageni kutoka nje ya nchi wanapotembelea nchini. “Mtu yeyote anaruhusiwa kuomba kuikodi, atapatiwa ankara yake… hata awe CUF, Chadema au chama chochote kile kama kuna nafasi anapata,” alisema.
 Alipoulizwa juu ya tuhuma za upendeleo kwa chama tawala hivyo kutoleta uwanja sawa wa ushindani, alijibu: “Upendeleo upi unaozungumza au unautaka?  Hata wewe mwandishi ukitaka tupigie simu ndege ikiwapo utapata.”
TGFA kwa sasa ina ndege nne ambazo ni Fokker F28 ya mwaka 1978 yenye usajili wa 5H-CCM, Piper PA-31 Navajo (1980, 5H-ILS), Fokker 50 (1992, 5H-TFG) na Gulfstream 550 ya mwaka 2004 iliyosajiliwa kwa namba 5H-ONE.
Kama mwaka 2010
Sakata la matumizi ya ndege ya Serikali lilishawahi kujitokeza mwaka 2010 wakati wa kampeni baada ya kumbeba mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma. Kitendo hicho kilimfanya aliyekuwa Meneja wa Kampeni kipindi hicho ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuonyesha risiti zilizotumika kulipia huduma za ndege hizo.

JAMBO LEO
SIKU chache baada ya kukatwa jina lake na Kamati ya Maadili na Usalama ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania urais kupitia chama hicho, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuwa wakati wa kuzungumza na Watanzania ukifika atasema.
Vilevile, amesema taarifa zinazoendelea kuenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hatima yake katika chama hicho ni za kuzipuuza.
Akizungumza na Jambo Leo jana kwa njia ya simu, Msemaji wa Lowassa, Abubakari Liongo alisema kuwa kuna taarifa nyingi zinazoendelea kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinamhusisha Lowassa.
Kauli hiyo ya Liongo imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa Lowassa anataka kujiunga na chama kimoja cha upinzani baada ya kukasirishwa na CCM kumkata jina lake mjini Dodoma.
Katika mchakato huo, majina matano yaliyopelekwa Kamati Kuu na Kamati ya Maadili ni Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali.
Majina hayo yalipelekwa Mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ambayo iliyachuja na kubakiza matatu, ambayo ni Dk Magufuli, Dk Migiro na Balozi Amina.
Majina hayo yalupelekwa mkutano mkuu ambao uliyapigia kura na Dk Magufuli akaibuka kidedea.
Liongo alisema hakuna ukweli wowote na iwapo kiongozi huyo atataka kuzungumza na vyombo vya habari atatoa taarifa rasmi.

Hivyo Liongo alisema wakati ukifika na Lowassa akamua kuzungumza na Watanzania atazungumza, lakini taarifa ambazo zinaendelea sasa kwenye mitandao ni za kuzipuuza.
Aliwaambia Watanzania kuwa taarifa hizo zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha sintofahamu hazitoki kwa Lowassa ,hivyo ni vema kuzipuuza na alilisitiza iwapo kutakuwa na taarifa yeye ndiyo mhusika mkuu.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba Watanzania kupuuza taarifa zinazosambazwa kuwa mheshimiwa anahamia Chadema.Kama Lowassa kuna jambo anataka kuzungumza tutawaita waandishi wa habari na ataongea kila kitu,”alisema Liongo.
Alisema hilo la kudai kuwa Lowassa anafanya mkutano na waandishi wa habari limechukua muda sasa, lakini ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho na kama atafanya hivyo itaelezwa , hivyo kinachotakiwa ni subira.
Azungumzia 4U Movoment
Kuhusu kundi la 4U Movement lililokuwa linamuunga mkono Lowassa katika harakati za kuwania urais kupitia CCM ambalo limeamua kwenda upinzani baada ya jina la kiongozi huyo kukatwa, Liongo alisema hawezi kuzungumzia kundi hilo, kwani halipo chini ya ofisi yake.
Kundi hilo juzi lilitangaza rasmi kuhamia upinzani huku likimshawishi na Lowassa naye kuhamia huko.
“Kundi hilo lipo kwa ushabiki, hivyo hatuwezi kuzungumzia wanayoendelea kufanya hivi sasa.Kundi hilo limeamua kuwa upande wa Lowassa kwa upendo wao,”alisema Liongo.
Alisisitiza huenda yanayofanywa na kundi hilo ni sehemu ya upendo wao, lakini siyo agizo kutoka ndani ya ofisi ya Lowassa.
Nbali ya 4U Movement kuamua kuhamia upinzani pia juzi madiwani 19, wenyeviti wa vijiji na wanachama wa CCM Wilaya ya Monduli mkoa ni Arusha walitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake juzi aliyekuwa Diwani wa kata ya Lepupurko Julius Kalanga wameamua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na dhuluma ndani ya CCM.
Wakati kwa upande wa Mtaribu wa 4U Movement Hemed Ally alisema kundi hilo lina wanachama takribani milioni 8.5, hivyo wakiamu kupeleka kura zao upande wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni wazi kuwa CCM itaanguka.
MAJIRA:
WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amekataa ombi la wananchi wa Jimbo la Katavi waliomtaka agombee tena ubunge wa jimbo hilo ili kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo aliyoianzisha.

Bw. Pinda alitoa msimamo huo jana baada ya kutoka kwenye Ibada ya Jumapili katika Kigango cha Kanisa Katoliki Kibaoni wilayani Mlele, mkoani Katavi.

Alisema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane akiamini wakati umefika wa yeye kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa jimbo hilo.

Aliongeza kuwa, ataendelea kuwa karibu na wananchi wa Katavi wakati wote kwani atakuwa na muda wa kutosha hivyo atashiriki kikamilifu katika mikakati mbalimbali ya kuwaletea maendeleo ili waweze kujikwamua kutoka kwenye umaskini.

Aliwataka wakazi wa jimbo hilo kuwa makini katika kuchagua mbunge na madiwani akisema kamwe watoa rushwa na wabadhirifu wasipewe nafasi katika uchaguzi ujao.

Akimshukuru Bw. Pinda, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani humo, Padri Aloyce Nchimbi, aliwaasa wananchi kumuenzi Waziri huyo hata akistaafu kwani bado watahitaji busara na uzoefu wake katika kujiletea maendeleo.

Bw. Pinda yuko kijijini kwake Kibaoni, wilayani humo kwa ajili ya mapumziko mafupi ambapo jana jioni ndiyo mwisho wa kurejesha fomu za ubunge ndani ya chama hicho.


TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top