TANGAZO
Bomba Kuu la Gesi Litakalotumika Kusafirishia Gesi Kutoka Madimba Mkoani Mtwara hadi Kinyerezi Mkoani Dar es salaam.
HABARI LEO:
MRADI wa bomba la gesi kutoka Mtwara
mpaka Dar es Salaam umekamilika na wiki ijayo gesi itakuwa na uwezo wa kufika
jijini Dar es Salaam.
Aidha kazi ya kufua umeme
kwa kutumia gesi asilia na kuuingiza katika mifumo ya Shirika la Umeme nchini
(TANESCO) itaanza mwezi ujao.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa
Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Kapuulya Musomba juzi wakati bodi ya
shirika hilo ilipofanya ziara ya kutembelea mradi huo kwa lengo la kujionea
hali halisi kabla ya gesi kuanza kusafirishwa kutoka Mtwara kuja Dar es alaam.
Musomba alisema kwamba
Agosti mosi mwaka huu, gesi itakuwa na uwezo wa kufika katika mitambo ya
kuzalisha umeme ya Kinyerezi One na Tegeta, Dar es Salaam.
Alisema licha ya kuwa na
uwezo wa kufika wiki ijayo, lakini wanatarajia gesi kwa ajili ya kufua umeme
kufika katika mitambo hiyo Septemba 6 au 7 kutokana na hoja za kitaalamu za
hatua ya mwanzo ya kuchakata na kusafirisha gesi.
Sehemu ya Kiwanda Cha Kuchakata Gesi Kilichopo katika eneo la Madimba Mkoani Mtwara.
Musomba alisema hayo akiwa katika kituo
cha Somanga Fungu ambapo kuna mitambo maalumu ya kupokea gesi kutoka Songosongo
na Mtwara, kisha kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam. Alisema hatua hizo
zinafuatwa kwa siku 45 ili kuhakiki vifaa vyote kuwa havina tatizo kuanzia
kuchimba, kuchakata na hata kusafirisha.
Alisema baada ya majaribio
hayo ya kupeleka gesi Dar es Salaam kufanikiwa, Septemba 15 wataanza kuingiza
umeme uliozalishwa kwa gesi asilia Tanesco ili watanzania waanze kuona matunda
ya gesi na bomba lenyewe.
“Kwa sasa Tanesco wana
mitambo ya kuzalisha megawati mia mbili za umeme, lakini hazifanyi kazi hivyo
sisi tutaanza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi na kuingiza Tanesco megawati mia
moja hamsini za umeme”alisisitiza Alisema tayari mpaka sasa wameshaajiri
wafanyakazi 30 katika vituo vya mitambo ya Kinyerezi na 11 Somanga Fungu tayari
kwa kuanza usafirishaji na uzalishaji katika mitambo.
Madimba Mkoani Mtwara
Alisema katika bomba hilo la kilometa
504 ambazo ni umbali wa mradi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam una valvu zaidi
ya 100, lakini kuu zipo 16 na kukitokea tatizo kwenye valvu zinafungwa kwa
ajili ya usalama.
Akizungumzia suala la
usimamiaji wa usalama katika bomba hilo, alisema wameweka mikakati mbalimbali
ikiwemo kuajiri watu wenye utaalamu wa ulinzi.
Pia alisema katika usalama
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo hofu ya ugaidi inayozidi
kuongezeka, huku wakitumia vifaa vya kisasa katika ulinzi wa bomba hilo pamoja
na kushirikisha wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi wa
shirika hilo, Michael Mwanda alisema anajivunia sana kukamilika kwa mradi huo
na kufikia hatua ya watanzania kuanza kuona matunda yake kwani awali kulikuwa
na maoni na vipingamizi mbalimbali.
Alisema wameona na kuridhishwa na
utendaji wa wataalamu wa ndani na nje ya nchi kwa ujenzi wa bomba hilo hivyo
viwanda vitaongezeka kwa kuwa na umeme wa uhakika jambo litakaloongeza
uzalishaji wa bidhaa pamoja na ajira.
Akizungumzia kushuka kwa
gharama za umeme, Mwanda alisema anavyoona yeye kutakuwa na unafuu kwani sasa
Tanesco wataoondokana na kuzalisha umeme kwa kutumia mitambo inayotumia mafuta.
Mradi huo umegharimu pesa za Marekani Dola bilioni 1.2 sawa na fedha za
Tanzania zaidi ya Sh trilioni 2.4.
Inaelezwa kuwa kukamilika
kwa mradi huo kutaokoa zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja sawa na Sh
trilioni 2 kwa mwaka, fedha ambazo zinatumika sasa kuagiza mafuta kwa ajili ya
kufua umeme kwa kutumia mitambo ambayo tayari ipo nchini.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD